HEADER AD

HEADER AD

BODI YARIDHISHWA UJENZI KITUO CHA KUDHIBITI WANYAMA WAKALI, WAHARIBIFU


Na Annastazia Paul, Simiyu

BODI ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeeleza kuridhishwa na ujenzi wa kituo cha kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.

Ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. Samia Suluhu la ujenzi wa vituo 16 vya kudhibiti wanyama hao wanaovamia makazi ya wananchi wanaopakana na hifadhi za taifa na mapori ya akiba nchini na kusababisha uharibifu.

Akizungumza wakati wa kukagua ujenzi wa kituo hicho cha kudhibiti wanyama wakali na waharibifu kilichopo katika pori la akiba Kijereshi, lililopo wilayani Busega mkoani Simiyu, Mwenyekiti wa bodi hiyo Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko amesema kazi ya bodi hiyo ni kuhakikisha mgogoro baina ya wanyama na binadamu unashughulikiwa ipasavyo.

     Kituo cha askari wa wanyamapori kilichopo katika pori la akiba Kijereshi ambacho kimejengwa kwa ajili ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.

"Kazi ya bodi yetu ni kuhakikisha kwamba mgogoro kati ya binadamu na wanyama unashughulikiwa ipasavyo na ndiyo maana tumeweza kutenga fedha  kuweza kuhakikisha kwamba kinajengwa kituo hiki.

"Sio hili tu tutatumia mbinu nyingine, njia nyingine za kitaalam kuhakikisha kwamba jengo hili lililojengwa hapa linakuwa ni chanzo cha udhibiti na hakutatokea mgogoro tena". Amesema Semfuko.

Profesa Suzana Augustino ni mjumbe wa bodi hiyo ambaye amesema tatizo la wanyama kuvamia maeneo ya makazi ya binadamu na kusababisha madhara limekuwa la muda mrefu na kujengwa kwa vituo vya askari katika hifadhi kutasaidia kudhibitiwa kwa wanyama hao.


"Tafiti nyingi zimefanyika kutafuta suluhu, lakini yawezekana sasa ujenzi wa vituo hivi vya kudhibiti wanyama waharibifu kwa mamlaka Kama TAWA kwa kushirikiana na wananchi itatusaidia." Amesema profesa Augustino.

Mhandisi Simon Chillery ambaye ni Naibu Kamishna wa Polisi ameiomba menejimenti ya TAWA kuhakikisha askari katika vituo hivyo wanakuwepo wa kutosha.

"Naiomba sana menejimenti ya TAWA kuhakikisha kwamba askari wanakuwepo wa kutosha, wanapewa maelekezo sahihi kuhakikisha kwamba kile ambacho tunakitarajia kinafanyika kwa ufanisi mkubwa." Amesema Chillery

Diwani wa Kata ya Lamadi Bija Lawrent amesema wanyama wamekuwa wakiharibu mazao shambani na hata kusababisha madhara kwa binadamu.

"Lengo ni kuhakikisha kwamba mazao yanakuwa salama ina maana tunapolima tuwe na uhakika wa kupata chakula lakini usalama pia kwa wananchi kwasababu tembo wanavamia na kung'oa nyumba za watu." Amesema Lawrent.








No comments