DKT. MPANGO KUZINDUA MAONESHO YA UTALII YA KISWAHILI
Na Andrew Chale,Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Phillip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi rasmi wa maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Tanzania yanayojulikana kama Swahili International Tourism Expo (SITE).
Maonesho hayo yatafanyika kwa siku tatu Oktoba,21 hadi 23 ,2022 katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam, yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘Kuupeleka Utalii katika Ngazi za Juu (Taking Toursim to the New Heights)'.
Akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya maandalizi ya onesho hilo la Sita (6), kwa mwaka huu Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Felix John aliyeambatana mkuu wa wilaya ya Ubungo Kheri James aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla,amesema maandilizi yote yamekamilika na wadau mbalimbali wa ndani na nje watahudhulia huku likitarajiwa kuleta matokeo chanya katika kukuza Utalii wa Tanzania.
‘’SITE 2022 ambalo tumekuwa tukilisubiria kwa hamu kubwa, tangu kuahirishwa kwake onesho la mwisho mwaka2019, tunaamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari na mmekuwa mabalozi wetu wazuri katika kuhabarisha na kutangaza vivutio vilivyopo nchini.
" Tayari maandalizi makubwa yamefanyika maonesho yatakayoanza Oktoba 21, Wafanyabishara wa kutoka ndani na nje ya nchi watahudhuria watapata fursa za kuonesha bidhaa, kutengeneza mtandao wa biashara, kuanzisha na kuimarisha mahusiano ya kibiashara’’ amesema Felix .
Ameongeza kuwa, tangu kuanzishwa kwake limekuwa la mafanikio makubwa ikiwemo ongezeko la waoneshaji (Exhibitors), na wanunuzi wa kimataifa ambapo ilisimama kwa muda kutokana na mlipuko wa UVIKO 19.
‘’Tutakuwa na mikutano ya wafanyabiashara B2B, B2G, Lakini pia kutakuwa na siku tano (5) za ziara za mafunzo (FAM trips) ambapo watatembelea vivutio vya utalii nchini ikiwemo Hifadhi za Taifa Serengeti, Mkomazi, Mikumi,Nyerere, Udzungwa,Ngorongoro, Kisiwa cha Zanzibar na maeneo mengine mbalimbali ya Utalii na Utamaduni.’’ Amesema Felix.
" SITE 2022 litahudhuriwa na waoneshaji zaidi ya 200 na wanunuzi wa Kimataifa takribani 100 kutoka masoko ya kimkakati hususani nchi za Marekani, Uholanzi, Afrika Kusini,India, Urusi, Hispania, UAE, Poland, Finland, Japan, Oman na zingine nyingi.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kheri James amewahakikishiwa watu wote kuwa wamejiandaa kwa tamasha hilo ikiwemo kuimarisha hali ya ulinzi na usalama huku akiwakaribisha watu wote kutembelea maonesho hayo kwa gharama nafuu ambapo watajifunza, watanunua bidhaa na pia watapata burudani mbalimbali.
Katika onesho hilo kiingilio kinatarajiwa kuwa Tsh . 5,000 kwa watoto na Wakubwa Tsh. 10,000, kutakuwa na kifurushi cha familia ambacho kitajumlisha Baba, Mama na watoto wawili Tsh 25,000.
Wadau waliodhamini onesho hilo ni pamoja na wadau mbalimbali katika sekta ya utalii, ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambaye ni mdhamini mkuu,Vodacom Tanzania, Kampuni ya ONA& METAS Stories, CRDB, TATO, na wengine wengi.
Hata hivyo, onesho hilo ni sehemu ya utekelezaji kwa vitendo program maalum ya Tanzania-The Royal Tour iliyohasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kwa lengo la kutangza vivutio vya utalii na fursa zilizopo nchini za uwekezaji.
Post a Comment