HEADER AD

HEADER AD

WAITARA : UCHAGUZI 2025 CCM ITAKUWA MSELELEKO, AMFAGILIA RAIS SAMIA


Na Dinna Maningo ,Tarime

MBUNGE wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu, imetoa fedha nyingi katika Jimbo la Tarime Vijijini ambazo zimejenga miradi mingi, hivyo kupunguza changamoto nyingi zilizopigiwa kelele na wapinzani.

Waitara ameyasema hayo mbele ya Waandishi wa Habari na baadhi ya Wazeee wa Mila kutoka koo 12 za Jamii ya Wakurya Octoba, 24,2022 katika Ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tarime, alipokuwa akieleza mafanikio yaliyopatikana katika Jimbo hilo kwa kipindi cha  mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi wakati wa kampeni na Ilani  ya uchaguzi ya 2020-2025 ya chama hicho.

Waitara amempongeza Rais Samia kwa kuwathamini wanatarime na kusema kuwa uchaguzi wa 2025 utakuwa ni mseleleko kwa CCM kwakuwa kero nyingi zilizowatesa wananchi ambazo wapinzani walizitumia kukikandia chama hicho, Rais Samia kazitatua kwa kutoa fedha nyingi kujenga miradi mbalimbali ikiwemo ya Afya,Maji,Elimu na Barabara.

" Jimbo langu limepokea fedha nyingi ambazo zimejenga miradi kulikuwa na changamoto nyingi ambazo upinzani walikuwa wanazikandia, tunaamini uchaguzi ujao hoja za kiupinzani zitakuwa chache maana changamoto nyingi zimetatuliwa. Miradi hiyo ni utekelezaji wa ahadi na Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Ilani ndogondogo za majimbo.

" Namshukuru sana Rais Samia Jimbo langu limepata mgao wa fedha na hata kuzidi majimbo mengine tunamshukuru na tunamuomba aendelee kutushika mkono, eneo letu lilikuwa na upinzani sana nawashukuru wanaccm kunichagua maana tuligombea wengi lakini nikashinda mimi, baada ya uchaguzi wananchi walikua na matarajio makubwa sana na sasa mafanikio wanayaona " amesema Waitara.

Waitara amesema miradi iliyofanyika itakuwa ni mtaji wa CCM katika uchaguzi 2025 na kwamba wanatarajia Rais Samia atakuwa mgombea ili kazi iendelee  2025-2030 na kwa miradi hiyo atashinda kwa kishindo kwakuwa amekua akitafuta fedha nyingi ambazo zimewezesha kujengwa miradi mingi nchini ikiwemo na Tarime.

Waitara ametaja baadhi ya miradi na kiasi cha fedha kilichotolewa na Serikali ya awamu ya sita fedha kutoka serikali kuu, kuwa ni pamoja na fedha za mfuko wa Jimbo kiasi cha Tsh. Milioni 104 zilizotolewa kwa miaka miwili katika mwaka huo wa fedha ambapo serikali hiyo imeongeza fedha kutoka Milioni 52 hadi Tsh.Milioni 71 zinazosubiriwa na zitakapofika zitapangiwa matumizi kwenda kutekeleza Huduma za Jamii.

Amesema katika mwaka huo wa fedha Jimbo lake limepokea fedha nyingi kiasi Tsh. Bilioni 5.4 kutoka Wakala wa  Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA ) kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na nyingi zimelimwa ikiwemo barabara ya Kiore na Mtana.

" Pia Rais ametoa fedha za kujenga barabara yenye urefu wa km 25 kutoka Mogabiri hadi Nyamongo, ametoa kibali na kutangazwa zabuni ujenzi wa barabara yenye urefu wa km 61 barabara ya Nyamwaga hadi Mugumu Serengeti sasa hatutakua na shida ya mawasiliano , " amesema Waitara.

Katika Huduma za Afya amesema baadhi ya miradi iliyopatiwa fedha kutoka serikali kuu ni pamoja na Tsh. Milioni 500 zilitolewa kujenga kituo cha Afya Manga, Tsh. Milioni 500 Zahanati ya Bumera, Tsh. Milioni 300 kuboresha Kituo cha Afya Magoto, Tsh. Milioni 300 kujenga kituo cha Afya Kwihancha, na kwamba zahanati zilizokuwa zimekwama kwa miaka mingi zimekamilika.

Kwa upande wa Elimu amesema fedha zilizotolewa kutoka Serikali kuu ni pamoja na Tsh. Milioni 600 ujenzi shule ya Sekondari Bukira, Tsh.Milioni 420 ujenzi wa madarasa shule  23 za Sekondari na kwamba hakutokuwa na upungufu wa madarasa utakaowakwamisha wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza.

         Mbunge Waitara akiteta jambo na Katibu wake Remmy Mkapa , kulia ni Mzee wa Mila

Fedha zilizotoka Serikali kuu kutekeleza miradi ya maji amesema ni pamoja na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria wa Tsh Bilioni 138 utakao hudumia majimbo matatu ya Rorya, Tarime na Serengeti.

" Kupitia RUWASA miradi mingi ya maji imejengwa kama vile mradi wa maji Korotambe, Nyagisya, Nyarwana, Gibaso, Nyamwaga, Kewanja, Nyantira, Keisangora, Magoma, Keisaka,Gamasara, karibu kata zote zina miradi ya maji,Tsh.Milioni 450 zimetengwa kutafuta chanzo cha maji.

"Uchaguzi ujao utakuwa ni mseleleko kwa CCM kwasababu ya mambo yanayoendelea kufanyika, hiyo ni baadhi ya miradi iliyojengwa kwa fedha kutoka serikali kuu, ndani ya miaka miwili miradi ya elimu, afya na huduma za kijamii tumepata Tsh.Bilioni 9.8, na kwa mapato ya ndani Halmshauri hukusanya zaidi ya Bilioni 6 ," amesema.

Akizungumzia fedha za Mpago wa Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) amemshukuru Rais Samia kutoa kibali ili fedha Tsh. Bilioni 5.6 kutoka Mgodi wa North Mara Barrick zianze kutumika kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo fedha hizo zilizuiliwa tangu 2020 pasipo kutolewa baada ya kuwepo kwa ufujaji wa fedha katika mwaka 2019/2020 pamoja na manunuzi ya vifaa kwa gharama kubwa kuliko uhalisia na vifaa vingine kuzidi mahitaji kama vile,saruji, nondo na tofari.

                  Mbunge Waitara akieleza mafanikio katika Jimbo la Tarime Vijijini

"Nampongeza Rais Samia kwa kutupatia kibali, na kuagiza zitekekezwe katika maeneo husika kwa mujibu wa sheria, fedha hizo za CSR zitaanza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya kijamii ambapo asilimia 70 ya fedha itajenga miradi kweye vijiji 11 katika kata tano zinazozunguka mgodi na asilimia 30 zitaenda kwenye kata zingine, kati ya fedha hizo Tsh. Milioni 48 zitapelekwa kituo cha Afya Magena kilichopo Tarime mjini," amesema.

" Nampongeza Rais wa Barrick kwa kuongeza uzito katika suala hili kuhakikisha fedha za CSR zinaanza kutumika na kibali kimetolewa, nawapongeza viongozi wa Serikali Makamu wa Rais Dkt.Mpango, Waziri mkuu , Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kwa usimamizi mzuri, hizi fedha za CSR nilizipigia kelele sana hadi bungeni viongozi wakasikia kilio changu na fedha zimeruhusiwa kutumika.

Waitara ameongeza " Tutakuwa wakali sana kusimamia fedha hizi, fedha hizo zitajenga miradi mipya, miradi viporo na kulipa madeni katika miradi ile ya CSR iliyokuwa imejegwa ambayo hayakulipwa baada ya zuio la fedha.

Amesema kuwa Tsh. Milioni 400 zitatumika kujenga Chuo cha Mafunzo Stadi (VETA) kitakachojengwa Nyamongo, Tsh. Milioni 180 kununua gari kufuatilia miradi ya CSR, Tsh. Milioni 140 kununua madawati, Tsh.Milioni 46 kwa ajili ya kulipia ada watoto wenye mazingira magumu pamoja na stendi ya kisasa itakayojengwa Nyamwaga.

Ameongeza kuwa soko la Afrika Mashariki Remagwe litajengwa, itajengwa Bucha kubwa ya kisasa ya nyama Nyamongo na kwamba kutaimarishwa mashindano ya michezo ili kupata timu ya mpira wa miguu ya Jimbo na kuongeza kuwa Barrick imeahidi kujenga uwanja wa michezo wa kisasa Nyamongo.

Mbunge huyo amesema kuwa wameyaelekeza makampuni yanayofanya kazi Mgodi wa North Mara ambayo yalikuwa hayalipi kodi kulipa ndani ya miezi mitatu ambapo wamebaini baadhi ya makampuni hayana leseni.

Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tarime Marema Solo amempongeza rais Samia kwa kuondoa ada ya kidato cha tano na sita na kutoa fedha nyingi kutekeleza miradi wilayani Tarime huku akimwomba kufika Tarime kuwasalimu kama anavyofanya ziara sehemu zingine.

        Katibu Mwenezi CCM Marema Solo

Marema amesema Chama hicho ngazi ya wilaya hakitokuwa tayali kuona fedha zilizotolewa na serikali zinafujwa badala ya kutekeleza miradi kikamilifu na kwamba kitahakikisha kinasimamia vyema fedha za CSR kama zilivyokusudiwa.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tarime Mathias Lugola amempongeza mbunge Waitara kwa kazi anayoifanya kuhakikisha jimbo linapata maendeleo pamoja na kupigania fedha za CSR ambazo kibali kimetolewa zifanye kazi Huku Katibu Mwenezi Marema akimpongeza kwa ushirikiano wake na Chama cha Mapinduzi pamoja na utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jimbo lake.

          Katibu Wazazi CCM akizungumza

Katibu wa Wazee wa Mila koo ya Butimbaru Mwita Nyasibora amempongeza Waitara kwa kazi anayoifanya ikiwa ni pamoja na kuwakumbuka wazee wa Mila kwa kuwashirikisha katika mambo mbalimbali ya kijamii huku wakimpongeza Rais Samia kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na kutoa fedha nyingi za miradi wilaya ya Tarime.

       Mzee wa Mila Mwita akizungumza








No comments