HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WAPINGA KAULI YA DC KISWAGA, WASEMA AMEPOTOSHWA


Na Daniel Limbe, Kahama

SIKU chache baada ya Mkuu wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Festo Kiswaga, kuelezea malalamiko ya mgogoro wa wananchi dhidi ya mgodi wa Barrick Gold, na kudai kuwa wananchi wote waliokuwa na maendelezo ya ardhi yao walilipwa stahiki zao ispokuwa ardhi pekee, baadhi ya wananchi wamepinga kauli hiyo.

Awali akizungumza na DIMA Online Kiswaga alitoa msimamo kwa wananchi wa Kakola wanaodai fidia kuwa hawawezi kulipwa madai yao kutokana na sheria iliyokuwepo wakati maeneo yao yanatwaliwa na serikali mwaka 1996 kutowapa haki ya kupata fidia.

Mbali na wananchi hao kutambua kuwa sheria iliyokuwepo haikuwapa haki ya kulipwa fidia ya ardhi, wamepinga vikali kauli ya Dc ya kwamba walilipwa maendelezo ya ardhi zao huku wakisema waliompa taarifa hizo walilenga kumpotosha.

Aliyekuwa Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Kakola mwaka 1996, George Kingi, amesema serikali iliwaondoa kwa nguvu wananchi waliokuwa kwenye vitongoji vitano pasipo hata kufanya uthamini wa mali zilizokuwepo maeneo hayo, badala yake wananchi waliamuliwa kuondoka na baadaye ililetwa mitambo na kuanza kusafisha maeneo yote pasipo kujali mali zilizowekezwa na wananchi hao.

"Wananchi waliondolewa kwa nguvu pasipo huruma, watu walipoteza mazao ya chakula, miti, makaburi, nyumba na hata visima walivyokuwa wametengeneza kwa nguvu zao, baada ya kuwaondoa wote mwaka 1997 na 1998 wakaitwa watu wasiozidi 15 ndio wakaambiwa watalipwa fidia" amesema.

"Kwa hali ya kawaida unaweza kufikiri mwenyewe je, vitongoji vitano vilivyosajiliwa na serikali vinaweza kuwa na watu wasiozidi 15 tu waliowekeza kwenye ardhi yote anayosema mkuu wa wilaya kuwa watu walilipwa"? alihoji Kingi.

George amesema iwapo watu walilipwa maendelezo wanamuomba Rais Samia awathibitishie kwa vielelezo vya majina ya watu wote waliolipwa mali zao kwa kile walioeleza kuwa imani yao imebaki kwa Rais Samia pekee.

Fabian Rwandobe,aliyekuwa mwenyekiti wa kitongoji cha namba mbili, amethibitisha kuwa hakuna mwananchi hata mmoja aliyelipwa fidia yoyote mwaka 1996 na kwamba yeye ni miongoni mwa wananchi waliovunjiwa nyumba zake pamoja na kusambazwa kwa kaburi la mwanaye wa kike aliyemzika katika eneo hilo.

"Nakuthibitishia hakuna mwananchi aliyelipwa fidia yoyote mwaka 1996, isipokuwa kwa wachache tu waliogoma kuondoka maeneo hayo ambao mwaka 1997 na 1998 walifanyiwa tathmini ya mali iliyokuwa imesalia ndio hao walilipwa. Nyumba zangu zilivunjwa na skaveta hadi likasambaza na kaburi la mwanangu wa kike" amesema Rwandobe.

Amesema ombi lao kubwa ni kwa Rais Samia aweze kuwasaidia wananchi hao wanyonge kupata angalau jasho lao kwa kuwa baadhi ya viongozi wa umma wamekuwa wakikwamisha jitihada za fidia yao badala yake wamekuwa wakijinufaisha binafsi kupitia mgogoro huo huku walengwa wakiambulia patupu zadi ya miaka 25 iliyopita.

Bombazi Antony Mkazi wa Kijiji cha Kakola amesema mashamba yake mawili yalifanyiwa uthamini mwaka 2012 ambapo shamba moja alipaswa kulipwa Tsh Milioni 85 na lingine Tsh. Milioni 33, lakini mwaka 2013 aliitwa na kupewa fidia ya Tsh 6,150,000 na shamba la pili alipewa  Tsh m Milioni 14 huku pesa zingine akiahidiwa kulipwa bila mafanikio hadi sasa.

Hamis Mwitazi, maarufu(Burebure) ambaye ni msadizi wa kisheria kutoka shirika la Chalao, amesema Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 Ibara ya 24 (2) inatamka wazi kuwa, Bila kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1) ni marufuku kwa mtu yoyote kunyang'anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengineyo bila idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili.

Wananchi wamemuomba Rais Samia Suluhu kuingilia kati mgogoro huo siyo kutaka fidia ya ardhi yao isipokuwa wanaomba angalau wapate fidia ya maendelezo yao kwa kuwa baadhi yao waliwekeza nyumba za makazi, nyumba za kulala wachimbaji (Guest), mashamba, miti na wengine walikuwa wamestili wapendwa wao waliofariki duniani.


Awali kupitia
DIMA Online Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga Festo Kiswaga alisema Wananchi wa Kijiji cha Kakola wanaodai fidia ya ardhi hawatalipwa kwakuwa walifanyiwa uthamini wakati wa sheria iliyokuwa ya kikoloni ambayo haikutambua malipo ya fidia ya ardhi.

Kiswaga alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi wa Kakola kupitia chombo hiki cha Habari wakimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kuingilia kati mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 kati yao na Mgodi wa Barrick Gold Corporation.

DC Kiswaga alifafanua " Huu mgogoro naujua, ukweli ni kwamba  wakati mgodi unachukua maeneo kulikuwa na sheria iliyokuwa inatumika ya mkoloni ambayo haikutambua haki ya fidia ya ardhi.

"Ulipofanyiwa uthamini ulikuwa hulipwi fidia kwahiyo watu waliofanyiwa uthamini wakati wa Sheria hiyo ya ardhi hawakulipwa kwakuwa ardhi haikuwa na thamani ,ulilipwa vile vilivyoendelezwa kama umejenga nyumba au umepanda miti, miembe unalipwa ila ardhi hulipwi mgogoro umetokana na hiyo sheria, hao hawatalipwa chochote" alisema Festo.

Aliongeza kuwa mgogoro huo ulishafika hadi Ofisi ya Waziri Mkuu lakini majibu ni yaleyale kuwa hawawezi kulipwa vivyohivyo na Wizara ya ardhi, kwamba wananchi walielezwa hawastahili kulipwa kwasababu ya sheria ya wakati huo, Waziri wa Madini, Mbunge wanalijua hilo.

REJEA:

Andiko la Mwanasheria Obedi Mathayo Ngilisho kupitia Mitandao ya Kijamii la Juni, 20, 2018 limeeleza mfumo wa milki ya ardhi wakati wa mkoroni kwamba;

MFUMO WA MILKI YA ARDHI WAKATI WA UKOLONI (1890- 1960)

Tanganyika ilitawaliwa na Wajerumani na Waingereza:-

Wajerumani (1890–1919)

>>>Tamko la Wajerumani la mwaka 1895 liliweka bayana kuwa ardhi yote ni mali ya Mfalme Kaiza wa Ujerumani.

>>>Walianzisha umiliki kwa njia ya Hati.

Waingereza (1919–1961)

>>>Walitunga sheria ya Ardhi na 3 ya 1923 kuweka msisitizo katika mfumo ulioanzishwa na Wajerumani na kutamka kuwa ardhi yote ni mali ya umma chini ya Gavana.

>>>Umiliki wa hati ulikuwa na nguvu kisheria dhidi ya umiliki wa kimila

Katika kipindi cha ukoloni wazawa walipoteza sauti juu ya ardhi yao.

C. KIPINDI CHA UHURU HADI SASA

Kipindi cha miaka ya 1961- 1990

>>>Mamlaka ya Gavana juu ya ardhi ilihamishiwa kwa Rais.

>>>Mwaka 1967 Azimio la Arusha lilitangazwa kuweka misingi ya uzalishaji mali mikononi mwa umma.

>>>Sheria zilizotungwa katika kipindi hiki ni pamoja na Sheria ya Utwaaji Na. 47 ya 1967 ambayo iliwezesha utwaaji wa ardhi kwa matumizi mbalimbali kama vile uanzishwaji wa Mashamba ya NAFCO na NARCO na Sheria ya Vijiji na Vijiji vya Ujamaa Na. 21 ya 1975 ambayo ilihalalisha uanzishwaji wa Vijiji vya ujamaa.

Kipindi cha kuanzia 1991 hadi sasa

>>>Licha ya kuwepo kwa Sheria hizo bado vijiji vingi viliendelea kuwa na migogoro kutokana na kuingiliana kwa haki na maslahi kati ya wakazi wa vijiji vipya na vya zamani

>>>Migogoro hiyo ilipelekwa kuundwa kwa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Masuala ya Ardhi mwaka 1991.

>>>Mwaka 1992 ilitungwa Sheria ya Milki ya Ardhi Tanzania ambayo ilifuta Vijiji vya asili na kuhalalisha vijiji vya ujamaa.

Tume ilitoa mapendekezo yake mwaka 1992 ambayo ni pamoja na:-

>>>Ardhi ipewe ulinzi wa Kikatiba

>>>Kuwepo na Sera na Sheria ardhi za kizalendo

>>>Kuweka milki ya hatma kwenye vyombo vyenye uwakilishi mpana wa wananchi

>>>Kuunda mfumo wa usuluhishi na utatuzi wa migogoro ya ardhi kuanzia ngazi ya kijiji

>>>Ardhi igawanywe katika makundi

Mapendekezo hayo yalipelekea kutungwa kwa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sheria za Ardhi Na. 4 na Na. 5 za mwaka 1999.


                     

No comments