OCD TARIME ASHTUKIA WIZI WA PIKIPIKI ZIKIWA ZIMEEGESHWA
Na Dinna Maningo, Tarime
MKUU wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Polisi Tarime, SSP Ramadhani Sarige amesema wizi wa Pikipiki umerudi tena huku wezi wakitumia mbinu mpya ya kuiba pikipiki zikiwa zimeegeshwa na wengine kuiba kwa njia ya kupora pindi wanapokuwa wamebebwa kwenye pikipiki.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wamiliki na waendesha Pikipiki mjini Tarime, Novemba, 28, 2022 katika ukumbi wa Polisi wakipewa elimu ya kutii sheria bila shuruti pamoja na umuhimu wa leseni ya usafirishaji , leseni ya udereva iliyotolewa pia na Maafisa wa Serikali kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Mara, Kikosi cha Usalama Barabarani Tarime Rorya, na TRA.
SSP Ramadhani amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka wezi wa pikipiki huku akiwaomba waendesha pikipiki kuwa makini wanapoendesha pikipiki zao na watoe ushirikiano pindi wanapowabaini wezi wa pikipiki.
"Wizi wa pikipiki unarudi tena kuna ripoti Bodaboda wanaibiwa pikipiki, ila wezi wamekuja na staili ya kubeba pikipiki ikiwa imepaki na wengine wanaporwa wakiwa wanasafirisha abiria, au kwa njia za utapeli, tunaomba ushirikiano wenu," amesema" Ramadhani.
Frankus Kalugendo ni miongoni mwa walioibiwa pikipiki ikiwa imeegeshwa amesema" Niliibiwa pikipiki mwezi uliopita ikiwa imepaki tukiwa kwenye mkutano wa injili Sirari, nilitoa taarifa Polisi ila bado haijapatikana Tunaendelea kuitafuta.
"Watu wanadai kuwa pikipiki zikiibwa hupelekwa Kenya au kwa wavuvi huko ziwani ambapo hutoa injini ya pikipiki na kuitumia kwenye boti" amesema Frank.
Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Pikipiki Wilaya ya Tarime, Joseph James amesema amekuwa akipokea taarifa za wizi wa pikipiki na ushirikisha Jeshi la Polisi kwa ajili ya ufuatiliaji kwa kushirikiana na waendesha pikipiki.
"Tumekuwa tukipokea taarifa za wizi wa pikipiki, tangu mwaka jana hadi sasa pikipiki 22 ziliripotiwa kuibiwa kati ya hizo nane zimeibwa zikiwa zimeegeshwa mfano mtu anapaki pikipiki yake anaingia sokoni akirudi hakuti pikipiki na umeifunga umeondoka na funguo lakini wanaiba na kuondoka nayo, amesema Joseph.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Polisi Tarime, ASP Barnaba Irumba amesema kuna pikipiki moja imekamatwa iliyokuwa imeibiwa na kwamba kama kuna mtu aliibiwa afike Polisi Bomani aione aitambue kama ni yake.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, SSP Denis Kunyanja amewashauri wamiliki na waendesha pikipiki njia ya kupata pikipiki pindi inapoibiwa.
"Kuna Kampuni ipo Mwanza ambayo ukiibiwa pikipiki ukawapa taarifa wanaifuatilia hatua kwa hatua hadi inakamatwa hata uibe uendeshe kupeleka wapi itakamatwa, kuna kifaa kinafungwa kwenye pikipiki yako ikiibiwa kokote itakakopelekwa wanaona.
" Baadhi ya pikipiki zilizoibiwa zimekamatwa kwa njia hiyo, mimi nipo tayari kuwaita waje wawape elimu ya kulinda pikipiki zenu kama mtakuwa tayari ili tudhibiti wizi wa pikipiki " amesema Denis.
Hata hivyo wamiliki na waendesha Pikipiki wamekubali ushauri huo nakuomba kampuni hiyo ifike Tarime ili kuwapatia elimu ya jinsi ya kulinda pikipiki zao.
Wakati huo, MKUU wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Polisi Tarime, SSP Ramadhani Sarige amewataka waendesha vyombo vya moto kuwa makini hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho mwa mwaka ambapo ajali uongezeka na kwamba suala la usalama ndio ajenda hivyo kila mtu anatakiwa kuzingatia Sheria za Barabarani.
Post a Comment