CHACHA HECHE : VIDEO CLIP HAIJAMDHALILISHA, HAKUPIGWA,HAKUNYIMWA KAZI
Na Dinna Maningo, Tarime
DIMA ONLINE imezungumza na Mseti Heche aliyeonekana katika Video Clip akiwa na kaka yake Mwl.Chacha Heche, mponda kokoto aitwae Marwa Mgeni akiwa na vibarua wenzake waliokuwa wakifanya kazi ya kuponda kokoto katika familia ya Heche.
Video hiyo ilisambaa katika Mitandao ya Kijamii ikimuonesha Chacha Heche akimwambia Marwa Mgeni avue tisheti ya rangi ya njano yenye nembo ya kijani ambayo ni sare ya Chama cha Mapinduzi (CCM), na yeye akatekeleza na kuvua vazi hilo.
Video hiyo ikakiibua Chama cha Mapinduzi ngazi ya Taifa na Wilaya ya Tarime wakilaani vikali kitendo hicho kilichofanywa na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Alichokisema Mseti Heche
Katika Video Clip, Mseti Heche alionekana kupinga kauli ya ndugu yake Chacha yakumtaka Marwa avue sare ya Chama , alipotakiwa kueleza kama yeye ndiye aliyempa kazi Marwa au Chache Heche amesema;
"Dada mimi siyo mwanasiasa ni vyema ukamtafuta Chacha mwenyewe ukazungumza nae mimi nilizuia amuache nikasema aendelee na kazi naomba umtafute Chacha mimi sijui chochote" amesema Mseti.
Chacha Heche azungumza
DIMA ONLINE imefanya mahojiano na Chacha Heche kufahamu sababu za kumtaka Marwa kuvua Sare licha ya kwamba walikuwa kwenye eneo la kazi eneo binafsi ambalo mtu yeyote ana haki ya kuvaa vazi lolote alipendalo ikiwa mwajiri hajatoa sare rasmi zinazotakiwa kuvaliwa kazini.
Mwandishi: Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha wewe unamwamrisha Marwa Mgeni kuvua sare ya CCM na akavua kitendo ambacho Chama cha Mapinduzi kimesema ulimdhalilisha mwanachama wao na kumbagua kwa Itikadi ya vyama, je wewe unalizungumziaje hilo?.
Chacha Heche: Yote hayo nitayazungumza maana kwanza hakuna clip ya dakika 3 inayoweza kuitwa ubaguzi, ubaguzi huwa ni tukio endelevu.
Kazi ya kokoto nimeifanya na huyo mzee kwa muda mrefu na hakuwa na hayo mavazi , naona nguo ni kichocheo.
Mwandishi: Kitendo cha kumwambia avue sare ya Chama chake huoni huo ni ubaguzi na udhalilishaji ?.
Chacha Heche:Hakuna udhalilishaji pale kwasababu hakuna aliyepigwa, kutusiwa wala kunyimwa kazi, ni muhimu ijulikane kuwa kuelekeza namna ya kuvaa sio unyanyasaji.
Mwandishi: Kitendo cha kumwambia avue nguo na akatii kuivua na kubaki na kaushi ya ndani huo sio udhalilishaji ?.
Chacha Heche: Kokoto huwa wanapiga wakiwa wamevaa vikaushi wote na mimi nilishawanunulia vifaa kwa fedha zangu ili kupunguza hata kuumia, nilitoa fedha za miwani, gloves na kaushi, kwanini asivae hizo atupe avae za CCM ni matusi, hapo naona huyu alipangwa kuchokonoa sio bure na wakachukua clip.
Mwandishi: Kumwambia avue sare si ni kumbagua kwa sababu tu ya sare?
Chacha Heche: Ukiambiwa uvae sare za kazi utakuwa umebaguliwa? kama mtu anakufahamu kwa muda wote kuwa wewe ni CCM na anaendelea kufanya kazi na wewe hakutaka kukubagua inakuwaje leo kumtaka uvue vazi la CCM iwe ubaguzi!
Chacha Cheche: Mimi kuanzia wewe mpaka hao wanaccm wanajua utu wangu na nisivyohangaishwa na siasa, nyuma ya pazia......kejeli kwa wanaccm wengine ukabila yalisababisha nibadili utaratibu tangu awali, mzee akaona haitoshi akaenda kupewa nguo mpya akaja nayo.
Mwl. Chacha Heche
Mwandishi: Lakini ile haikuwa sare ya kazi na kila mtu alivaa nguo yake anayoipenda maana hawakuwa na mavazi rasmi ya kazi ambayo yalipaswa kuvaliwa.
Chacha Heche: Kelele zilizokuwa zinatawala pale tagu awali na huwa natembelea kule niliona nizizime kwa kuwapa fedha wote wanunue matisheti civilian yule akaenda kuongeza tisheti mpya ya CCM na mimi nimemlipa kununua nguo inayomfaa isiyo na ushabiki afanye kazi yake bila bughudha.
Mwandishi:Wewe ni Mwadventista Msabato unatakiwa kuwapenda hata wavaa sare za CCM maana Wasabato wapo wa vyama vyote.
Chacha Heche: Kuwapenda ni kuwasaidia na hilo wanajua nafanya kwa kiwango gani. Afanye kazi alipwe kipato chake aende kwake ameshiba asibaguliwe kwa chakula wala asifukuzwe nadhani hilo ndilo lengo kuu ila kufuata utaratibu kwamba hii kitu tunza utavaa ukiwa unaondoka ni kosa?nisaidie hilo.
Mimi ni Chama gani natakiwa nielekeze uvae chama gani kama unapenda sare za chama, nisaidie hilo nieneze chama gani?
Mwandishi: Pale palikuwa ni eneo binafsi la kazi hapakuwa na mkutano wa chama au kikao ambapo mtu ana haki ya kuvaa nguo yoyote iwapo kazi hiyo hawana sare za kazi wanazotakiwa kuvaa.
Chacha Heche: Kwa muktadha wa kueneza chama na kiitikadi unaruhusiwa wewe ukiwa unafanya kazi kwangu ufanye na sare zako zinazokinzana na Itikadi yangu?.
Mwandishi: Ni kifungu gani kwenye Ilani yenu au katiba yenu ya chama inasema mtu akiwa anafanya kazi kwako anatakiwa asivae sare isiyo ya chama chako?.
Chacha Heche: Kila mwanachama kwa mujibu wa katiba ni mwenezi wa chama, CCM wanatumia ubabe sisi tunashawishi kukuonesha madhara yao.
Chacha Heche: Ndio maana nachukia anayechanganya siasa na kazi muda wa kazi ni kuweka vyama pembeni ungekuwa na nia ya kunielewa ungenielewa. .....kama aliitwa CCM sisi hatumfungi amepata mtaji, wawasaidie watu wote wanaohangaika na maisha wawatoe kwenye shida nchi nzima.
Mwandishi:Kwenye ile Clip ulisikika ukisema " yaani mimi nikulipe alafu uvae sare ya CCM, lakini Marwa alisema aliyempa kazi ni Mseti na siyo wewe, je nani aliyempa kazi?.
Chacha Heche: Kazi ni yangu mimi huwa nikiwa bize Mseti ananisaidia kuwapa ujira ili wasinisubiri, huo ni utaratibu wangu maana hakuna mkataba wa maandikiano yeye na Mseti sasa wanajuaje kazi siyo yangu.
Kilichosemwa na CHADEMA Tarime
DIMA ONLINE imewasiliana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Tarime Mjini, Bashir Abdallah (Sauti) kufahamu Chama kinasema nini kuhusiana na Video hiyo naye amesema;
Bashir Abdallah
"Mwandishi kwakuwa Chama cha CCM ngazi ya Taifa tayari kimejitokeza kuzungumza kupitia taaarifa waliyoitoa sina cha kuzungumza, nikuombea kwakuwa CCM Taifa ndiyo wamelizungumza hilo la Video basi ni vyema ukazungumza na viongozi wa CHADEMA ngazi ya Kitaifa" amesema Bashir.
Je Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ngazi ya Taifa na Wananchi wanasemaje juu ya Video Clip hiyo?.
Endelea kufuatilia DIMA Online itakujuza.
Post a Comment