HEADER AD

HEADER AD

WAADVENTISTA WA SABATO WAMWANGUKIA RAIS SAMIA UHURU WA KUABUDU


Na Dinna Maningo, Dodoma

IMEELEZWA kuwa usaili wa nafasi za kazi zinazotangazwa na serikali pamoja na mitihani ya vyuo na shule kufanyika siku ya jumamosi ambayo ni siku ya ibada takatifu kwa waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania, kitendo hicho kinawanyima haki vijana kuingia kwenye mchakato wa kupata ajira.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania Kanisa la Waadventista wa Sabato Mch. Jeremiah Izungu wakati akisoma Taarifa ya Kanisa hilo Novemba, 19, 2022 katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Utume na Huduma ya Kanisa hilo Jimbo la Kati mwa Tanzania yaliyofanyika katika makao yake Makuu Jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu akiwa ameongozana na baadhi ya viongozi wa serikali wameshiriki maadhimisho hayo na kuwahutubia viongozi na waumini wa kanisa hilo na akazindua ujenzi wa kanisa la Dodoma na kuzindua mnara wa kumbukumbu ya Jubilee ya miaka 50 ya Utume na Huduma.

Mch. Jeremiah Izungu amesema " zipo changamoto ambazo kanisa limekuwa likikutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake, changamoto hizo ni pamoja na usaili wa nafasi za kazi zinazotangazwa na serikali mara nyingi hufanyika siku ya jumamosi ambayo ni siku ya ibada takatifu, kitendo hiki kina wanyima haki  vijana wa kiadventista kuingia kwenye mchakato wa kupata ajira.

     Rais Samia akihutubia Kanisa la Waadventista wa Sabato

"Kwa kufanya hivyo kunafanya vijana wetu wenye sifa wasipate nafasi ya kulitumikia Taifa lao la Tanzania. changamoto nyingine ni uhuru wa kuabudu, baadhi ya vyuo na shule wanafanya mtihani siku ya ibada ya jumamosi.

" Pamoja na miongozo mbalimbali kutolewa na serikali bado baadhi wanalazimisha waadventista kufanya mitihani na wanapoacha kufanya mitihani wanakatili njozi zao za kuendelea na masomo yao ambayo ni haki ya msingi kwa kila mtanzania" amesema Mch.Jeremiah.

Amesema changamoto nyingine ni uhaba wa wataalamu wabobezi kwenye hospitali za kanisa, hivyo kanisa hilo limemuomba rais Samia kuwafutia kodi inayotozwa kwenye taasisi zao za elimu za kanisa ili kurahisisha utoaji huduma kwa jamii ya watanzania.

Mch.Jeremiah ameiomba serikali kuwapatia wataalamu wabobezi kwenye hospitali zao na kwamba serikali itambue kuwa kanisa la Waadventista wa Sabato ni jamii ya Kikristo isiyokuwa chini ya mwamvuli wowote wa madhehebu ya Kikristo kama vile CCT, TEC na CPTC, hivyo linajitegemea.

Akijibu maombi ya kiongozi huyo wa dini, Rais Samia amesema amesikiliza changamoto hizo zilizotajwa na amepokea maombi yote ameyabeba na watayafanyia kazi na kuwapatia mrejesho baada ya mashauriano na wenzake serikalini.

       
"Nimesikiliza changamoto kwanza mmetaja suala la usaili na mitihani kufanyika siku ya Jumamos ambayo ni siku ya ibada , nilikuwa namtania baba askofu nikamwambia sasa kama watu wanaitwa kwenye usaili jumamosi au anafanya mtihani anakwenda ameshiba Yesu Kristo moyoni siku takatifu huyo ni dalili tosha anayekwenda siku hiyo anaenda kufaulu.

"Kwa hiyo hilo la kusema jumamosi wasifanye usaili tutaliangalia vizuri lakini naona waende na ile mioyo kwamba nakwenda kwa nguvu za Yesu na mtakwenda kushinda, na nimesikia maombi yenu ya kutaka kufutiwa Kodi inayotozwa kwenye taasisi za elimu za kanisa ili kurahisisha huduma kwa jamii.

"Uhitaji wa madaktari bingwa kwenye hospitali zenu na kutambuliwa kwenye serikali kuwa kanisa linajitegemea halipo chini ya mwamvuli wowote wa umoja wa madhehebu ya Kikristo maombi nimeyachukua" amesema.

Ameongeza ,"Natambua deni nililorithi kwa mtangulizi wangu Dkt. John Magufuli la kusaidia ujenzi wa nyumba ya ibada pale Chamwino,niseme tu baadhi ya maombi yanaweza kufanyiwa majibu ya haraka na mengine yanahitaji mashauri ya kina na wenzangu serikalini"amesema.

Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Geofrey Pinda amewapongeza waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Jimbo la Dodoma kwa kutimiza miaka 50 na kuongeza kwamba Mawaziri wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia wanafanya kazi vizuri na kanisa hilo na Itaendelea kushirikiana katika maeneo yote yanayowagusa kwa namna moja au nyingine.

           
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria

" Mawaziri wote tunaguswa na nyie kwasababu nyie ndiyo watanzania wenyewe ndio wananchi wa Tanzania kwahiyo Waziri wa Mambo ya Ndani atasimamia usalama kama majukumu yake yalivyo lakini pia atasimamia utaratibu wa jinsi ya uendeshaji wa shughuli za kanisa.

"lakini sisi kama Katiba na Sheria tutasimamia taratibu za uendeshaji kwa maana ya kusimamia sheria, na nipende kuwahakikishia waumini mahali popote panapoteteleka katika sheria tupo wa ajili ya kurekebisha miundo na mwenendo na taratibu ili muweze kufanya kazi zenu kwa Uhuru mkubwa na kwa amani kubwa sana ambayo mnaiona" amesema Naibu Waziri.

Naibu Waziri amesema wao kama Wizara ya Katiba na Sheria wanaendelea kususitiza kwamba nchi ya Tanzania haina mlengo wa dini na ndiyo maana hata kwenye maadhimisho hayo Rais Samia ameshiriki pamoja nao kama Watanzania na amekuwa akishiriki katika maeneo mbalimbali bila upendeleo .

Hata hivyo Rais Samia amewapongeza waasisi wa kanisa hilo katika kazi ya injili Mkoani Dodoma na Tanzania kwa ujumla, kwakuwa wamefanya kazi kubwa ya kutangaza habari njema na wokovu na kutekekeza mioyo ya Watanzania, waumini wa Kanisa hilo.

        
          Rais Samia akiwakabidhi vyeti waasisi wa kanisa hilo la Dodoma SDA


" Biblia takatifu inasema katika kitabu cha Isaya 52: 7 naomba ninukuu inasema; jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, yeye aitangazae amani aletaye habari njema ya mambo mema, yeye autangazaye wokovu, auambiaye sayuni, Mungu wako ana miliki." Rais Samia amenukuu.

Rais Samia amelishukuru kanisa hilo kwa maombi yao ambayo wamekuwa wakiyafanya kwa ajili ya serikali na Taifa kwa ujumla  nakwamba kupitia maombi ya viongozi wa dini Taifa linaendekea kudumu katika umoja, amani na mshikamano.

" Kama mnavyofahamu Taifa letu haliwezi kupiga hatua ya maendeleo pasipokuwa na amani,umoja na mshikamano, ninyi ni mashahidi wa jinsi Mataifa ya jirani wanavyoshindwa pamoja na rasilimali nyingi walizo nazo wanashindwa pamoja na rasilimali walizonazo wanashindwa kupata maendeleo kwasababu tu ya machafuko na kutotulia kwa Mataifa hayo.

Amesema watu wanatambua madhara makubwa yanayoipata dunia kutokana na vita inayopiganwa huko ulaya kwani vita inapiganwa mbali lakini madhara yake yanaenea dunia nzima.


Nukuu ya Katiba

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 19.-(1) Kila mtu anastahili kuwa na Uhuru wa mawazo, Imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.

(2)Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli za uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.

(3) Hifadhi ya haki zilizotajwa katika ibara hii itakuwa chini ya taratibu zilizowekwa na sheria ambazo ni muhimu katika jamii ya kidemokrasia kwa ajili ya usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii na umoja wa kitaifa.

(4) Kila palipotajwa "dini" katika ibara hii ifahamike kwamba maana yake ni pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengineyo yanayofanana au kuambatana na neno hilo nayo yatatafsiriwa kwa maana hiyo.






No comments