VIJANA 70 TARIME KUSOMA BURE MAFUNZO YA UFUNDI FDC
Na Dinna Maningo, Tarime
SERIKALI inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu imegharamia malipo ya ada kwa wasichana 50 ambao hawakubahatika kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne kusoma bure bila malipo elimu ya Sekondari nje ya mfumo rasmi kwa miaka miwili na ufundi kwa fani atakayoitaka.
Pia wavulana 20 kupitia Mjumbe Mstaafu wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Gerald Martine kupitia mfadhili wake wamefadhiliwa kusoma bure katika fani ya useremala na uwashi.
Hayo yamesemwa Desemba, 30, 2022 na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tarime (FDC), Charles Marwa ambaye pia ni Katibu wa Malezi, Elimu na Mazingira Wilaya ya Tarime CCM na Kamishna wa Skauti Wilayani humo wakati akizungumza na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM ngazi ya Kata wakiwemo Wenyeviti na Makatibu Malezi, Elimu na Mazingira katika ukumbi wa Chuo hicho.
"Gharama ya ada unapojiunga na chuo ni 100,000, gharama za bweni ni 145,000 na kwa kutwa ni 150,00 fedha ambazo Rais wetu ameamua kuwasaidia vijana ambao hawakubahatika kufanya mtihani wa kidato cha nne kusoma bure, wao wanachotakiwa kuja nacho siku ya kufungua chuo ni mahitaji yake binafsi kama godoro, Bima ya afya, ndoo ya kuogea hata kama vimeshatumika aje navyo hivyohivyo.
"Rais wetu ameondoa malipo ya ada kwa wasichana 50 watakaojiunga kusoma pamoja na vijana wa kiume waliofadhiliwa na mdau mwingine, tunawashukuru sana kwa ufadhili huo, fursa hii ni kwa kata zote wilayani Tarime.
"Nimewaita viongozi wa Jumuiya ya wazazi kwakuwa uchungu wa mwana aujueye mzazi watusaidie kutafuta vijana wawili kila kata kwajinsi wao watakavyoona njia sahihi za kuwapata vijana kupitia Kata zao" amesema Charles.
Makamu huyo ameongeza" ziliwahi kutoka nafasi za ufadhili tukawapa wenyeviti wa mitaa watusaidie kuwapata vijana hasa wale ambao walishindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali, vijana wanaotoka kwenye mazingira magumu toka Tarime.
"Chakusikitisha baada ya kupokea vijana tukagundua baadhi ya vijana walitoka nje ya Tarime , mwingine alitoka Geita, Rorya , Kenya na maeneo mengine hatukuweza kuwakataa maana tayari walikuwa wamekuja na mabegi tukawaacha wakaendelea na masomo, sasa hivi tumeona tuwatumie Jumuiya ya Wazazi watusaidie kutuletea vijana kutoka kwenye maeneo yao" amesema Charles.
Mjumbe Mstaafu wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi CCM Gerald Martine amesema ataendelea kutafuta wafadhili ili kusaidia vijana wapate elimu.
"Uchungu wa mwana aujuaye mzazi, mimi nimetafuta mfadhili akakubali kulipia vijana 20 mtajua wenyewe namna mtawapataje hao vijana, wafadhili wakija wakakuta tumefanya vizuri wataongeza idadi ya vijana wengine, tukifanya vibaya wataondoa msaada.
"Hizi fursa ni adimu wengine wakipata wanazigombania ila huku kwetu zikija siasa zinaingia, naomba Tarime ni yetu tuijenge kwa pamoja"amesema Gerald.
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji CCM Wilaya ya Tarime, Daniel Bhoke amesema wazazi wasiwanyime watoto fursa ambao walishindwa kusoma kutokana na sababu mbalimbali.
Katibu Jumuiya ya Wazazi Kata ya Nkende Jastine Marwa Manga amempongeza Makamu huyo wa chuo kwa kuwapa wazazi jukumu la kutafuta vijana kwakile alichosema kwamba Jumuiya hiyo imekuwa ikisaulika.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kutoa fursa hii kwa vijana wa Tarime kijifunza ufundi na elimu ya Sekondari, tunamshukuru Katibu Malezi kwa kulisimamia hili, ni kiongozi anayetekeleza ahadi zake kwa vitendo.
" Sasa ni jukumu letu kwenda huko kwenye Kata zetu tukae na viongozi wetu tuone tunawapata vipi hao vijana wawili kila kata, tumepewa fomu tukishajadiliana watajaza ambazo zimetolewa bure bila gharama" amesema Manga.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Binagi amesema" Tunampongeza Kaimu Mkuu wa Chuo wakati wa uchaguzi alituahidi kushirikiana na sisi Jumuiya ya Wazazi kusaidia elimu.
"Tunamshukuru na Gerald kuwezesha vijana wa kiume kusoma bure, tunaenda kukaa na jamii ili tuone namna gani ya kupata hawa watoto " amesema John.
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji CCM katika Wilaya hiyo David Machumbe amewasisitiza viongozi hao wa jumuiya ya wazazi kusaidiana katika shida na raha hata pale watoto watakaposhindwa kwenda shule kutokana na sababu mbalimbali waungane ili kutatua changamoto hizo.
Fani zitolewazo katika chuo hicho ni Mafunzo ya ufundi stadi, ufundi magari, ufundi umeme wa majumbani, kilimo na mifugo, kushona na kudarizi, useremala, uashi na ufundi bomba.
Mafunzo ya muda mfupi ni udereva, kompyuta, kushona na kudarizi, umeme. Mafunzo Maalumu ni elimu ya Sekondari nje ya mfumo rasmi (Elimu haina mwisho), utunzaji wa watoto wadogo na mpira fursa.
Post a Comment