HEADER AD

HEADER AD

TSC TARIME YAWAFUKUZA KAZI WALIMU WANNE WENGINE WAPEWA ONYO


Na Dinna Maningo, Tarime

TUME ya Utumishi wa Walimu ( TSC ) wilaya ya Tarime mkoa wa Mara imewafukuza kazi walimu wanne kwa makosa ya utoro na kughushi vyeti huku wengine watano wakipewa onyo kali.

Akizungumza na DIMA Online ofisi ya TSC, Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu wilaya ya Tarime Agutu Christopher amesema Tume hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imepokea mashauri 10 ya nidhamu ya walimu.

Amesema  kati ya mashauri hayo, manne yalitolewa maamuzi ambapo walimu wanne wamefukuzwa kazi kwa makosa ya utoro kazini na kughushi vyeti ambao ni Tabani Daniel aliyekuwa mwalimu katika shule ya msingi Kenyamanyori katika Halmashauri ya Mji Tarime.

Amesema Tabani amefukuzwa kazi kwa utoro kazini tangu Mei, 5,2018 hadi Agasti, 30, 2021 shauri lake lilipowasilishwa TSC Agasti, 30, 2021.

Wengine ni Editha Lusumbo aliyekuwa mwalimu shule ya msingi Buguti katika Halmashauri ya Mji Tarime kwa kosa la utoro kazini tangu Juni, 26, 2020 hadi Agasti, 30, 2021 shauri lake lilipofikishwa katika Tume hiyo Agosti, 30, 2021.

Amesema waliofukuzwa kazi kwa kughushi vyeti ni Magdalena Mwanyika aliyekuwa mwalimu wa shule ya msingi Tumaini shauri lake liliwasilishwa Desemba,1, 2021 pamoja na Mary Mniko aliyekuwa mwalimu wa shule ya msingi Bisarwi katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime shauri lake liliwasilishwa Septemba, 8, 2022.

Waliopewa onyo kwa kosa la utoro kazini ni Mwalimu Phinias Malingumu wa shule ya msingi Kemakorere na Mwalimu Nyamanche Kulwa wa shule ya msingi Kikomori.

Amesema walimu wengine watano mashuri yao ya utoro kazini yanaendelea kusikilizwa ambao ni Dorin Mushi wa shule ya msingi Mangucha, Meremo Boniface Marwa wa shule ya Sekondari Kibasuka , Zephania Magesa wa shule ya msingi Mturu, Juma Makuri shule ya msingi Buguti na Musa Nzugilwa wa shule ya Sekondari Muriba.

Ameongeza kuwa kesi moja ya Victoria Jonasi aliyekuwa mkuu wa shule ya Sekondari Manga inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya wilaya ya Tarime akikabiliwa na shauri la Rushwa na Uhujumu Uchumi.

        Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu wilaya ya Tarime Agutu Christopher

"Tunawataka walimu wafanye kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili ya walimu na miiko ya kazi, tume ya utumishi inashughulika na huduma za utumishi wa walimu, kusajili walimu wanaoajiriwa, kupandisha madaraja , kushughulika na masuala ya kinidhamu kwa walimu na kustaafisha walimu.

" Vilevile tunafanya kazi ya kuwafikia walimu ngazi ya kata tunawaelimisha kuhusu sheria na kanuni za utumishi wa walimu pamoja na kutunza thamani waliyopewa na serikali kwa ajili ya kuelimisha umma wa Tanzania" amesema Agutu.

Akizungumzia upandishwaji wa madaraja kwa walimu amesema jumla ya walimu 102 wamepandishwa madaraja kati ya hao 59 ni kutoka Halmashauri ya wilaya ya Tarime na 43 Halmashauri ya Mji Tarime.

 


No comments