KILIMO BIASHARA CHA MBOGA MATUMAINI MAPYA KWA VIJANA WA KIJIJINI - 2
Na Dinna Maningo, Tarime
VIKUNDI
vya Vijana katika kijiji cha Matongo Kata ya Matongo - Nyamongo wilaya
ya Tarime mkoani Mara,vilivyoanzishwa kwa ajili ya Kilimo Biashara
vimekuwa na nia ya dhati katika kilimo kutokana na juhudi za vijana
ambazo wamezionesha kwenye uandaaji wa shamba kwa kushirikiana pamoja
kuhakikisha wanatimiza ndoto yao ya kujiinua kiuchumi.
Wanakikundi
wanasema baada ya kujiunga na kilimo biashara wamepata elimu ya kilimo
cha kisasa ambayo hawajawahi kuipata,wengine wanasema kuwa kupitia mradi
huo wamefika Arusha mkoa ambao hawajawahi kufika tangu wazaliwe hivyo
mradi umewezesha wao kutalii katika mkoa huo.
Mwanakikundi
wa senta shule Mseti Mwita anasema "Nina wake wawili na watoto sita
nafurahi kuwa miongoni mwa wakulima wa kilimo biashara ndio mara yangu
ya kwanza kujihusisha na kilimo cha mboga cha umwagiliaji nimepata elimu
ya kilimo biashara.
"
Kingine kizuri zaidi tangu nizaliwe sijawahi kufika Arusha lakini
kupitia mradi huu nimefika kwa kugharamiwa gharama zote na mgodi
nimejifunza mengi kuhusu kilimo ni wajibu wangu kuhakikisha elimu
niliyoipata itanisaidia kakua kiuchumi kupitia kilimo biashara " anasema
Mseti.
Katibu wa
kikundi cha Masangora Lameck Chacha mwenye mke na watoto sita anasema "
Nilikuwa sijui kilimo biashara ni nini,watu wa mahusiano wa mgodini na
serikali walitupatia elimu kisha tukapelekwa Arusha kujifunza kwa
wakulima wenzetu kilimo biashara,nashukuru nimepata elimu na nimefika
mkoa ambao sijawahi kufika,tulipokuwa shule tuliambiwa mali utaipata
shambani matarajio yangu ni kuona kilimo hiki kinakuwa tija kwa vijana
wa kijijini "anasema Lameck.
Katibu
wa kikundi cha Kegonga B Julius Ntakamazi anasema " Tunashirikiana bila
shida tulienda Arusha tukajifunza kupanda mbegu,kutawanya,kupanda na
kukuza tunawashukuru wataalam walitupatia elimu ya kilimo bora cha
kisasa tuna hakika kupitia kilimo hiki tutajiongezea kipato"anasema
Ntakamazi.
Mwanakikundi Julius Ntakamazi akiwa sambani akilima |
Anasema
kuwa wananchi wa kijiji cha Matongo mashamba yao yapo kando kando ya
mto Mara,msimu wa mvua mto hufurika na kuharibu mazao hivyo anategemea
kupata mafanikio kupitia kilimo biashara kwakuwa eneo lililotengwa ni
rafiki kwa kilimo cha mboga.
"Tunaushukuru
uongozi wa kijiji kwa kutoa ekali 10 kuwapa vijana na mgodi
umeviwezesha vikundi miundombinu ya kilimo kwa kutoa vifaa vya kitaalam
kufanikisha kilimo biashara,kule tunakolima karibu na mto Mara udongo ni
wa kichanga mvua ikinyesha kidogo mazao yanakauka,mvua ikiwa nyingi
yanatokea mafuriko mazao yanasombwa na maji.
"
Tunalima mazao kizamani kwa kurusharusha mahindi shambani tukivuna
mazao ni kidogo kwasababu hatulimi kitaalam,ila kupitia kilimo biashara
nimejifunza namna ya kuandaa matuta,namna ya kutumia kamba kunyoosha
matuta,kuacha njia ya kupita kati ya tuta na tuta ambayo hata kweye
mavuno pikipiki au bajaji itapita shambani kubea mazao,elimu ambayo
nilikuwa sina" anasema.
Sadock
anasema kuwa kilimo biashara kitasaidia kupunguza matukio ya uvamizi
ndani ya mgodi "huu mradi ni wa majaribio wameanza na vijana 100, mgodi
umeokoa vijana 100 ambao hawawezi kwenda tena kuingia mgodini kuchukua
mawe ya dhahabu.
"Muda
mwingi watakuwa shambani zile fikra za kuona kuwa ili upate pesa mpaka
uingie mgodini zimeondoka kwakuwa vijana wametambua fursa nzuri ambayo
hawakuhifahamu ya kilimo biashara,vijana wa Matongo wamepata bahati.
Anaongeza
"Umefika hapa umeona wakulima wanakula chakula hawajanunua kwa pesa yao
wamegharamiwa na mgodi, wameandaa shamba, mambo ya kitaalam
wanaelekezwa na wataalam wetu wa halmashauri ambao nao wamejitahidi
kuhakikisha vijana wanaona uthamani wa kilimo hiki"anasema Sadock.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Vikundi 10 vya Kilimo Biashara Marwa Mkeba ambaye ni
mwanakikundi cha Kemagutu anasema kuwa vikundi vina jumla ya vijana 100
kati yao wanawake ni 13 waliojiunga na kilimo hicho na kila kikundi
kimeandaa shamba kwaajili ya kuotesha mbegu za mboga zitakazo tawanywa
shambani.
Marwa Mkeba Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vikundi 10 vya Kilimo Biashara |
Mkeba anasema kuwa vikundi vyote vimekuwa na mwitikio wanaendelea na shughuli za
shamba kwa kufuata maelekezo ya wataalam hatua kwa hatua,lengo ni
kusaidia vijana kubadilika kifikra wasiende kuvamia mgodi bali
wajishughulishe na kilimo cha biashara
"Tunaishukuru
Halmashauri ya wilaya ya Tarime kupitia Idara ya Kilimo kwa elimu
wanayotupatia ya kilimo bora,tunaushukuru uongozi wa mgodi kwa
kutuwezesha tunauomba usituache waendelee kutushika mkono wawe walezi
wetu ili tufikie lengo la kujikwamua kiuchumi"anasema Mkeba.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Matongo Daud Itembe anasema kuwa sababu ya mradi huo
kuanzishwa kijijini ni kuwasaidia vijana wasiinge mgodini kitendo
ambacho kilivunja mahusiano kati ya kijiji na mgodi pindi vijana
walipokamatwa kwa kuingia mgodini kuchukua mawe yenye dhahabu.
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Matongo Daud Itembe
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Matongo Daud Itembe
"Tuliongea
na uongozi wa mgodi tufanye nini ili vijana wasiweze kuingia mgodini
nikawaambia kijiji kina ardhi ya kutosha vijana wawekeze kwenye
kilimo,baada ya kupata mradi tuliitisha mkutano wa kijiji tukawaeleza
kusudio,tukawaunganisha vijana wa kike na kiume na watu wazima kama
walezi wao kwenye vikundi,tuliomba vijana ambao hawafanyi kazi mgodini
ndio wajiunge kwenye mradi.
"Kijiji
kina vitongoji tisa kila kitongoji kilileta watu 15 wakachunjwa kwenye
mkutano wakapatikana watu kumi kwa kila kikundi,hatukubagua mtu kujiunga
wala kuangalia anatoka chama gani cha siasa, watu walichaguliwa kwenye
mkutano wa hadhara wakawa wanataja huyu anaweza huyu hapana na vitongoji
ndio vilikuwa vinapitisha watu.
Anasema
kuwa baada ya watu kuchaguliwa kupitia mkutano wa hadhara walipata
elimu ya kilimo biashara ambapo kila kikundi kilitoa viongozi wawili
ambao walipelekwa mafunzo mkoani Arusha.
"Na
mimi nilienda nikashiriki mafunzo ni mradi wa kisasa tuliona watu wana
maeneo madogo ya kilimo lakini wanapata mazao mengi, bahati nzuri mgodi
umetangaza ajira kuajiri afisa kilimo ili kusimamia wanakikundi kwa
ukaribu,mradi huu ukikamilika miradi mingine itaibuliwa mgodi utatoa
fedha za kuendesha miradi,soko lipo wateja ni mgodi na tutatafuta masoko
mengine "anasema Daud.
Swai
Godwin ni Afisa Kilimo kata ya Matongo anasema kuwa lengo la kuanzishwa
mradi huo ni kuwawezesha vijana hao kubadilisha mawazo na fikra kwamba
pesa si mpaka uipate kwenye Dhahabu inapatikana na kwenye kilimo.
"Kikundi kina vijana 100 sasa hivi kinachofanyika ni uaandaji wa shamba darasa
kisha zinapandwa mbegu,mgodi ulisema utaleta mbegu za mboga za
nyanya,kabeji na zinginezo zitakazopandwa kwenye shamba,hawa vijana
watazalisha kila kitakachozalishwa mgodi utanunua kitakachobaki soko
litatafutwa ,serikali ya kijiji imetoa eneo na nguvu kazi za
vijana,halmashauri imetoa wataalam na mgodi unatoa miundombinu yote
katika kilimo hicho.
Afisa Kilimo Kata ya Matongo Swai Godwin |
"Hii mipira unayoiona imeandaliwa na mgodi kwa ajili ya umwagiliaji shamba
kwa njia ya matone,kazi ya mpira ni kutoa maji kwa kila mmea,ekari moja
inakuwa na matuta 62 maji yatatoka mtoni takribani mita 400 yatavutwa
yaingie kwenye bwawa la kutunza maji lenye urefu wa mita 25 upana
15,kina mita 2,hayo maji yatakayovutwa kutoka kwenye mto kuja kwenye
bwawa yatachujwa mchanga wakati yanatoka bwawani kuingia kwenye mipira
yatakuwa yanachujwa tope "anasema Swai.
Swai
anasema kuwa mfumo huo ni mzuri kwa kilimo hususani vitunguu ambavyo
vinahitaji maji wakati wote anawaomba wana kikundi kutumia vyema fursa
hiyo yenye utajiri ili waondokane na umaskini huku akiwahakikisha kuwa
soko lipo wajitahidi katika kilimo hicho.
Kituo
cha Utafiti na Mafunzo ya Mboga na Matunda (HORTI-TENGERU) kilichopo
mkoani Arusha,mwaka 2018 kilitoa Mwongozo kwa Wakulima na Maafisa Ugani
wa utayalishaji wa kitalu bora cha mbogamboga,kuhamisha miche toka
kwenye Kitalu,Uvunaji na Uhifadhi.
Kwa
mujibu wa Mwongozo huo umeeleza kuwa,Mboga za majani ni sehemu muhimu
katika mlo wa mwanadamu,mboga hutoa virutubisho muhimu kama vile
protini,vitamini,na madini ambayo ni muhimu katika mwili wa mwanadamu
kwa afya bora.
Ulaji wa
mbogamboga katika nchi nyingi za Afrika zilizo chini ya jangwa la sahara
ikiwemo Tanzania,upo chini ya kiwango kinachoshauriwa na Shirika la
Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO),hivyo basi uzalishaji wa miche bora
kitaluni na utunzaji wa miche bustanini/shambani kwa kutumia mbinu za
kisasa ni msingi muhimu katika kuboresha upatikanaji na ulaji wa mboga
kwa kaya na jamii kwa ujumla.
...............Itaendelea
Post a Comment