HEADER AD

HEADER AD

RAIS SAMIA AVUTIWA NA KANISA LA WASABATO LINAVYOWALEA WATOTO, VIJANA


Na Dinna Maningo, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu amesema amefurahishwa na kuvutiwa na Kanisa la Waadventista Wasabato namna wanavyowaandaa na kuwalea watoto na vijana ili wakue katika maadili mema na kumcha Mungu.

Rais Samia ameyasema hayo Novemba, 19, 2022 wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Utume na Huduma ya Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kati mwa Tanzania yaliyofanyika katika makao yake makuu Jijini Dodoma.

Rais Samia amelipongeza kanisa hilo kwa kazi kubwa ya kutangaza habari njema na wokovu na kuielekeza mioyo ya watanzania, waumini wa kanisa hilo kwa Mwenyezi Mungu kupitia Yesu Kristo.

"Nimekuwa nikishiriki katika shughuli kadhaa zinazoandaliwa na madhehebu mbalimbali ya dini lakini kwa bahati mbaya sikuwa nimepata nafasi kujumuika na wasabato, na leo ni heshima kwangu kuwa na Kanisa la Waadventista Wasabato.

" Kwa baraka za Mungu leo nimepata fursa hii hadhimu kukutana nanyi kwenye siku hii takatifu ya Sabato kwa ajili ya tukio muhimu, hii ni baraka na neema ya kipekee kwangu, nawashukuru sana kwa mapokezi makubwa" amesema Rais Samia.

Rais Samia amevutiwa kuona katika Kanisa hilo kuna watoto na vijana wanafahamu kupiga gwaride huku akifurahishwa na nyimbo nzuri zilizoimbwa na kwaya ya Nyarugusu pamoja na kwaya ya wanafunzi wa shule ya msingi Ellen White.

"Nimewakuta vijana wangu wakipiga Gwaride vizuri wakanivisha skafu nikasema mpaka kanisani kuna gwaride kumbe!. Ni vijana waliotengenezwa na wameiva, kwahiyo nawashukuru sana mwenyezi Mungu awabariki kwa ukarimu wenu" amesema.


        Vijana wa Chama cha Watafuta njia (Pathfinder Club) wa Kanisa la Waadventista wa Sabato wakimvalisha skafu Rais Samia Suluhu.

Ameongeza kusema,"Jambo lingine linalonifurahisha na kunivutia katika kanisa hili ni namna mnavyowaandaa na kuwalea watoto na vijana ili wakue katika maadili mema na kumcha mwenyezi Mungu, na nimefurahishwa mno mno mno na kwaya zilizoimba.

" Wameimba maudhui ya kidini wamejengwa mioyo yao kidini, wameimba maudhui ya kizalendo wamejengwa kizalendo na niwaimbaji wazuri mno wanaimba vizuri mno, kwahiyo niwashukuru sana kwa uimbaji huu mzuri" amesema Rais Samia.

         Kwaya ya Nyarugusu

Rais Samia ametoa wito kwa viongozi wote wa dini wa madhehebu mbalimbali  nchini kuwahimiza waumini kuzingatia Mila, Tamaduni na Maadili ya Kitanzania.

"Bila kuwa na vijana waadilifu, Magereza yetu yangekuwa yamejaa, vyombo vya ulinzi na usalama vingekuwa na kazi ngumu sana ya kupishanapishana huku panya rodi, huku panya njia ingekuwa kazi kubwa sana na majaji wetu wangekuwa na kazi kubwa.

"Kwa hiyo niwashukuru sana kwa kutusaidia ulezi, kutusaidia kujenga maadili na kukuza uzalendo wa Taifa.Na huo ni wito kwa viongozi wote wa dini zetu wa madhehebu mbalimbali nchini kuimiza waumini kuzingatia maadili ya kitanzania" amesema Rais Samia.

Katibu Mkuu wa Jimbo la Kusini mwa Tanzania Mch. Jeremiah Izungu akisoma taarifa ya Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania, amesema katika kipindi chote kanisa linafanya kazi kubwa katika kulea waumini wake kiroho, kimwili na kiakili, pia kutoa mchango mkubwa wa kuimalisha maadili na kuimalisha huduma za kijamii.


Amesema katika shughuli za kiroho Kanisa limeendelea kuweka msisitizo mkubwa kwa jamii ya Tanzania kumcha Mungu na kuchukia maovu na imewezesha kuimalisha kazi ya kiroho lakini pia kujenga jamii inayozingatia maadili na kuchukia maovu ya aina zozote.





No comments