HEADER AD

HEADER AD

WATOTO 869,040 SIMIYU KUPATIWA CHANJO YA POLIO



Na Annastazia Paul, Simiyu.

JUMLA ya watoto 869,040 wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Simiyu wanatarajia kupata chanjo ya matone ya polio katika awamu ya nne ambapo kampeni ya elimu kuongeza uelewa kwa jamii inaendelea.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa chanjo mkoa wa Simiyu Beatrice Kapufi kwenye kikao cha kamati  ya afya ya msingi ya mkoa ambapo chanjo hiyo itaanza Desemba, 1 hadi 4, 2022, amesema dawa za chanjo zimeshagawiwa na wanaendelea na kampeni ya kutoa elimu ili kuongeza uelewa kwa jamii na kuwafikia watoto wengi zaidi.

"Hii ni awamu ya nne tunatarajia kuchanja watoto 869,040 ambapo dawa zilizogawiwa ni 890,000 na tunatarajia kuwa na timu 1668 ambazo zitafanya zoezi hilo, lengo la kampeni hii tunayoendelea nayo ni kuongeza uelewa kwa wanajamii kuhusu faida ya chanjo ya polio.

" Pia kuwafikia watoto wengi zaidi watakaopata chanjo ya matone ya polio katika maeneo yetu na taasisi zetu na kuwafikia watoto wengi zaidi ili wapate chanjo itakayowaongezea kinga dhidi ya ugonjwa wa polio." amesema Kapufi.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda amemtaka mganga mkuu wa mkoa huo kuweka makadirio ya juu ya watoto wanaotarajiwa kupata chanjo ili kuwafikia watoto wengi zaidi huku akiwaasa viongozi wa dini kuwa sehemu ya  kuwahamasisha waumini wao ili wajitokeze kuwapeleka watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupata chanjo hiyo.


Dk. Nawanda amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu imejipanga kuhakikisha wanatoa chanjo zote kwa watoto ambao wanahitajika huku akiongeza kuwa zoezi hilo la utoaji wa chanjo litatekelezwa kwa asilimia 100 kwasababu kila kitu tayari kipo na kinachosubiriwa ni muda wa kuanza kuchanja.

"Nitoe rai kwa RMO basi tujipangie malengo yaliyo makubwa zaidi, naamini safari hii tumeweka makisio makubwa ili mwisho wa siku tupate nafasi na sisi ya kuwafikia walengwa walio wengi zaidi, rai nyingine kwetu sisi tuliohudhuria kikao hiki tukawe mabalozi wazuri katika zoezi hili.

"Nanyi ndugu zangu, viongozi wa dini kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili katika ibada zetu basi tukaweke msisitizo zaidi ili tuhakikishe wanajamii wanafahamu, lengo ni kuhakikisha kila kaya yenye mtoto aliye chini ya miaka mitano ambaye hajapata chanjo tuhakikishe wote wanapata, wadau wote hakikisheni mnashiriki kikamilifu." amesema Dk. Nawanda.


Mganga mkuu wa mkoa wa Simiyu Dk. Boniphace Marwa amesema idadi ya watu waliopata chanjo ya UVIKO 19 imeongezeka na kuuwezesha mkoa huo kupanda kutoka nafasi ya tatu kutoka mwishoni hadi nafasi ya tano kitaifa.

"Katika kipindi cha Agosti - Septemba tulikuwa nafasi ya tatu kutoka mwisho kwasababu hapa katikati kidogo hatukuwa na kampeni kutokana na ukosefu wa rasilimali mbalimbali, lakini tulipata wadau wakatushika mkono na sasa hivi tupo nafasi ya tano kitaifa, tumepanda juu hatupo mwisho tena."  amesema Dk.Marwa.






No comments