HEADER AD

HEADER AD

DC ITILIMA AWANYOSHEA KIDOLE WAHUJUMU MIRADI YA MAJI


Na Mwandishi wetu, Itilima

SERIKALI wilayani Itilima mkoa wa Simiyu, imewaonya baadhi ya watu wanaohujumu miundombinu ya maji iliyojengwa na wadau wa maendeleo ili kusogeza karibu huduma kwa jamii.

Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Faiza Salim Novemba 2,2022 wakati akikagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Shirika la World Vision wilayani hapo na kusema kuwa serikali haitosita kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya uharibifu kwenye miradi inayotekelezwa.

Amesema licha ya wadau wa maendeleo kujitahidi kutumia gharama kubwa ili kuwasogezea wananchi huduma muhimu kwa lengo la kuwasaidia kuondokana na adha mbalimbali zinazowakabili, baadhi yao wamekosa uaminifu na kuamua kufanya uharibifu.


"kufanya hivyo ni kuwakatisha tamaa wadau waliojitoa kutekeleza miradi kwa lengo la kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto zinazowakabili hivyo hatutamvumilia 
yeyote atakayehujumu miradi na yeyote atakayeshindwa kuendana na utekelezaji atafute sehemu itakayomfaa kuishi," amesema Faiza.

DC Faiza hajaweka wazi hasara zilizosababishwa na uharibifu  wa miundombinu hiyo lakini amewataka wananchi  kila mmoja kwa nafasi yake kulinda na kuitunza miradi yote ili isiharibiwe kwa ajili ya manufaa ya baadae huku akisisitiza utoaji taarifa.

Amesema endapo itabainika mradi wowote umehujumiwa lakini viongozi wa maeneo husika wakaa kimya bila kutoa taarifa wao pamoja na kijiji kizima watawajibishwa.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha kilugala eneo ambalo limemwamsha DC Faiza baada ya hujuma ambazo hazikuwekwa wazi zilizofanyika katika mradi uliogharimu Tsh. Milioni 460 wameeleza adha walizokuwa wanakabiliana nazo kabla ya mradi huo.


Mkazi wa kijiji cha Kilugala Lulu Mang'ombe amesema," Kabla ya kupata mradi huo tulikuwa tunalazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya  kilomita tano kwenda kutafuta maji na yalikuwa yanapatikana kwa shida," amesema.

Wakieleza juu ya uharibifu wa mradi wa maji Mang'ombe wamekili kufanyika kwa uhujumu katika mradi huo hali iliyosababisha wastishwe kuchota maji bure na kulazimika kulipia hivyo kusababisha sintofahamu kwao wakidai hawakuwa na taarifa ya kutosha juu ya mradi huo na sababu ya mabadiliko. Hata hivyo  kwa sasa maji yameanza kutolewa bure.

Mratibu wa mradi wa maji wa Kanadi na Luguru, Nyamoko George amesema mradi huo unanufaisha zaidi ya watu 8, 000 pamoja na vijiji 3 ambapo umegharimu kiasi cha Tsh Milioni 460.


Shirika hilo limefadhili mradi wa ujenzi wa vyoo matundu 8 uliogharimu kiasi cha Tsh Milioni 42 ambapo wanafunzi zaidi ya 1000 wananufaika na mradi huo huku kukitajwa kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa vyoo matundu 28 kwa wasichana na 38 kwa wavulana.

Ujenzi wa Zahanati ya Ikungulipu iliopo katika kata ya Luguru umegharimu kiasi cha  Tsh. Milioni 142 na wanahudumia wagonjwa 80 kwa siku ambapo pia katika mradi wa maji wa Nangale uliogharimu Tsh.Milioni 217 umewezesha kunufaisha zaidi ya wananchi 2000.






No comments