HEADER AD

HEADER AD

CHADEMA KUFUFUA UPYA TRILIONI 1.5 RIPOTI YA CAG


>>>Kimesema kitawaambia wananchi zilikopotelea Trillioni 1.5

>>>Chatarajia kutaja miradi iliyojengwa kwa fedha za mikopo

Na Dinna Maningo, Tarime

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kimesema kinatarajia kutoa elimu na kuwaambia wananchi kuhusu fedha Tsh. Trilioni 1.5 zilizotajwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2016/2017.

Chama hicho kimesema kwamba kwa mujibu wa aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Assad, ilielezwa kiasi hicho kutojulikana matumizi yake hivyo kupitia mikutano ya hadhara kitawaelimisha wananchi na kueleza zilikopotelea fedha hizo. 

Pia kitawaambia wananchi juu ya miradi mbalimbali iliyotekelezwa kwa fedha za mikopo kutoka nje ya nchi licha ya Serikali ya awamu ya tano iliyoongozwa na Hayati Dkt.John Magufuli kudai kutekeleza miradi kwa fedha za mapato ya ndani na sio kwa fedha za mikopo kutoka nchi za nje.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Tarime Mjini, Bashir Abdallah maarufu Sauti wakati akizungumza na DIMA Online akieleza namna walivyojipanga kufanya mikutano ya hadhara na baadhi ya hoja wanazotarajia kuzisema kwa wananchi.

"CAG alikagua hesabu za Serikali Trilioni 1.5 hazikujulikana zimepotelea wapi si maneno yetu ni maneno ya CAG ambaye ni mtu wa Serikali na ni chombo halali cha Serikali ambacho kina mamlaka ya kukagua mahesabu ya Serikali kikikagua taasisi zote vikiwemo vyama vya siasa kama ambavyo hata sisi CHADEMA tumekuwa tukikaguliwa.

" Ni fursa kwetu kuitumia mikutano ya kisiasa ya hadhara kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mambo mbalimbali zikiwemo fedha Trilion 1.5 ambazo hazijulikani zipo wapi na hazina maelezo" amesema Bashir.

Akieleza kuhusu miradi iliyojengwa kwa fedha za mikopo iliyodaiwa kujengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya nchi amesema " Wapinzani tuna mambo mengi ya kuzungumza ni pamoja na ukopaji wa fedha ambao ulikithiri fedha zilikopwa sana kutoka nje ya nchi.

"Lakini Watanzania tukawa tunadanganywa kwamba zinatokana na Mapato ya ndani, mambo ambayo tulipaswa kuyazungumza, kuwaelimisha wananchi wayafahamu ili waweze kujua kwamba pesa hii siyo ya kukopa ama pesa hii ni ya kukopa.

" Kwahiyo miradi yetu imeendeshwa kwa fedha za kukopa. Wananchi na jamii nzima ya Kitanzania walipaswa kuyafahamu haya kupitia mikutano ya hadhara lakini ilizuiliwa ikafungwa"amesema Bashir.

Akizungumzia athari ya kisiasa ya kufungwa kwa mikutano ya hadhara, Bashir amesema kutofanyika mikutano kulivikosesha vyama vya siasa kunadi Sera na Itikadi zao kwa jamii lakini vilevile kupata wanachama wapya.

"Mikutano ya kisiasa inatoa fursa vyama vya siasa kutoa Sera na Itikadi zao kwa jamii, wananchi kujiunga na chama hicho kutokana pia na falsafa ya vyama hivyo, mikutano ilisaidia vyama kukua na kupata wanachama.

"Kustishwa kwa mikutano ilikuwa ni ukiukwaji wa Katiba Ibara ya 20 hili hali inataja vyama vipo huru kukutana na wananchi na kutafuta wanachama, hali hiyo ilipelekea nchi hii kuonekana sio ya kidemokrasia ni nchi inayoendeshwa kwa mfumo ambao viongozi wanataka kuendesha wanavyotaka wao na sio inavyotaka Katiba na Sheria za nchi"amesema.

Ameongeza" Tulifungiwa hata vikao vya ndani ulikuwa ukionekana Polisi wanakuja kukuzuia kuwa hamruhusiwi kufanya mikutano, mfano Mwenyekiti wetu Mbowe na viongozi wetu wa Kitaifa kwa nafasi walizo nazo katiba imewapa mamlaka ili waitishe mikutano wazungumze na watu lakini mambo hayo yalikuwa hayafanyiki yalizuiliwa.

"Mbowe anaambiwa anapaswa kufanya mkutano kama ni mbunge wa eneo husika wakati huyo ni kiongozi wa Chama wa Kitaifa kama ilivyokuwa kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa awamu iliyopita aliyekuwa akizunguka nchi nzima na kufanya mikutano.

"Tulinyimwa Demokrasia CCM ikawa inafanya mikutano mara kwa mara wakati huo wanazuia vyama vingine kufanya mikutano, yaani mnakwenda kukutana kamati tendaji ya chama lakini mnazuiliwa, hii ilididimiza haki na ustawi wa jamii, taifa na maendeleo" amesema Bashir.

DIMA Online ilimuuliza Mwenyekiti huyo kwamba je kuzuiwa kwa mikutano huwenda ni kwasababu ya mikutano ya kisiasa ya vyama vya upinzani kudaiwa kugubikwa kelele, vijembe na majungu badala ya hoja za msingi zinazochochea maendeleo? naye amesema.

           Mwenyekiti CHADEMA Jimbo la Tarime Mjini Bashir Abdallah

"Makelele huwezi kuyaogopa kwa kuwafungia watu wasizungumze ukifunga watu wasizungumze ndio unatengeneza janga kubwa zaidi kwasababu hujui fikra zao hujui wanawaza nini.

"Mwisho wa yote kama watu hawazungumzi na hawakutani matokeo yake utapata Taifa ambalo halitakuwa na ustawi wa kijamii na halitakuwa na maendeleo kwasababu Demokrasia ndio inaleta maendeleo" amesema Bashir.

Amesema mikutano ya hadhara haikusitishwa kutokana na kelele za kisiasa" Ilistishwa kutokana na uoga wa watawala wa viongozi wa awamu iliyopita, walijipa sifa ya wao kuwa ni watakatifu ikapelekea wao kuwa waoga kusemwa na kukosolewa.

"Haukuwepo uhuru wa wananchi kuhoji Lakini sasa tuna uwezo wa kulihoji hilo na kupata ukweli,  je ni wapi tutatoa elimu hiyo ni kukutana kwenye mikutano ya hadhara kuwapa elimu ikiwemo ya Trilion 1.5 " amesema kiongozi huyo.

Bashir amesema mikutano ya hadhara ilikuwepo hata kabla ya uhuru na kwamba mikutano ilipostishwa walitumia bunge lao la wananchi kusema mambo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

"Sisi CHADEMA tuna bunge la wananchi maana yake wale wote waliogombea ubunge nchini wana Spika Suzan Lyimo na Spika anaendelea na kazi zake na wabunge wanaendelea kuwasemea wananchi popote walipo kwa kutumia Vyombo vya Habari vikiwemo vya mitandao ya kijamii na vikao mbalimbali" amesema.

Kuhusu Rais Samia kuruhusu mikutano ya jadhara Mwenyekiti huyo amepongeza hatua hiyo huku akisisitiza umuhimu wa kupata katiba mpya ambayo itakuwa na udhibiti wa viongozi watakaokiuka katiba.

"Tunahitaji Katiba mpya ambayo itakuwa na udhibiti wa viongozi ambao wanataka kukiuka katiba ili kuwepo na mwelekeo mmoja wa nchi ambao utatusaidia kila atakayeingia kwenye mamlaka au kwenye taasisi anaiheshimu katiba kwasababu ameapa kuilinda kwa hali na mali na viapo vingine anavyoviapa," amesema.

Mwenyekiti huyo amepongeza kurejeshwa kwa mikutano ya hadhara na kusema kuwa Rais Samia amekidhi mahitaji ya Katiba Ibara ya 20 inayoruhusu mikutano ya hadhara pamoja na Sheria ya vyama vya siasa ya 1992.

"Mikutano hii ilikuwepo hata kabla ya uhuru, Chama cha TANU na TAA vilikuwa ni vyama vya upinzani kwa mkoloni na wao walikuwa wanafanya vikao na mikutano, Nyerere alikutana na watu mbalimbali, wafanyakazi na wananchi ili wamuunge mkono wamwondoe mkoloni na walimuondoa" amesema Bashir.

Mwenyekiti huyo ameiambia DIMA Online kwamba mikutano ya hadhara itaanza ndani ya mwezi huu Januari, 21, 2023, utafanyika uzinduzi wa Kitaifa wa mkutano wa hadhara wa kwanza katika eneo litakalopangwa na Kamati kuu.

Amesema baada ya mkutano huo kila Kanda zitafanya uzinduzi kwenye Makao Makuu ya Kanda na kisha Mikoa na Majimbo.


No comments