HEADER AD

HEADER AD

RC DODOMA AWAKARIBISHA WAADVENTISTA WASABATO KUTEMBELEA MIRADI YA SERIKALI


Na Dinna Maningo, Dodoma

SERIKALI Mkoani Dodoma imewakaribisha Waadventista wa Sabato kutembelea miradi ya Serikali inayotekelezwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu.

Ukaribisho huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule wakati akitoa salamu za mkoa katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Utume na Huduma ya Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kati mwa Tanzania yaliyofanyika katika makao yake makuu Jijini Dodoma, Novemba, 19,2022.

Rosemary amewakaribisha Waadventista wa Sabato kutembelea miradi ya Serikali katika mkoa wa Dodoma ukiwemo mradi wa Reli ya mwendokasi ambayo imefikia hatua zaidi ya asilimia 90, barabara ya mzunguko, ujenzi wa uwanja wa ndege ambao unaendelea kujengwa, Vituo vya Afya, Hospitali, Madarasa, miradi mikubwa ya kilimo inayoendelea pamoja ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

"Nipende kuwakaribisha Waadventista wa Sabato watembelee miradi ya serikali ambayo rais anaendelea kutekeleza kwa kasi kubwa ambayo ameitolea fedha , mtembelee muone uwanja wa ndege mkubwa wa ndege wa Msalato unaoendelea kujengwa ambao utakuwa mkubwa Tanzania utakapokamilika , mtembelee barabara ya mzunguko ambayo hamuwezi kuipata eneo lolote Tanzania," amesema  Rosemary.

Mkuu huyo wa Mkoa amewashukuru waadventista wa sabato kwa ushirikiano wanaotoa kwa serikali ya mkoa huo kwa utoaji wa huduma ikiwemo huduma ya elimu, afya na mambo mengine.

Amewashukuru kwa jinsi walivyoshirikiana na mkoa katika suala la sensa hivyo kuchangia matokeo mazuri  ya mkoa wa Dodoma kwakuwa walifanya kazi nzuri ya kuwaelimisha waumini wakawa tayali kuhesabiwa.


              Mkuuu wa Mkoa Dodoma

Rosemary amesema kanisa la Waadventista wa Sabato ni kati ya watu ambao wamekuwa wakisisitiza maadili na uzalendo kama sehemu ya mahubiri yao, wamekuwa wakiombea taifa na kumwombea Rais Samia.

"Mh. Rais niwape upendeleo wa kutosha Kanisa la Waadventista wa Sabato ni kati ya watu ambao wamekuwa wakisisitiza maadili na uzalendo, na mara nyingi tukikutana nao na hata maaskofu wamekuwa wakinituma salamu kwajo wanasema mwambie rais tupo pamoja na yeye, na nilipowaona leo nikajua leo watakuwa wamefurahi sana, salamu zote watazitoa wenyewe sio kupitia kwa mtu mwingine.

" Nitoe salamu nyingi kwa Kanisa la Waadventista wa Sabato mkoa wa Dodoma kufika miaka 50 niwatakie mafanikio mema katika kuendeleza kanisa lakini pia nchi yetu ya Tanzania hongereni sana ," amesema.

Pia amempongeza Rais Samia kwa jinsi anavyofanya kazi kubwa na nzuru ya kuiongoza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akisisitiza amani, upendo, haki na uchapakazi.

" Rais umeweza kutuunganisha watanzania na kututaka tufanye maendeleo bila kujali dini zetu, vyama vyetu vya siasa, makabila yetu na wakati wote Rais umetaka tutende haki.

"Vitabu vya dini vinasema haki italiinua Taifa, umeamua kuliinua Taifa kwa kutenda haki na nikupongeze kwa kutupa miradi mikubwa ya kimkakati ya kitaifa na miradi ya wananchi wa Dodoma" amesema Rosemary.

Akisoma Taarifa ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania  katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Utume na Huduma ya Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kati mwa Tanzania yaliyofanyika katika makao yake makuu Jijini Dodoma Nivemba, 19,2022;

Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania katika Kanisa hilo Mch. Jeremiah Izungu amempongeza Rais Samia kwa namna anavyoongoza vyena na ametaja miradi ya kanisa ya huduma za jamii.


Mch.Jeremiah amesema " Kanisa la Waadventista wa Sabato tunakupongeza kwa moyo wa dhati kwa namna ambavyo unatuongoza vyema, tumeshuhudia moyo wako wa upendo na mapenzi makubwa uliyonayo kwa watanzania katika kila nyanja.

"Kuhusu elimu, madarasa yamejengwa kwa wingi hii imewapunguzia wazazi mzigo wa kuchangia ujenzi wa madarasa, kwenye afya vituo vya afya na hospitali vimejengwa kwa wingi na tiba imeboreka kwa upatikanaji wa vifaa tiba na madawa, hususani maji kweli umewatua wakina mama ndoo kichwani.

"Katika suala la kielimu maandiko matakatifu yanasema mkamate elimu  usimwache aende zake. Mithali 4: 13, ili kutekeleza jukumu hilo kanisa limechangia kutoa huduma bora ya elimu kwa kujenga na kuanzisha shule za awali 27, shule za msingi 23, shule za Sekondari 18, Chuo cha Veta kimoja, Chuo cha kati kimoja, Chuo cha afya kimoja na Chuo kikuu kimoja" amesema Mch. Jeremiah.

Amesema kanisa limekuwa na lengo la kuimalisha afya ya Jamii, na limeendelea kutoa msisitizo katika afya ya jamii na kufundisha jamii nzima ya Tanzania kanuni za afya kwa makusudi ya kuboresha afya bora miongoni mwa watanzania. Kanuni hizo ni Lishe bora, mazoezi, unywaji wa maji ya kutosha, kujiepusha na njia au tabia zinazoweza kuudhuru mwili na kumtegemea Mungu katika maisha yao.

Ameongeza kuwa kanisa linao mpango endelevu wa kuchangia damu salama kila ifikapo machi ya kila mwaka ili kuifanya benki ya damu salama kuendelea kutoa huduma zake kwa Tanzania.

" Mpango wa afya ulianza pale kwenye bustani ya edeni mwenyezi Mungu alitoa mwongozo wa kutunza afya zetu katika ulaji wa vyakula sahihi, maelekezo hayo yanatoka Mwanzo 1:29, Mambo ya walawi 11: 1-47. Katika huduma za afya kanisa limefanikiwa kuwa na Zahanati 29, Kliniki ya Meno moja, Hospitali mbili na Poly Clinic  moja" amesema Mch.Jeremiah.

Rais Samia amepongeza kanisa hilo kwa kazi ya kutangaza injili na kuielekeza mioyo ya watanzania, waumini wa kanisa hilo kwa mwenyezi Mungu kupitia Yesu Kristo pamoja na kutoa huduma za kijamii, pia akalipongeza kanisa kwa mwaliko na mapokezi mazuri katika kushiriki maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50.

Rais Suluhu akiwa ameongozana na baadhi ya viongozi wa serikali wameshiriki maadhimisho hayo ambapo alihutubia kanisa hilo na kuzindua ujenzi wa kanisa la Dodoma pamoja na kuzindua mnara wa kumbukumbu ya Jubilee ya miaka 50 ya Utume na Huduma.








No comments