UWT BUNDA WAOMBA ELIMU YA UONGOZI IWE ENDELEVU
Na Jovina Massano, Bunda
WENYEVITI na Makatibu wa Kata pamoja na Matawi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Bunda Mkoani Mara, wamesema elimu endelevu ya uongozi inahitajika kwa viongozi ili kuleta uwajibika katika Chama, Jamii na Familia.
Wakiongea na Mwandishi wa DIMA OLINE wakati wa mafunzo kwa viongozi wa UWT Wilayani Bunda yaliyofanyika hivi karibuni Desemba, 20, 2022, Mwenyekiti wa UWT Tawi la Nyasura Teodora Laurent amesema mafunzo ya uongozi yaliyotolewa na Chama yamewasaidia kujua mipaka na majukumu katika ngazi ya uongozi waliyonayo.
"Tunaomba mafunzo haya yawe endelevu kwani yametujenga sana katika kujua majukumu yetu kama viongozi na uwajibikaji kwenye nafasi tulizonazo lakini pia yametupatia uelewa mpana kiuongozi.
"Kwa upande wangu hii ni mara yangu ya kwanza kupata elimu hii tunamshukuru sana Mwenyekiti wa UWT Wilaya Marysiana Sabuni kwa kuweza kulisimamia hili",amesema Teodora.
Ameongeza kuwa amefahamu wajibu, majukumu na sifa za kiongozi na namna ya kujitoa kuhakikisha UWT inapata manufaa lakini pia mbinu za uongozi ikiwemo kujielimisha, kujitolea na kushirikiana ndani ya UWT na Chama kwa ujumla.
Katibu wa UWT Tawi la Maliasili Kata ya Nyamakokoto, Anna Hussein amewapongeza wakufunzi kwa kuweza kufundisha kwa utashi wa hali ya juu na kusaidia waelimishwaji kuelewa bila tatizo na kwamba asilimia kubwa ni mara ya yao ya kwanza kupata elimu ya uongozi hadi ngazi ya familia.
"Mimi binafsi nilichaguliwa lakini nilikuwa sielewi nianzie wapi niishie wapi na hata namna ya kuwashirikisha wenzangu katika kazi, mafunzo haya yamenijenga na kuninufaisha katika uongozi wangu, jamii inayonizunguka na kwa familia yangu ",amesema Anna.
Mkufunzi wa mafunzo hayo Fyeka Sumera amesema elimu waliyoipata itawasaidia viongozi hao kufanya kazi za Chama kwa ufanisi mkubwa.
Amesema pia ni utekelezaji wa maagizo ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu kwamba Jumuia zote na chama zitoe mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wapya na wa zamani.
"Niwapongeze viongozi wa UWT wilaya, CCM wilaya pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Bara wa Chama Cha Mapinduzi Joyce Ryoba Mang'o kwa kuwezesha mafunzo haya kufanyika, matarajio yangu ni utekelezaji wa majukumu ya Chama kwa kiwango cha juu kwa viongozi hawa",amesema Fyeka.
Hata hivyo mkufunzi wa somo la uongozi, uwajibikaji na majukumu Michael Nkoba, amewapongeza waelimishwaji kwa kuhudhulia kwa wingi lakini pia kuwa tayari kufundishika na kuwa na utulivu wa hali ya juu.
"Tumeweza kuwaelimisha juu ya majukumu yao na kuonesha mpango kazi wa UWT katika maeneo wanayoyaongoza na tumewaonesha malengo ya UWT ya Chama cha Mapinduzi, kanuni ya mwaka 2022 toleo la mwaka 2022. Matumaini yetu ni kuona viongozi wanaenda kutekeleza kwa vitendo", amesema Michael.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)Bara, Joyce Mang'o amewaomba viongozi hao kuhakikisha wanafika kwenye maeneo yao hadi ngazi za chini kutoa elimu waliyoipata ili iweze kuwa chachu ya ongezeko la wanachama wapya.
"Mafunzo haya yakaongeze kasi ya wanachama wapya na mhakikishe mnahamasisha pia wanachama waliopo na wapya kujisajili katika Mfumo wa kidigital katika maeneo yenu", alisema Joyce.
Post a Comment