HEADER AD

HEADER AD

WAZEE WA MILA WAONYA WANANCHI WANAOHARIBU MISITU YA ASILI



Na Dinna Maningo ,Tarime 

WANANCHI wilayani Tarime mkoa wa Mara wametakiwa kujenga tabia ya kuhifadhi na kulinda misitu ya asili ili iwe endelevu kizazi hadi kizazi ikiwemo inayotumiwa na wazee wa mila na sio kuikata ovyo kwa matumizi binafsi hali ambayo imesababisha miti ya asili kuzidi kupungua.

Wakizungumza na DIMA Online baadhi ya Wazeee wa mila wamesema awali wananchi waliheshimu misitu inayotumiwa na wazee wa mila kwa shughuli za kimila zikiwemo za matambiko lakini kwa sasa hawana uoga na kuzidi kuharibu misitu ya asili kwa kukata miti ovyo.

Katibu wa Wazee wa Mila Koo 12 za Jamii ya Wakurya wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, Bonifas Meremo amesema ," Watu wamekosa nidhamu wanavamia misitu kwa siri inayotumiwa na wazee wa mila kwa ajili ya vikao na matambiko tunaomba waache mara moja, sisi wazee tunasaidia uhifadhi wa misitu ya asili ukienda huko Bwirege watu wanakata miti ovyo," amesema.

Thomas Marwa mzee wa mila koo ya Butobori mkazi wa mtaa wa Nyandoto amesema watu wamekuwa wakiingia kwa siri kukata miti katika msitu wa wazee wa mila wa Inano na Bugucha , amewataka kuacha mara moja.

" Koo yetu ya Butobori ina wazee wa kimila 12, Tunazuia watu wasiingilie misitu hiyo lakini hawasikii wanaingia kwa siri wanakata miti yaani mikaa inazidi kumaliza miti ya asili, wanafanya hivyo wakijua wazee wa mila wamekuwa wapole, zamani waliieshimu walikuwa hawathubutu hata kuvunja tawi la mti wanajua adhabu iliyowakabili.

" Sasa hivi wazee wa mila wamekuwa wapole, utauwa watu uwamalize kweli ? tukisema tuchukue hatua tutaumiza watu, wazee wa mila kwa sasa hatutaki hayo mambo tunaomba na wao wasituchokoze, huwapati kwasababu wanaiba kwa siri tukiwakamata tunawatoza mbuzi mmoja lakini bado hawaachi, tulitoa sehemu ya msitu ikajengwa Zahanati ya Masurura , narudia tena naomba waache huo mchezo," amesema akisisitiza.



Mzee huyo wa mila amesema msitu wa Inano kuna kisima cha asili ambacho hakijawahi kukauka hata msimu wa kiangazi hutoa maji na kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi.

" Hata jua liwake kiasi gani maji hayakauki msitu umesaidia kisima kisikauke, pia msitu huo tunautumia kwenye matambiko yetu wakati mwingine tunatoa miti kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za kijamii 

Mzee wa mila kutoka kata ya Nyarero ambaye pia ni katibu wa mila koo ya Nyabasi Julius Nyang'ora, amesema milima ya serikali nayo imevamiwa na watu na kufanya uharibifu na kwamba  wazee wa mila ndiyo pekee waliobaki kutunza mazingira ya misitu ya asili.

" Milima iliyokuwa chini ya Serikali nayo ilmevamiwa watu wanakata miti ovyo , maeneo ya mlima yameuzwa na kugeuzwa kuwa makazi ya watu , wenyeviti wa vijiji wanadanganyika na fedha kidogo wanauza maeneo ambayo ni ya asili na kusababisha uasili wa mazingira yetu kupotea , milima hiyo tunaitegemea sana kwasababu inachangia kuleta mvua.

" Watu waache kukata miti ili kuendeleza uhifadhi, kwa huku kwetu msitu wa Wazee wa mila haujavamiwa na wananchi ulitengwa kwa ajili ya matumizi ya wazee wa kimila yakiwemo matambiko huwezi kusenya kuni wala kukata mti ukikata unadhurika maana ni maeneo yaliyozindikwa na madawa mazito na huwa tunakutana kila jumamosi kufanya vikao vyetu," amesema .

Mzee wa mila kutoka koo ya Bukira Wambura Mtongori amesema wanakabiliwa na changamoto ya utatuzi wa migogoro ambapo wazee wa mila wanapotoa maagizo au adhabu ndogondogo kama njia ya kujenga maadili kwenye jamii watuhumiwa huenda kushtaki serikalini kwenye vyombo vya sheria na hivyo maamuzi yao kutotambuliwa.




Amesema hali hiyo imesabaisha kupungua kwa nidhamu na maadili ndani ya jamii kwakuwa wazee wa mila hawana nguvu kisheria ya kuwawajibisha wenye hatia hivyo kuendelea kudharauliwa na jamii.



No comments