HEADER AD

HEADER AD

MABOTTO: VIONGOZI WA KISIASA MSITUMIE NAFASI ZENU KUKWEPA KODI

 

Na Jovina Massano, Musoma.

MBUNGE wa Jimbo la Bunda Mjini Mkoani Mara, Robert Mabotto amewashauri viongozi wa kisiasa kutotumia nafasi walizonazo kukwepa kulipa kodi kwakuwa Serikali hutumia kodi hizo kuwapelekea wananchi miradi ya maendeleo na mahitaji mengine ya Kitaifa.

Ameyasema hayo hivi karibuni wakati  akipewa tuzo  ya mlipa kodi kwa hiari na kwa wakati kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)mkoa wa Mara, ambapo wafanyabiashara 28 kutoka wilaya za mkoa wa Mara walipewa tuzo.

Amesema kodi  haikwepeki na pia ipo kwenye vitabu vya dini na unapofanya biashara halafu hulipi kodi unakuwa umewanyima na kuwadhulumu watu stahiki zao hivyo taratibu na sheria zilizowekwa zifuatwe kwa maendeleo ya Nchi.

"Mara nyingi sisi viongozi wa kisiasa tunapopata nafasi hizi tunaweza kuzitumia vizuri aidha vibaya kwa kufanya kama chaka la kujificha ili tusiweze kutozwa kodi mimi ni kiongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu.

"Kwa kazi kubwa ambayo Rais anaendelea kuifanya ninawiwa kusema kuwa ni vizuri wafanyabiashara wote walipe kodi bila kusukumwa wala kulazimishwa kwani maendeleo ya nchi yetu yanaletwa na sisi wenyewe kupitia kodi zetu", amesema Mabotto.


       

Ameongeza kuwa hivi sasa miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati kwa sababu wafanyabiashara wengi wanalipa kodi kwa wakati bila shuruti tofauti na hapo nyuma miradi ilikuwa inachukua muda mrefu kwa kuwa wengi walikuwa wakikwepa kulipa Kodi.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Patrick Chandi ameipongeza TRA kwa kutoa tuzo kwa walipakodi kwani kwa kufanya hivi kutaleta morari kwa wafanyabiashara kulipa kodi  bila kusukumwa.

"Nawapongeza sana TRA kwa kuweza kutambua umuhimu kwa walipakodi na kuweza kuwatunuku tuzo, hii itasaidia msukumo mkubwa kwa wafanyabiashara kulipa kodi bila kusukumwa.

" Huko nyuma ukusanyaji ulikuwa wa mabavu purukushani ya kukamatwa na Polisi ikiwemo na kufungiwa akaunti hii ilifanya watu kutokuweka fedha Benki ubunifu huu wa ulipaji kodi umeleta matokeo chanya tunayoyaona hivi sasa kodi ni kwa maendeleo yetu", amesema Patrick.

Kamishna wa walipakodi wakubwa Alfred Mregi amewapongeza baadhi ya wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa kuwezesha TRA katika kushirikiana kudhibiti magendo.


"Katika mpango huu wa sita tunategemea mawazo na mchango wenu ili kuongeza vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza wigo wa kodi na kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi yetu.

"Pia nawapongeza baadhi ya wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa kuwezesha TRA kudhibiti magendo kwani kumesaidia mapato mkoani hapa kuongezeka",alisema Mregi.

Afisa Elimu na huduma kwa mlipakodi Geofrey Comoro amewakumbusha wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu kwa walipakodi mara tu wanaposikia tangazo kutoka TRA ili kujua mabadiliko ya kodi yanapotokea.









No comments