TARURA MUSOMA : BARABARA YA SHABANI ITAWEKEWA LAMI
Na Jovina Massano, Musoma
MENEJA wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Musoma mkoa wa Mara Mhandisi Joseph Mkwizu, amesema Barabara ya Shabani iliyopo Kata ya Kitaji iliyofanyiwa matengenezo kwa kiwango cha changarawe ipo kwenye mpango wa kutengenezwa kwa kiwango cha Lami kupitia mradi wa Benk ya Dunia.
Akizungumza na Mwandishi wa DIMA Online Mhandis Joseph amesema barabara hiyo itatengenezwa kwa kiwango cha lami ambapo muda wowote ndani ya mwezi huu wa Oktoba, 2022 watafanya usanifu pamoja na barabara nyingine Manispaa ya Musoma.
"Barabara hii ni ya muda mrefu ilikuwa imefika ukomo wa maisha yake na tulipokea malalamiko kwa wananchi wa eneo hilo waliomba ifanyiwe marekebisho ili ipitike kutokana na hali ya mashimo yaliyokuwepo hivyo tuliamua kuirudisha kwenye hali ya zamani ya changalawe ili ipitike ikiwa ni suluhisho la muda mfupi wakati huo tukisubilia kutengeneza kwa kiwango cha lami, hilo ndilo tumelifanya kwa sasa hivi.
" Tupo kwenye hatua ya kukamilisha baada ya hapo tutasubiri mradi mkubwa wa lami, tutaiwekea lami na utekelezaji wake utafanywa na benki ya dunia kwa mwaka wa fedha 2023/2024 lakini mwezi huu wa kumi Mhandisi mshauri atakuja kufanya usanifu ," amesema Joseph.
Amesema barabara hiyo iliyotengenezwa kwa kiwango cha changarawe ina urefu wa mita sita, ukarabati wake unagharimu zaidi ya Tsh Milioni 6 ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 TARURA imetenga zaidi ya Tsh Milioni 100 kwa ajili ya matengenezo barabara nyingine za manispaa ya Musoma.
Amesema kuwa ili kupunguza adha ya vumbi kwa wananchi wa eneo hilo zitawekwa alama za kudhibiti mwendo pamoja na kuweka matuta na kwamba mwendo kasi wa vyombo vya moto ndiyo unachangia uwepo wa vumbi.
Mhandisi Joseph Mkwizu
Ameongeza kwamba umwagiliaji wa maji unaofanyika ni kwa kipindi cha matengenezo hivyo ukarabati ukikamilika zoezi la umwagiliaji litakuwa limeisha, amewaomba wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hicho cha matumizi ya barabara hiyo ya changarawe.
>>> Oktoba , 17, 2022, DIMA Online iliripoti habari kuhusu barabara hiyo ya Shabani ambapo Madiwani na Wananchi wa mtaa wa Shabani walisema wanapata kero ya vumbi baada ya kufanyika ukarabati wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ambayo awali ilijengwa kwa kiwango cha lami.
Post a Comment