UKOSEFU WA MALISHO TISHIO KWA VIJIJI VINAVYOPAKANA NA HIFADHI
>>>Wafugaji wasema ukosefu wa malisho unavunja mahusiano na Hifadhi
>>>Wasema Pori lililochukuliwa na Hifadhi ndilo lenye nyasi
>>> Wachoshwa na mateso
Na Dinna Maningo, Tarime
UKOSEFU wa malisho ya mifugo unavikumba vijiji mbalimbali wilayani Tarime mkoa wa Mara, vikiwemo vijiji nane vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA), jambo linalosababisha kuibuka migogoro ya mara kwa mara baina ya wafugaji na Hifadhi.
Migogoro hiyo hutokea pindi wafugaji wanaposwaga mifugo kupeleka malishoni maeneo ya mpaka wa hifadhi na ndani ya hifadhi hiyo, baadhi wanasema maeneo hayo ni ya kijiji yalitumika kwa ajili ya malisho kizazi hadi kizazi huku Hifadhi nayo ikisema maeneo hayo ni ya hifadhi wananchi wameyavamia na kulisha mifugo pamoja na uwindaji wa wanyama wa hifadhini .
Inaelezwa kuwa askari wa hifadhi ya Serengeti hukamata mifugo na wafugaji kuwa wameingia eneo la hifadhi nakufikishwa katika vyombo vya sheria huku wengine wakitajwa kuuwawa kwa kupigwa risasi, kupotea wakiwa ndani ya hifadhi, vipigo pindi wanapokamatwa, kitendo ambacho kimevunja mahusiano mazuri kati ya hifadhi na wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi.
Vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA ) ni Kijiji cha Kenyamsabi, Masanga na Masurura vilivyopo kata ya Gorong'a, kijiji cha Karakatonga, Gibaso na Nyabirongo kata ya Kwihancha, na kijiji cha Nyandage na Kegonga kata ya Nyanungu.
Makenge Mkami mfugaji na mkazi wa Kijiji cha Nyandage anasema ukosefu wa malisho umesababisha chuki kati yao na hifadhi kwakuwa mifugo hukosa malisho, eneo walilolitegemea lilichukuliwa na hifadhi ya Serengeti.
"Tumeshakuwa wahanga wakimbizi ambao kilio chetu hakijawahi kusikilizwa, 2021 nilikamatiwa ng'ombe 21, kondoo 5 na mbuzi 8 zilikamatwa na askari wa hifadhi wakazitaifisha, chanzo chote cha haya ni ukosefu wa malisho, maeneo yaliyopo ni ya kilimo.
"Tulizoea kwenda kuchungia eneo la mlimani ambalo watu wanauwawa, serikali haijawahi kututengea maeneo ya malisho watu wanapoteza maisha , wengine wanauwawa, mifugo inakamatwa" anasema.
Chacha Kichele anasema " Nilikamatiwa ng'ombe 6 wakiwa eneo wanalosema ni lao nilipofuatilia sikupewa hadi leo hii, wafugaji tuliopakana na hifadhi tunateseka sana," anasema Chacha.
Moja ya eneo wafugaji wanalolitumia kuchunga mifugo
Chacha Maranya mkazi wa Kijiji cha Kegonga anasema " Nilipigwa risasi kwenye paja nikiwa nachunga ng'ombe mlimani nilimtambua kwa jina askari mmoja ilikuwa Oktoba,2019 , ni eneo ambalo wafugaji wengi wanalitumia kuchunga tofauti na hilo hakuna lingine, ukichunga ukakutwa na watu wa hifadhi wanakukamata na kuchukua mifugo," anasema.
Marwa Chacha mkazi wa Kijiji cha Kenyamsabi kata ya Gorong'a mwenye ulemavu wa macho anasema alipata upofu kutokana na mateso aliyopata baada ya kukamatwa na askari wa hifadhi.
Marwa Chacha mwenye ulemavu wa macho
" Nina mke na watoto wanne ilikuwa Oktoba,2,2018 nikiwa nachunga mifugo eneo la mlimani nikakamatwa na askari wa hifadhi walinipiga sana, wakanibeba kwenye gari lao hadi ndani ya hifadhi kichakani nikateswa kwa vipigo kisha wakanipeleka kambini huko nikakuta askari wengine.
" walinipiga sana wakanilisha pilipili nyingi nikawa nazitafuna nilifanyiwa manyayaso makali kitendo kilicho athiri afya yangu na kuwa kipofu sioni, kabla ya vipigo nilikuwa mzima niliona vizuri sasa hivi nimekuwa baba wa kukaa tu nyumbani," anasema Marwa.
Mbusiro Mwita mkazi wa Kijiji cha Nyandage anasema" Ng'ombe wangu walikuwa wakichungwa na watoto eneo la mlimani wakachukuliwa na askari na kupelekwa hifadhini kwenye kambi yao Lenyangaka watoto walikimbia.
" Nilizifuatilia wakaniambia nizitambue nikazitambua zilikuwa ng'ombe 10, mbuzi 8,na kondoo 5 wakaniambia njoo hapa wakanifungia kwenye chumba, wakataifisha ng'ombe sasa nipo sina Ng'ombe watoto walizoea kunywa maziwa zilitusaidia kulimia shamba " anasema mbusiro.
Moja ya eneo wafugaji wanalolitumia kuchunga mifugo
Wajane walia na Hifadhi ya Serengeti
Tatizo la ukosefu wa malisho katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi limesababisha wanawake kuwa wajane wanasema waume wao wailuwawa wakiwa malishoni na wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha ndani ya hifadhi hiyo wakati wakiwa wanachunga mifugo kwenye maeneo yenye malisho yanayopakana na hifadhi.
Wankuru Sensema anasema," mme wangu alikuwa akichunga ng'ombe mlimani akapigwa risasi wakaondoka nae kwenye gari lao huko ndani ya hifadhi hadi leo sijawahi kumuona aliuwawa tangu 2019 aliniacha na watoto 5 wengine hawasomi maisha ni magumu sina pesa za kuwagharamia," anasema.
Rebeka Nyang'anyi anasema ," Mimi na mme wangu tulienda kukata nyasi za kuezekea nyumba mme wangu akakamatwa na watu wa hifadhi mimi nilikimbia wakaondoka nae hadi leo hii hajawahi kupatikana, ilikuwa Agasti, 14,2020 bado naendelea kusubiri, aliniacha nikiwa mjamzito sasa mtoto ana miaka miwili.
" Watoto wananisumbua wananiulizia baba yao nina maisha magumu,Rais ni mwanamke mwenzetu atusaidie maeneo ya malisho yapatikane wanaume wanauwawa tumebaki wajane watoto wanabaki kwenye shida kubwa kwa sababu tu ya mgogoro wa hifadhi na wafugaji, ukifuatilia kwenye vijiji vilivyopakana na hifadhi vina wajane wengi na watoto wasio na baba kwa sababu ya hifadhi " anasema Rebeka.
Ghati Mwita anasema," Mme wangu alienda kuchunga ng'ombe mpaka sasa sijampata na ng'ombe hazijapatikana ilikuwa mwezi ,11,2020 tulishatafuta sana kila mahali kwenye magereza na maeneo mbalimbali lakini hatujampata alipandishwa kwenye gari na askari wa hifadhi watu wakiwa wanaona wakaondoka nae hadi leo hii hajawahi kupatikana ," anasema Ghati.
" Mme wangu alipeleka mifugo kweye chumvichumvi hifadhini akapotelea hukohuko, alikamatwa na askari wa hifadhi tangu 2017 aliniacha na watoto sita na mifugo haikupatikana tulifuatilia tukawaomba ng'ombe wakasema hawana " anasema Bhurwa Nyangi.
Sabina Anthony anasema ," Mme wangu aliuliwa na askari wa hifadhi akaniacha na watoto wawili mmoja akiwa na wiki moja, mimi, baba mkwe na mama mkwe tulikuwa tunamtegemea yeye sasa hivi nahangaika mwenyewe kuhudumia watoto " anasema.
Sabina Anthony (katikati)akiwa na wanae ,baba mkwe na mama mkwe wake
Bhoke Mwita mkazi wa kijiji cha Kegonga anasema ," mifugo huwa inachunga kwenye mlima ambako ndiko kuliko na kambi ya askari wa hifadhi eneo la Kenyangaka usawa wa kitongoji cha Iyema kijiji cha Kegonga, watu wa hifadhi wanaziswaga na kuzipeleka hifadhini huku wakipiga risasi hewani na wakati mwingine kuua kabisa "anasema.
Bhoke Charles anaongeza ," Mme wangu aliuliwa hifadhini na askari wa hifadhi aliniacha na watoto watatu maisha ni magumu angekuwepo tungesaidiana kuhudumia familia lakini ninahangaika peke yangu hata pesa ya kununua nguo za shule kupata ni shida nafanya vibarua vya kupalilia mashamba ya watu, msimu wa kilimo ukiisha maisha ni magumu zaidi " anasema Bhoke.
Mgesi Ryoba mkazi wa Kijiji cha Nyabirongo anasema wafugaji hawana sehemu ya kunywesha maji mifugo wanategemea maji yaliyopo eneo la hifadhini, " Wakikukamata unabambikiziwa kesi ya nyara za serikali na wakikukamata na mifugo wanaichukua wanaeda nayo wanataifisha na mahakamani unapelekwa.
"Ndugu yangu alikuwa ni fundi ujenzi akaenda kunywesha maji mifugo kumbe kulikua na doria ya askari wa hifadhi walimkamata akauwawa huko,kibaya zaidi wakifia ndani ya hifadhi miili inabaki huko huko basi wawe wanatupatia tunazika,wanafanya hivyo ili kupoteza ushaidi kuwa aliuliwa na askari wa hifadhi"anasema Mgesi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyandage Mwita Kiha anasema kuna eneo katika Kijiji hicho lililotumika kwa malisho wamezaliwa na kukuta likitumika kwa ajili ya malisho, lakini likachukuliwa kuwa Hifadhi na mifugo inapoingia kwenye eneo hilo hukamatwa pamoja na wafugaji.
"Kijiji chetu tunategemea malisho kwenye eneo tulilolitumia miaka yote likachukuliwa na hifadhi, upande wa kushoto tumepakana na Kenya alafu kulia tumepakana na hifadhi, wakati wa oparesheni vijiji tulitenga maeneo ya Kilimo na maeneo ya malisho ambayo yalichukuliwa na kukabidhiwa hifadhi" anasema.
Mwenyekiti Kijiji cha Nyandage akionesha eneo ambalo wafugaji hukamatwa na kuuwawa na mifugo kuchukuliwa na Askari wa wahifadhi
Mwenyekiti wa kijiji cha Kenyamsabi Mwita Raphael anasema kuwa pori ni moja lililochukuliwa kwa matumizi ya hifadhi ndilo lenye nyasi na hakuna sehemu nyingine zaidi ya hilo kwakuwa maeneo mengine yanatumika kwa kilimo.
"Tuliomba Serikali itupatie eneo lakini ilishashindikana kinachofanyika askari wakiona mifugo inachunga wanaikamata nakuipeleka hifadhini ili ukomboe mfugo unalipa 150,000 mbuzi 60,000 na lisiti utapewa au usipewe wakikukamata unapelekwa mahakamani kifungo ni miaka mitatu na faini laki tano"anasema Raphael.
Amos Chacha Mwenyekiti wa Kijiji cha Karakatonga anasema kijiji hicho hakina mahusiano mazuri na hifadhi kutokana na matukio ya wafugaji kupotea kwa mazingira ya kutatanisha wanapokuwa wakichunga ndani ya eneo la hifadhi na wakipotea hawaonekani tena.
"Zaidi ya wachungaji wa mifugo 10 walikua wakichunga hifadhini hawajawahi kuonekana yupo ambaye alijeruhiwa kwa risasi akapatiwa matibabu huyo ndiyo yupo ni mzima pamoja na wengine wawili " anasema Mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kegonga Waryoba Mwita anasema kuwa wananchi wanategemea kilimo na ufugaji ili walime shamba wanatumia jembe la kukokotwa kwa ng'ombe na kwamba katika kijiji hicho kuna eneo moja pekee la mlimani linalotumika kwa malisho.
" Hakuna eneo lingine zaidi ya mlimani tumepakana na Kenya,tulikuwa tunachunga kwenye maeneo ya Wakenya nao wanayatumia kulima mazao.Novemba,19,2021 askari wa wanyamapori walikamata mifugo ya Mwenyekiti mwenzangu wa kijiji jirani alikua ikichunga kwenye eneo la Ushoroba. Hayati John Magufuli wakati wa uhai wake alisema tuendelee kutumia eneo hilo wakati huo serikali ikiendelea na mchakato wa utatuzi.
Mwenyekiti huyo anaongeza kusema " Hadi sasa serikali haijatatua kuhakikisha tunapata maeneo ya malisho mbona mikoa mingine vijiji vimepewa ardhi ambayo ilikuwa ya hifadhi lakini Tarime hakuna, ukienda kufuatilia mifugo unakamatwa unapelekwa mahakamani na unataifishiwa mifugo yako, watu wameogopa kufuata mifugo hifadhini maana wakifika watakamatwa, wanaifungia mifugo inakosa chakula ikifa kisha wanaitupa" anasema Warioba.
Warioba anaiomba Serikali kutenga eneo la malisho kwakuwa vijiji havina maeneo ya malisho na vimepakana na vijiji vya Kenya eneo la Trans Mara,eneo la Ang'ata watu wa kabila la Wakarengina (Kipsisi) na kwamba mifugo ndiyo kila kitu katika kukuza kipato cha mwananchi wa kijijini.
John Mkira ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru kata ya Nyarukoba anasema wafugaji wanaopakana na hifadhi ya Serengeti wanapata changamoto kubwa ya malisho ya mifugo na hivyo kujikuta wakiingia mikononi mwa sheria ambapo chanzo kikubwa ni ukosefu wameneo ya malisho ya mifugo.
Anaiomba serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kupitia upya mipaka hiyo ikiwezekana ipunguze eneo la hifadhi na kuvipatia vijiji ili wachunge mifugo yao,kwa kufanya hivyo itasaidia kuondoa migogoro na kujenga mahusiano mazuri kati ya wafugaji na Hifadhi ya Serengeti.
Nyumba ziliyoezekwa kwa nyasi
........Itaendelea
Post a Comment