HEADER AD

HEADER AD

MARWA MGENI : NAPENDA KUVAA SARE YA CCM NIKIWA KIBARUANI


  >>> Ni kuhusu ile Video Clip iliyosambaa mitandaoni

Na Dinna Maningo, Tarime

HIVI karibuni ilionekana Video Clip katika Mitandao ya Kijamii ikimuonesha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mwl.Chacha Cheche ambaye ni Mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akimwambia avue Tisheti mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Marwa Mgeni maarufu (mponda kokoto).

Tisheti hiyo wengine huita fulana aliyokuwa ameivaa Marwa, ilikuwa ya rangi ya njano yenye nembo ya kijani ambayo ni sare ya Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa amevaa suruali ya rangi ya kaki, kichwani akiwa amevaa kofia nyeupe.

Marwa alivua Tisheti yake na kuendelea na kazi. Katika Video hiyo kulikuwa na watu wengine wakifanya kazi ya kupiga kokoto, kila mtu akiwa amevaa mavazi yake ambayo hayakuwa sare za kazi, kati ya watu hao mmoja alionekana akiwa amevaa kofia yenye rangi zinazofanana na rangi zilizopo kwenye Nembo ya CHADEMA.

Chacha alisikika akisema,"Mzee yaani mimi ninakulipa alafu unakuja na nguo ya Chama cha Mapinduzi hapa! yaani unakuja kututukana, haya weka kwenye mfuko, wewe ni wa Chama cha Mapinduzi? yaan hapa kama unataka ukae vizuri jiunge na ya Peoples basi (alacha kutuchafura mura) anakuja kutuchafua!.

"Mseti yeye huwa haeleweki ni popo lakini huyu asije na nguo ya Chama cha Mapinduzi hapa hata ukikamatwa sitakusaidia ....kwanza ni dekio unavaaje hiyo? sema nikupe Tisheti bwana, Chama cha tozo mura watu sasa hivi hata karambirambi sh.10,000 unatumia ndugu yako kijijini wanakula au wewe hujawahi kuliwa hizo hela?,nyie hamliwi?.

Baadhi ya watu katika Video hiyo walionekana kupinga kauli ya Chacha na wegine wakionekana kumuunga .

Katika Video hiyo alionekana mtu mmoja aliyevaa nguo shati nyeupe na suruali nyeupe akimtete Marwa ambaye alitambulika kwa jina la Mseti Heche mdogo wake Chacha Heche ambaye alisikika akimtetea kwa kusema;

" Mwache mzee bwana, mzee wewe fanya kazi.....si ni chama chake kama ni Chama chake ana uhuru.....basi mpe nguo ya CHADEMA Sasa " ilisikika sauti ikisema.

Video hiyo ikakiibua Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya Taifa ambapo Novemba,29,2022 kupitia Katibu Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu akatoa taarifa kwa umma kikilaani vikali kitendo hicho kilichofanywa na Mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Shaka Hamdu

CCM imesema kitendo hicho ni cha udhalilishaji na utwezaji wa haki ya msingi ya mtanzania kuamini katika imani ya chama chake bila kuingiliwa, na ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 3 (1) na ibara ya 20 (1) na Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa na marekebisho yake 2018.

Pia Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Tarime kikizungumza na Waandishi wa Habari kupitia Katibu wa Chama hicho Varentine Maganga, kimemuelekeza Mkuu wa Wilaya hiyo kuchukua hatua huku kikiwataka Viongozi wa CHADEMA na Chacha Heche wajitokeze kuomba msamaha kwa Watanzania na kwa Marwa Mgeni kwa kitendo kilichofanyika kupitia Video Clip.

                    Varentine Maganga

Chama hicho ngazi ya wilaya kimeahidi kutafuta namna nzuri ya kumwezesha Marwa Mgeni na kumfanya awe mfanyabiashara kwa kumpatia mtaji afenye biashara ya ujasiliamali na kuachana na kazi ya kuponda kokoto ambapo kimempatia fedha laki mbili ili kujikimu kwa muda huo kikitafuta namna ya kumwezesha.

Chama hicho kimeonesha kusikitishwa kwa video hiyo huku kikiwashagaa Viongozi wa CHADEMA ngazi ya Wilaya , Mkoa na Taifa kutojitokeza kukemea na hivyo kukiomba kiombe msamaha kwa Watanzania, Chama cha CCM na kimuombe msamaha Marwa Mgeni.

Chama hicho kinamtaka Chacha Heche ajitokeze kuomba msamaha na akiombe radhi Chama cha CHADEMA kwakuwa amekidhalilisha na wasipofanya hivyo watajua ndiyo mafunzo wanayowafundisha wanachama wao kufanya hivyo.

DIMA ONLINE imefika Nyumbani kwa Marwa Mgeni mtaa wa Rebu Sokoni mjini Tarime na kufanya mahojiano nae kupata undani wake, ambapo ilijitambulisha na kumuuliza maswali kadhaa kuhusu  video clip naye alikuwa na haya ya kusema;

Marwa Mgeni akiwa nje ya nyumba yake

Mwandishi: Shikamoo!hujambo?

Marwa Mgeni: Marahaba, sijambo.....

Mwandishi: Ile Video iliyosambaa ikionesha unavua sare ya CCM umefanikiwa kuiona?

Marwa Mgeni: Ndiyo nimeiona kwa watu hata wewe kama unayo nioneshe tena niione maana mimi sina simu ya tachi.

Mwandishi: Je hii Video ni ya kweli?

Marwa Mgeni: Ndiyo ni yakweli kabisa. 

Mwandishi : Tukio lilitokea lini ?

Marwa Mgeni: Lilitokea tarehe 27, Novemba, 2022 tukiwa mtaa wa mafarasini nikiponda kokoto kwenye mji wa familia ya Heche. 

Mwandishi: Ulikuwa unamfanyia nani kazi?.

Marwa Mgeni: Nilikuwa namfanyia Mseti ambaye ni mdogo wake na Chacha Heche, walifika wakakuta tunafanya kazi Chacha akaniamuru nivue Tisheti ya CCM niliyokuwa nimeivaa kama ulivyoona kwenye video na mimi nikavua.

Mwandishi: Sasa wewe kwanini ulikubali kuvua nguo yako ya Chama si ungekataa?.

Marwa Mgeni: Nilivua maana nilipata hofu alikuwa mkali niliogopa na ndiyo maana sikumjibu chochote, nikavua na kuendelea na kazi.

Mwandishi? Ni mara yako ya ngapi kwenda kufanya kazi katika familia ya Heche?

Marwa Mgeni: Mara nyingi sana hata nyingine nilishamfanyia dada yake, Chacha na Mseti.

Mwandishi : Ni mara yako ya ngapi kwenda kufanya kazi kwenye familia ya Heche ukiwa umevaa nguo ambayo ni Sare ya CCM?

Marwa Mgeni: Mara nyingi tu huwa navaa sema haijawahi kutokea Chacha kunikuta nikiwa nimevaa sare ya Chama, siku hiyo ndiyo alikuja tulipokuwa tunafanya kazi ya Mseti ambapo ni jirani na nyumbani kwake alinikuta ndio kuniamrisha nivue.

Mwandishi: Kwanini unavaa Sare ya Chama wakati unajua mahali unakofanyia kibarua bosi wako mmoja ni mwanachadema na hata aliwahi kuwa Katibu wa CHADEMA mkoa wa Mara, huoni wewe ndio sababu ya yeye kukuamuru uvue nguo ya CCM kwakuwa yeye si mwanaccm?.

Marwa Mgeni: Mimi napenda kuvaa vazi la CCM sio mara ya kwanza kuvaa sare ya CCM nilishazoea, na sikujua itamkwaza kwasababu ni nguo tu haihusiani na kazi.

Mwandishi :Baada ya Video Clip kusambaa mitandaoni CCM imekuita kuzungumza na wewe? kama wamekuita wamekueleza nini ?.

Marwa Mgeni:Nilipofika waliniuliza mzee unafanya kazi gani? nikawaambia yakupiga kokoto,wakaniambia usiende tena kupiga kokoto, wakasema watanitafutia mtaji wakanipa pesa ya kujikimu kwa siku chache wakati huo wananitafutia mtaji, na wamesema Chacha Heche aniombe samahani na aiombe CCM samahani.

Mwandishi: Wamekupa shilingi ngapi?

Marwa Mgeni: Hiyo siwezi kukuambia maana sikujui vizuri ila nimeambiwa nipumzike nisifanye tena kazi ya kokoto na nilipoenda ofisini wamenipa Tisheti mpya hii niliyovaa na kiasi cha fedha.

Mwandishi:Kazi ya kuponda Kokoto umeianza mwaka gani?.

Marwa Mgeni: Nimeianza tangu mwaka 2007, mimi ni mzaliwa wa Nyarutu -Soroneta kata ya Binagi, hapa mjini nimekuja kutafuta maisha.

Mwandishi: Mbali na kuponda kokoto unajishughulisha na kazi gani nyingine?.

Marwa Mgeni: Najishughulisha na ufugaji wa nguruwe ninao 27, mtu akitaka namuuzia, bei ni kati ya elfu hamsini hadi Milioni moja na nusu itegemea na ukubwa wa nguruwe.

Mwandishi :Je umeoa na una watoto?

Marwa Mgeni: Ndiyo nimeoa na nina watoto 10 kati ya hao wasichana ni wawili na wavulana wanane na nina wakamwana na wajukuu.

Mwandishi: Ukipewa mtaji utafanya biashara gani?.

Marwa Mgeni: Nikipewa mtaji nitafanya biashara ya ndizi mbichi na kuachana kabisa na kazi ya kuponda kokoto.

Je Mseti Heche, Chacha Heche, Uongozi wa CHADEMA na Wananchi wanasemaje kuhusu Video Clip hiyo ?.

Endelea kufuatilia DIMA Online.

No comments