WALIOCHAGULIWA CCM WILAYA WAPONGEZWA
MWENYEKITI wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja amewapongeza viongozi wa ngazi mbalimbali nchini waliochaguliwa katika uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya wilaya.
Mgeja aliyekuwa mmoja wa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM Wilaya ya Kahama,alitoa pongezi hizo jana katika eneo la Kinu cha Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) kilichopo Mhongolo,wilayani humo.
Akitoa maoni yake kwa waandishi wa habari kuhusu uchaguzi huo uliofanyika kote nchini kwa ngazi za wilaya kwa nyakati tofauti, alisema binafsi kwa mtazamo wake uchaguzi ulikwenda vizuri na aliona umefanyika kwa haki,uhuru na kwa kufuata misingi ya demokrasia ya ndani ya CCM.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wa Mkoa huo na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC),alisema viongozi waliochaguliwa na wajumbe wanastahili kupongezwa kwa ushindi.
“Binafsi nawapongeza viongozi mbalimbali nchini waliochaguliwa kuanzia nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya,Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa,Halmashauri Kuu ya Wilaya,Mkutano Mkuu wa Mkoa,Kamati za Siasa na Makatibu wa Itikadi na Uenezi, uchaguzi umekwisha kwa ngazi ya wilaya sasa wakafanye kazi kuhakikisha ilani ya uchaguzi ya CCM inatekelezwa ili kukirahisishia Chama uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025,”alisema Mgeja.
Aliwaomba kuyaacha yaliyopita na kuganga yajayo baada ya uchaguzi hivyo kwa sasa wakaunganishe makundi ya wanachama waliowaunga mkono na ambao hawakuwaunga mkono na kuwa kitu kimoja kama ilivyokuwa awali kwa sababu CCM ni moja na ile ile.
“Kufanya hivyo wataonyesha ukomavu wa demokrasia na kisiasa, na kinachohitajika sasa baada ya uchaguzi ni umoja,upendo na mshikamano ndani ya Chama kwani waswahili wana usemi ‘Umoja ni nguvu na Utengano ni udhaifu’, hivyo tugange yajayo na yaliyopita si ndwele,”alisema.
Mgeja amewatakia kheri viongozi wote walichaguliwa Nchini kwa nafasi mbalimbali kwa kipindi cha uongozi miaka mitano na kuwaahidi makada wa CCM kuwapa ushirikiano utakaohitajika wenye manufaa katika ujenzi wa Chama ili kazi iendelee.
Post a Comment