HEADER AD

HEADER AD

SHERIA YA LESENI ZA USAFIRISHAJI KUWASHUKIA BODABODA MARA

Na Dinna Maningo, Tarime

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Mara, imewataka wamiliki wa Pikipiki kukata leseni ya usafirishaji kwakuwa inatoa uthibitisho wa mtu anayefanya biashara ya usafirishaji na endapo asipokuwa na leseni atawajibishwa kwa mujibu wa sheria ya usafirishaji .

Imeelezwa kuwa mtu anapokuwa na leseni ya usafirishaji ni uthibitisho kwamba amekidhi vigezo vinavyohitajika yeye kubeba abiria ama kubeba mizigo hivyo kunakuwa na masharti ya kumwezesha kupata leseni ya usafirishaji.

Akitoa elimu ya kutii sheria bila shuruti na umuhimu wa leseni ya usafirishaji kwa wamiliki na waendesha pikipiki Wilayani Tarime , Afisa Mfawidhi Mamlaka ya Udhibiti Usafirishaji (LATRA) Mkoa wa Mara, Ngereza Pateli amesema gharama ya leseni za usafirishaji ni Tsh. 17,000 zinazopatikana ofisi ya LATRA, ofisi ya Afisa Biashara wa Halmashauri pamoja na mtandaoni.

Amesema wamiliki walio wengi hawana leseni ya usafirishaji kitendo ambacho ni kinyume cha Sheria ya Usafirishaji ya mwaka 1973 iliyofanyiwa mapitio ya mwaka 2019.

"Huduma ya usafirishaji ina sheria ambayo imetungwa na Bunge ambayo inasimamiwa, sheria ya leseni za usafirishaji ya mwaka 1973 ilikuwa haitambui pikipiki ya magurudumu mawili na matatu kufanya biashara ya usafirishaji, mwaka 2009 sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na Bunge.

" Mwaka 2010 zikatungwa kanuni ambazo ndizo zilikuwa zinatumiwa na iliyokuwa SUMATRA, ilivyofika 2019 ikatungwa sheria iliyoanzisha LATRA na kufuta ile ya SUMATRA, sheria ile ya 1973 na mapitio yake ya 2009 zinatambua  Bodaboda na Bajaji na zimeendelea kutumiwa na LATRA.

Ameongeza" Kisha mwaka 2020 zikatungwa kanuni  za kurahisisha kutumia hizo sheria kwa wadau na endapo usipokuwa na hiyo leseni kuna adhabu ukikamatwa faini ni Tsh 25,000, zamani ilikuwa laki moja ikapunguzwa.

" Usipotoa afisa anatakiwa kukupeleka mahakamani na kule utalipa mara mbili ya ile anayokulipisha ofisa, yaani Tsh 50,000 au ukafungwa kifungo kisichopungua miezi sita jela ama vyote pamoja" amesema Ngereza.

Amesema sheria ya leseni za usafirishaji ndiyo inayowapa wasafirishaji uwezo wa kufanya biashara ya usafirishaji hivyo sheria hiyo ndiyo inawasimamia wafanyabiashara wa usafirishaji.


"Taratibu zilizowekwa kwenye kanuni zinamtaka yeyote anayefanya biashara ya usafirishaji lazima aingie kwenye kundi la kufanya biashara, pikipiki hiyo iwe na peti namba kwa maana ya kibao chenye rangi nyeupe chenye maandishi meusi, lazima anayetaka kufanya biashara ya usafirishaji awe ni mtanzania.

"Awe amasejiliwa na mamlaka ya Mapato na kupewa kadi ya pikipiki inayoonesha yeye ni mfanyabiashara wa kitanzania, sheria hiyo inamuelekeza huyo mtu mwenye bodaboda (pikipiki) ahakikishe kwamba anapata leseni ya kufanya biashara kutoka kwenye mamlaka inayotoa leseni hizo ,huruhusiwi kufanya biashara ya usafirishaji bila kuwa na leseni ya usafirishaji" amesema Ngereza.

Ameongeza" Vigezo vinavyotakiwa ili upate leseni ya usafirishaji unatakiwa kuwa na leseni ya udereva chombo unachohitaji kutoa huduma ya usafirishaji, uwe na dereva mwenye leseni ya udereva , pikipiki iwe imekatiwa Bima, lazima pikipiki iwe katika muundo wa utoaji huduma ya usafirishaji iwe na miundombinu yote ya kuweza kubeba abiria

Anasema mtu anapokwenda kuchukua leseni anapaswa kwenda na vitu hivi;  " Lazima awe na kadi ya usajili wa pikipiki husika ,mmiliki anatakiwa kuwa na kitambulisho cha mpiga kura na kwamba mtu anaponunua chombo cha usafirishaji anatakiwa kubadilisha umiliki wake.

" Ada ya leseni hiyo ni 17,000 kwa mwaka mzima, ambayo utalipa kupitia ankra ya malipo ya serikali (Control Namber) alafu atalipia mwenyewe kwa kupitia benk au namba yake ya simu kisha atapatiwa leseni" amesema Ngereza.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, SSP Denis Kunyasa amesema serikali imeweka sheria zake na ili mfanyabiashara awe halali anatakiwa awe na vigezo vinavyotambulika.


SSP Denis amesema asiyekuwa na vigezo vilivyowekwa kisheria atawajibishwa hivyo wamiliki na waendesha pikipiki wanapaswa kutii sheria bila shuruti.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Pikipiki Wilaya ya Tarime Joseph James amesema wamiliki na waendesha pikipiki zaidi ya 300 wameshiriki elimu hiyo ya kutii sheria bila shuruti kuhakikisha wanakuwa na leseni zinazowaruhusu kufanya biashara zao.


Pia amekipongeza Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, LATRA na TRA kwa kutoa elimu kwa wamiliki na waendesha pikipiki na kwamba elimu waliyoipata wataifikisha kwa waendesha Pikipiki ambao hawakubahatika kushiriki katika elimu hiyo.



No comments