NYASI ZA ASILI ZAZIDI KUTOWEKA
Na Dinna Maningo , Tarime
MIFUGO mingi nchini Tanzania inategemea chakula cha Nyasi za asili ambazo hupatikanaji wake siyo mgumu ukilinganisha na nyasi za kisasa za kupandwa zinazopatikana katika baadhi ya maeneo na kwa gharama.
MIFUGO mingi nchini Tanzania inategemea chakula cha Nyasi za asili ambazo hupatikanaji wake siyo mgumu ukilinganisha na nyasi za kisasa za kupandwa zinazopatikana katika baadhi ya maeneo na kwa gharama.
Nyasi za asili hujiotea zenyewe juu ya ardhi bila kupandwa na Binadamu hivyo kuiwezesha mifugo kujipatia chakula kwa urahisi bila kutozwa fedha za malisho.
Kadri siku zinavyozidi kusonga nyasi za asili zinapungua kwa kasi na maeneo mengine zimetoweka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo shughuli za kibinadamu kama kilimo, shughuli za uchimbaji wa madini, mabadiliko ya Tabianchi na uharibifu wa mazingira, hali inayoathiri mifugo katika maeneo yenye changamoto ya malisho.
Wilayani Tarime Mkoa wa Mara baadhi ya nyasi za asili zinazidi kutoweka, ili kuzipata unalazimika kutembea mwendo mrefu takribani zaidi ya km 5 kuswaga ng'ombe kupeleka maeneo yenye nyasi ambayo bado hayajatumika kwa shughuli za wananchi huku wafugaji wengine wakilazimika kupanda nyasi za kisasa ili mifugo ipate chakula.
Je ni aina gani za nyasi zilizopotea ? Nyasi zipi zisizo rafiki kwa mifugo ? je wafugaji wamelazimika kupanda aina gani za nyasi ili kunusuru mifugo? Nini kauli ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo?.
DIMA Online imefika katika baadhi ya maeneo na kubaini uwepo wa changamoto za nyasi za asili baada ya kuzunguka huku na kule kuzitafuta, na imezungumza na wananchi wakiwemo wafugaji kufahamu hali ilivyo ya upatikanaji wa nyasi za asili.
Wafugaji wanakiri kutoweka kwa badhi ya nyasi za asili na zilizopo hazitoshelezi mahitaji ya mifugo huku majina ya nyasi wakiyataja kwa lugha ya Kabila la Kikurya, wanasema nyasi za asili zina faida kwa malisho zinachangia kuongezeka kwa maziwa na shughuli za ujenzi na zinanenepesha mifugo.
Wafugaji wanataja baadhi ya aina hizo za nyasi za asili kuwa ni Rumurwa, Runyeru, Kihongoro, Likengeng'e, Rusyaga, Matete, na Tutu ambazo zinaliwa na mifugo huku Nyasi ya Runyeru ikionekana kusifiwa na wafugaji wengi.
Nyasi ya asili
Ghati Marwa mkazi wa mtaa wa Nyamisangura anasema nyasi ya Runyeru ni nzuri ni aina ya Nyasi inayoota maeneo ya miinuko kama kwenye vilima " Kati ya nyasi zote runyeru ni aina ya nyasi tunayoiaminia ng'ombe akila anatoa maziwa mengi, ananenepa ni laini lakini sasa hivi huzipati mpaka utafute sana, mbali na malisho nyasi hizi tulizitumia kama ufagio unachuma unafagilia nyumba au unauza mfagio mmoja sh. 200 sasa hivi hazipatikani " anasema Ghati.
Rhob Muhere anasema mbali na malisho nyasi za asili ni muhimu kwa ujenzi ," kuna Nyasi inaitwa itutu hii ni nzuri kuezekea nyumba lakini inapatikana kwa shida ndiyo maana hata ujenzi wa nyumba za nyasi umepungua baada ya nyasi kukosekana mtu anaona ajenge hata slopu ya bati ,tumepoteza utamaduni wetu wa nyumba za nyasi" anasema Rhibi.
Sababu za kupotea nyasi za asili
Imebainika kuwa maeneo yaliyokuwa na nyasi za asili yamemalizwa na shughuli za kilimo, ardhi imezidi kutumika kulima mazao mbalimbali na kusababisha nyasi kutoweka.
Sadock Mrimi mkazi wa kijiji cha Matongo anasema nyasi za asili zilizopatikana kwa wingi kwa urahisi zinazidi kupungua na zingine kupotea kabisa katika maeneo ambayo zilipatikana kwa urahisi zikiwemo nyasi za Rumurwa, Kihongoro, Runyeru, Tutu, na matete.
" Nyasi za asili upatikanaji wake ni wa shida kuna ritete hii ni Nyasi ndefu yenyewe inawashawasha , ili upate mpaka uende kule eneo la Mukora, kadri watu wanavyolima mashamba nyasi za asili zinapungua maana maeneo yaliyokuwa na nyasi watu walilima wakapanda mazao kama mahindi, mtama na mihogo"
Bhoke Marwa mkazi wa mtaa wa Kokehogoma anasema siku zinavyokwenda nyasi za asili zinazidi kutoweka hali ambayo imesababisha mifugo kula nyasi zisizo rafiki ambazo zinawachana ulimi zikiwemo nyasi aina ya Rikoro. (aina ya nyasi inayopenda kuota eneo lenye chemichemi au kandokando ya mto)
" Nyasi zilizo rafiki kwa mifugo zimetoweka mifugo ikikosa nyasi inalazimika kula irikoro lenyewe siyo zuri kwenye ncha zake ni kali zinakata ulimi ng'ombe hawapendelei kula wanakula wakati wa ukame"anasema Bhoke.
John Marwa anasema " Mwandishi mifugo inakabiliwa na changamoto ya malisho hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho wakati huohuo hata maeneo yaliyo na nyasi za asili bado nyasi ni chache na upatikanaji wake ni wa shida ili upate nyasi za asili unalazimika kutembea umbali zaidi ya km 5-10 kuswaga mifugo kwenda kutafuta nyasi za asili.
" Kuna nyasi za Runyeru hizi ni kiaminio kwa mifugo ikila zinakua na maziwa mengi ,kwa hapa Halmashauri ya mji Tarime zinapatikana kata ya Nkende katika shule ya msingi ya Ncharo ukienda kule utazikuta.
Mwandishi wa DIMA Online akafunga safari hadi shule ya Msingi Ncharo nakushuhudia nyasi hizo kwa jina la kikurya Runyeru, ni nyembamba zinaota kwa kurefuka kwenda juu,upepo unapovuma nyasi hizo uinama na kuinuka ,zimeota eneo la mwinuko (mlimani) kwenye eneo la shule.
Nyasi hizo siyo nyingi ni chache zimeota eneo dogo ambalo ni la shule, zipo kwasababu uongozi wa shule umepiga marufuku wananchi kupeleka mifugo eneo la shule, zinatumiwa na wanafunzi ambao huzichuma kama ufagio kufagilia madarasa.
Marwa Chacha Mkazi wa Kijiji cha Nyakunguru Kata ya Kibasuka anasema shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu zimechangia kupotea kwa nyasi za asili kwamba watu walihamishwa kwenye maeneo yao waliyoishi na kwenda kujenga nyumba kweye maeneo ya wazi yaliyokuwa na nyasi za malisho.
" Baadhi ya wananchi wanoishi kwenye Vijiji vilivyopakana na Mgodi wa North Mara walihamishwa na mgodi ukachukua maeneo kwa ajii ya shughuli za mgodi ,watu hao wakahamia kwenye maeneo yaliyokuwa tupu wakajenga nyumba na kuanzisha shughuli za kilimo na maeneo mengine kwakuwa ni ya dhahabu yakamilikiwa na watu kwa ajili ya shughuli za wachimbaji wadogo.
Annastazia Mkami mkazi wa kijiji cha Kewanja anasema Mabadiliko ya Tabianchi na uharibifu wa mazingira yameathiri upatikanaji wa nyasi za asili, wakati wa kiangazi maeneo yenye nyasi za asili hupotea kutokana na kupigwa jua hivyo huchipua msimu wa mvua.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kerende Mniko Magabe anasema ongezeko la idadi ya watu imesababisha maeneo yaliyokuwa na nyasi kuondolewa na kujenga makazi ya kuishi na maeneo mengine kutumika katika shughuli za uchimbaji wa madini.
"Kuna mlima kulikuwa kuna nyasi nzuri laini tunaita kwa kikurya (Urunyeru) watu walikuwa wanapita kwenda kulisha mifugo, lakini ongezeko la makazi likasababisha watu kuziba njia, watu wamejenga miji imeongezeka, mashamba na uchimbaji wa dhahabu pamebanana ng'ombe hawapiti tena," anasema Mniko.
Mzee wa Mila ambaye ni Katibu wa koo ya Nyabasi Jamii ya Kabila la Wakurya waishio Tarime Julius Nyang'ora anasema nyasi za asili zimepotea katika baadhi ya maeneo kutokana na watu kulima mashamba katika maeneo ambayo nyasi zilipatikana jambo ambalo limesababisha mifugo kukosa malisho ya kutosha.
" Watu wamelima sana kwenye yale maeneo ambayo awali hayakulimwa yaliyokuwa na nyasi nyingi za asili, ukilima zinaota nyasi zingine ambazo siyo rafiki kwa chakula cha mifugo mf.kuna nyasi tunazitambua kwa jina la kikurya urumurwa hizi ni nyasi nzuri lakini zinazidi kupotea maana zenyewe zinapenda kuota kwenye mahame ambayo ndiyo yana rutuba, kwa sasa ni chache kuzipata mpaka utafute sana.
Kwa mujibu wa Kitini kilichoandaliwa na Idara ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kinaeleza kuwa Malisho ni chakula cha msingi cha mifugo kinachojumlisha aina mbalimbali za nyasi na mikunde.
Inaelezwa kuwa utunzaji wa malisho ni muhimu ili kuhakikisha kwamba mifugo inapata chakula bora na cha kutosha wakati wote . Ukuaji na ustawi wa aina za malisho hutofautiana kutegemea hali ya hewa na mazingira mbalimbali.
Kitini hicho kinaeleza faida ya kupanda malisho, hurahisisha upatikanaji wa chakula cha mifugo chenye viini - lishe Kama wanga, protini, Madini na vitamini ,hurutubisha ardhi hasa malisho aina ya mikunde. Huzuia mmomonyoko wa ardhi. Miti malisho kama lukina,Sesbania na Grilicidia hutumika kama kuni na Kinga ya upepo.
Idara hiyo ya malisho inataja baadhi ya aina za nyasi za kupandwa zilizofanyiwa utafiti wa kitaalamu ni Guatemala ( Tripscum Laxum) ambayo hustawi zaidi kwenye eneo lenye mvua ya wastani , Mabingobingo/ Bana grass ambayo hustahimili ukame, Guinea grass malisho hustawi katika aina mbalimbali za udongo na kuvumilia ukame na joto.
Zingine ni Rhodes grass hustawi katika maeneo yanayopata mvua za wastani hadi nyingi ambapo nyasi Jamii ya mikunde ni Desmodium ambayo hustawi vizuri, huvumilia ukame kiasi na huchipua haraka baada ya kukatwa pamoja na Miti ya Lukina ( Leuceana leucocephala) ambayo hupandwa kwa kutumia mbegu moja kwa moja shambani au kwenye vitalu na Miche kuhamishwa shambani.
Sera ya Taifa ya Mifugo
Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 inaeleza kuwa sekta ya mifugo hutoa mazao mengi ya mifugo yanayotumika nchini na hivyo kupunguza uagizaji wa mazao hayo kutoka nje ya nchi. Mchango wa sekta ya mifugo kwenye uchumi wa Taifa, huchagia katika kuzalisha chakula, hivyo kuchangia katika ukahika wa chakula.
Mazao mengine ni kubadilisha malisho na masalio ya mazao kuwa chakula,chanzo cha mapato na ajira kwa wananchi wa vijijini, kutoa ngozi za mazao mengine,kutoa mbolea na wanyama kazi kwa ajili ya kilimo endelevu na kuchangia katika majukumu ya kijadi kwenye jamii.
Sera hiyo inaeleza kuwa,vikwazo vinavyokabili maendeleo katika sekta ya mifugo ni tatizo kubwa katika mfumo wa umilikaji wa ardhi, rasilimali za maji na malisho ni kutokuwa na utaratibu wa kutenga na kumilikisha ardhi kulingana na taratibu za sheria au kimila.
Post a Comment