WAFUGAJI : WATAFITI NJOONI TARIME MTAFITI NYASI YA RUNYERU
Na Dinna Maningo, Tarime
NYASI za Asili ni chakula cha mifugo na imekuwa ikila ili kujenga mwili, na ni sehemu ya kudumisha utamaduni wa malisho ya kiasili, mifugo ikipata malisho ya kutosha itakuwa na maziwa yenye virutubisho na nyama yenye radha ambayo ikitumiwa na Binadamu itamjenga vyema kimwili na kibiashara.
Nyasi za asili hazijapewa kipaumbele ukilinganisha na nyasi za kisasa ambazo zimekuwa zikitiliwa mkazo ili wafugaji wazitumie kulisha mifugo yao kama njia mojawapo ya kukabiliana na ukosefu wa malisho.
Maeneo mengi hususani ya vijijini katika wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, bado hayajafikiwa na nyasi za kisasa, wafugaji wanaendelea kutembea huku na kule kusaka malisho ya asili huku wafugaji wanaofuga kisasa wakihangaika kusaka nyasi ili kulisha mifugo yao.
Kuzidi kupotea kwa nyasi za asili kunapelekea wafugaji waseme kuwa kuna haja ya watafiti kuzitafiti nyasi za asili ambazo zinaaminiwa na jamii kutokana na ubora wake kwa mifugo , vinginevyo nyasi zilizosalia nazo zitatoweka kabisa.
Watafiti waombwa kufika Tarime kutafiti nyasi za asili
Wafugaji wanawaomba watafiti mbalimbali wa malisho ya mifugo ikiwemo Taasisi ya Mifugo Tanzania TALIRI kufika Tarime kuzungumza na wafugaji ili kufahamu changamoto za malisho.
Wafugaji wanasema ikiwezekana nyasi za asili ikiwemo aina ya nyasi inayotambulika kwa jina la Kabila la Kikurya RUNYERU zifanyiwe utafiti kama zinafaa kupandwa kisha iwe ajenda kuhakikishia wafugaji wanatenga maeneo kupanda nyasi hizo ili ziwe endelevu kwakuwa ni nyasi ambazo wafugaji wanaziunga mkono katika ubora wake kwa mifugo.
Nyasi ya asili aina ya Runyeru (jina la Kikurya)
Ester Nyamhanga mkazi wa Kijiji cha Matongo anasema ," Mimi nimechunga mifugo zaidi ya miaka 30 tangu nikiwa mtoto, kuna nyasi ambazo mifugo ikila inajisikia furaha ni sawa na binadamu kuna chakula unachopenda kula ukikiona unafurahi na chakula kingine ukila ni bora liende ilimradi ushibe ila hukipendi.
"Mifugo nayo ni hivyo hivyo kuna nyasi inazipenda na zingine haizipendi zitakula ilimradi siku iende zishibe lakini sio chakula bora kwao, nyasi za runyeru ni nzuri inapendwa na mifugo huota sehemu kavu zenye mwinuko kama mlimani haipendelei kuota sehemu yenye maji , kwakuwa maeneo hayo yanaingiliwa na shughuli za kibinadamu hali inayochangia nyasi za runyeru kutoweka.
"Mifugo kama Ng'ombe wanapenda sana nyasi za runyeru lakini upatikanaji wake ni wa kubahatisha, maeneo kulikokuwa zimeota watu wanayatumia kwa kilimo, na eneo lingine Mgodi wa North Mara ulichukua.
" Nyasi za runyeru zimebaki kidogo zipo Masangora, Kerende na Murito nako ni kidogo ili uzipate kwa wingi labda ufunge safari kwenda wilaya ya Serengeti kule utazipata,"anasema Ester.
Joseph Muhere mkazi wa mtaa wa Kokehogoma anasema " Watanzania tupende vitu vya kwetu na tuvifanyie tafiti na tuviendeleze , tuna aina nyingi za nyasi za asili hapa nchini ambazo zinatumika kwa malisho vizazi hadi vizazi mpaka sasa.
" Lakini hazijafanyiwa utafiti ili kuthibitisha ubora wake badala yake tunanunua nyasi za kigeni kutoka nje ambazo huwenda zilitoka huku nchini wazungu wakaenda kuziboresha kwao wakazirejesha kisasa na kutuuzia.
"Nyasi ya Runyeru ni nyasi ambazo kila mfugaji anazijua uzuri wake ni nyasi ambazo mifugo ikila inanenepa inakuwa na maziwa mengi lakini sijui kama zilishafanyiwa utafiti.
" Tunaomba watafiti waje wazitafiti maana zinazidi kupotea wakati miaka iliyopita zilistawi sana ni chakula bora kwa mifugo, waje watupatie utalaamu wao namna gani ziendelezwe mifugo ifurahie chakula cha Runyeru," anasema Joseph.
Ester John mkazi wa Rebu Senta anasema Nyasi za asili zifanyiwe utafuti kwakuwa ndizo zinazopatikana maeneo ya vijijini vinginevyo zitatoweka kabisa ," Nyasi za asili zifanyiwe tafiti ,huwa tunasikia kuna nyasi za kisasa lakini hatujawahi kuziona ni vyema nazo zikasambazwa kama wanavyosambaza pembejeo za kilimo ili ziwafikie wafugaji wanunue ziuzwe kwa bei nafuu mifugo ipate chakula"anasema .
Wapanda Nyasi za kisasa kunusuru Mifugo
Kukosekana kwa nyasi za asili baadhi ya wafugaji wenye mifugo michache wameamua kupanda nyasi za kisasa aina ya Mabingobingo na zingine hawazifahamu kwa jina halisi zaidi yakuziita nyasi za kisasa zimepandwa katika maeneo yao kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Hata hivyo nyasi hizo za kisasa bado hazijawafikia wafugaji wengi kwenye vijiji na mitaa mbalimbali wilayani Tarime, zinapatikana kwa uchache katika baadhi ya Kata ikiwemo Kata ya Ganyange ,Nyanungu na Kata ya Binagi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyandage Mwita Kiha anasema kuwepo migogoro ya wafugaji na maafisa wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti baadhi ya wafugaji wakalazimika kupanda nyasi za kisasa aina ya Mabingobingo ili kulisha mifugo yao.
Mabingobingo
Anasema bado nyasi za kisasa hazitoshelezi mahitaji kutokana na wafugaji wengine kuwa na mifugo mingi na hivyo kulazimika kwenda kuchunga kwenye maeneo yenye nyasi za asili ambapo huingia mgogoro na hifadhi pamoja na wakulima pindi mifugo ichungapo kwenye maeneo hayo.
" Vijiji nane vimepakana na hifadhi ya Serengeti vinakabiliwa na ukosefu wa malisho kwasababu eneo kubwa lenye malisho ya asili lipo ndani ya hifadhi, wapo wachache waliopanda nyasi za kisasa aina ya Rusyagha (Mabingobingo) hata mimi nimepanda tuliomba kwa watu waliopanda ni nzuri lakini hazitoshelezi mahitaji ya mifugo.
" Kuna Nyasi za asili ambazo ni nzuri kwa mifugo ni vyema serikali kupitia wataalamu wake wakaja kuzitafiti ikiwezekana zizalishwe kwa wingi tuzipande maana zenyewe zinajiotea hukuhuku kwenye mazingira yetu ni rahisi kuzipata ,tusipozifuatilia zitapotea na hazitpatikana tena na hapo tutakuwa tumeathiri mifugo kwa kuikosesha nyasi za asili ambazo zilikuwa chakula chao bora, " anasema Mwita.
Mwita Chacha mkazi Rebu anasema serikali imekuwa ikiwashauri wafugaji kufuga mifugo michache kutokana na uhaba wa malisho na maeneo machache ya kufugia, lakini pamoja na kufuga mifugo michache wanakabiliwa na ukosefu wa nyasi za kulisha mifugo.
" Ufugaji wa mifugo michache ni mzuri ukilinganisha na ufugaji wa ng'ombe wengi hasa kwa sisi tunaoishi mitaa ya mjini lakini bado tunapata shida ya nyasi tunazunguka sana kutafuta nyasi, kinachotusaidia ikifika jumapili ni siku ya mnada tunaenda sokoni kuokotaokota ile mikungu tupu ya ndizi mbichi tunaikatakata na kulisha mifugo, malisho ya kununua yana gharama sana," anasema Mwita.
Maswi Mosama ni mkazi wa kijiji cha Borega A kata ya Ganyange anasema wafugaji wenye mifugo michache ndio wanaweza kutumia nyasi za kisasa kwakuwa huoteshwa eneo dogo ambalo halikidhi mahitaji ya mifugo mingi.
Nyasi za kisasa zilizopandwa Kijiji cha Borega A
"Mimi nina Ng'ombe watano nilipanda nyasi za kisasa zile laini ambazo niliwezeshwa na kampuni ya gederi iliyokuwa inakopesha Ng'ombe,unapewa ng'ombe jike ikizaa watoto watatu wanachukua ndama watatu alafu wanakuachia ng'ombe inakua mali yako.
"Na sharti lao ili wakupe Ng'ombe mpaka uwe umepanda nyasi za kisasa na umetengeneza banda ukiwa navyo mnaingia mkataba wanakupa nyasi unapanda kisha wanakupa ng'ombe, kiasi fulani ilisaidia wafugaji wakapanda nyasi, ukizunguka baadhi ya mashamba utakuta nyasi za kisasa" anasema Maswi.
Sylvanus Gwiboha ni mfugaji wa Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo mkazi wa Mtaa wa Kohehogoma mjini Tarime anayefuga kisasa, anasema uhaba wa malisho unatokana na mabadiliko ya hali ya hewa, kuchelewa kwa mvua au kunyesha pasipo uhakika kunaathiri uotaji wa nyasi.
Sylvanus anasema mwingiliano wa mifugo katika maeneo ya kuvuna nyasi ni tatizo " Hii ni kwa wanaochunga kuchungia katika maeneo yaliyopandwa nyasi kwa ajili ya mifugo wa ndani, usipoweka mlinzi unakuta wameingiza ng'ombe zao wanaharibu nyasi, inaongeza gharama za ufugaji na jambo hili huzua mgogoro wa wafugaji kwa wafugaji " anasema Sylvanus.
Anasema baadhi ya nyasi za asili hupatikana mabondeni lakini kwasasa baada ya mvua kupungua mabonde mengi yamelimwa mazao hivyo kuathiri malisho ya mifugo na kwamba wakati mwingi mwezi wa kumi kila mwaka wafugaji wanalazimika kulisha mifugo majani ya viazi (Malando ) tokana na msimu wa mavuno.
Mfugaji huyo anasema baadhi ya watu wanauza nyasi zilizoota mabondeni wakisema ni maeneo yao hivyo wafugaji kulazimika kulipa Tsh. 5,000 hadi Tsh10,000 kwa ujazo wa bajaji moja na bado hulipa usafiri Tsh 8,000 hadi Tsh10,000 kulingana na umbali ambapo mifugo inayofugwa ndani ambayo yenyewe haiendi kutafuta malisho nje bali inaandaliwa malisho ikiwa nyumbani mifugo hiyo inahitaji bajaji 2 hadi 3 za nyasi kwa siku.
" Tunatafuta malisho mbali sana na mji ambapo gharama za usafiiri kwa tripu moja ya bajaji inafika Tsh.15,000, Gharama hizi zimechangia kuongeza gharama za uzalishaji wa maziwa hata kupelekea kuuza maziwa Lita moja Tsh 1,300.
"Japo bado ni kidogo kukidhi gharama kwani msimu huu debe moja la pumba limepanda kutoka Tsh 4,000 hadi Tsh 7,500 na wakati mwingine hazipatikani kwani wastani wa bei ya kilo 18 za mahindi imefikia Tsh 22,000, chakula bora kilichochanganywa kitalamu kilo 70 inauzwa Tsh Tsh 55,000 hadi Tsh 60,000 ambacho kinatumika kwa siku 7 kwa mtu mwenye ng'ombe watano" anasema Sylvanus.
Anaongeza " Gharama ni kubwa inatulazimu kubana matumizi mfano ng'ombe anayekamuliwa lazima umpe chakula hicho ili aendelee kukupa maziwa vizuri na hapo nimepiga hesabu ya chini kilo 2 kwa siku "anasema.
Anatoa wito kwa wafugaji wote wa ndani na nje kupata maeneo ya kumiliki na kupanda nyasi za kutosha ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwani kwa mujibu wa taarifa ya hali ya hewa iliyotolewa kupitia vyombo vya habari tarehe 27, Oktoba, 2022 inaonesha mvua zitanyesha kwa mgawanyiko na chini ya wastani hivyo kuathiri mazao na malisho.
Anasema jambo lingine ni kuvuna na kutunza malisho ya kutosha ndani ili kusaidia msimu ambao nyasi zitapungua au hazitakuwepo, lakini pia Wataalam wa mifugo wasaidie elimu ya kutengeneza malisho kitaalamu vinginevyo mifugo ya wafugaji itakufa kama ilivyokufa ya wenzao huko afrika ya kati.
Pia wafugaji wauze mifugo ili iendane na eneo la malisho (livestock carrying capacity) itasaidia kutopata hasara za mifugo kufa kwani itatunzwa kwa mujibu wa kitaalamu. Anatoa wito kwa wataalamu wa mifugo wajitokeze waelimishe wafugaji mbinu bora za uzalishaji wa nyasi nyingi kwa eneo dogo lililopo (Hydroponics).
Kwa mujibu wa Kitini kilichoandaliwa na Idara ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kinaeleza kuwa Malisho ni chakula cha msingi cha mifugo kinachojumlisha aina mbalimbali za nyasi na mikunde.
Inaelezwa kuwa utunzaji wa malisho ni muhimu ili kuhakikisha kwamba mifugo inapata chakula bora na cha kutosha wakati wote . Ukuaji na ustawi wa aina za malisho hutofautiana kutegemea hali ya hewa na mazingira mbalimbali.
Kitini hicho kinaeleza faida ya kupanda malisho, hurahisisha upatikanaji wa chakula cha mifugo chenye viini - lishe Kama wanga, protini, Madini na vitamini ,hurutubisha ardhi hasa malisho aina ya mikunde. Huzuia mmomonyoko wa ardhi. Miti malisho kama lukina,Sesbania na Grilicidia hutumika kama kuni na Kinga ya upepo.
Idara hiyo ya malisho inataja baadhi ya aina za nyasi za kupandwa zilizofanyiwa utafiti wa kitaalamu ni Guatemala ( Tripscum Laxum) ambayo hustawi zaidi kwenye eneo lenye mvua ya wastani , Mabingobingo/ Bana grass ambayo hustahimili ukame, Guinea grass malisho hustawi katika aina mbalimbali za udongo na kuvumilia ukame na joto.
Zingine ni Rhodes grass hustawi katika maeneo yanayopata mvua za wastani hadi nyingi ambapo nyasi Jamii ya mikunde ni Desmodium ambayo hustawi vizuri, huvumilia ukame kiasi na huchipua haraka baada ya kukatwa pamoja na Miti ya Lukina ( Leuceana leucocephala) ambayo hupandwa kwa kutumia mbegu moja kwa moja shambani au kwenye vitalu na Miche kuhamishwa shambani.
Post a Comment