HEADER AD

HEADER AD

WATU WENYE ULEMAVU: MIKUTANO ITAMSAIDIA RAIS KUPATA TAARIFA ZILIZOJIFICHA


Na Dinna Maningo, Tarime

BAADHI ya Watu wenye Ulemavu wa Viungo Wilayani Tarime Mkoa wa Mara, wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu kuisimamia Katiba ya nchi kwa kuondoa zuio la mikutano ya hadhara lililotolewa na Serikali iliyopita ya awamu ya tano iliyoongozwa na Hayati Dkt John Pombe  Magufuli.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na DIMA ONLINE wamesema wamefurahishwa na kauli ya Rais Samia aliyoitoa hivi karibuni ya kuondoa zuio na kuruhusu mikutano ya hadhara ya kisiasa kwa kile walichoeleza kuwa itamsaidia Rais kupata taarifa mbalimbali ambazo pengine bila mikutano asingezifahamu.

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Halmashauri ya Mji Tarime, Mekaus Maingu amesema Rais Samia ametekeleza Katiba Ibara ya 20 inayotoa haki ya watu kukutana na wengine, kushirikiana, kuchangamana na kutoa mawazo yao.

            Mekaus Maingu

"Tunampongeza sana Rais Samia ni msikivu, watu walilalamika sana kuzuiliwa kwa mikutano ya hadhara ametumia busara kubwa kuhakikisha anaisimamia Katiba na kuilinda.

"Kupitia mikutano ya siasa atapata taarifa nyingi za hadhara hata ambazo zilikuwa ni siri, kama ni mapungufu atayajua na kuyarekebisha na akubali kukosolewa maana unapokosolewa inakusaidia kuyajua mapungufu kisha unayaboresha" amesema Mekaus.

Katibu huyo wa Shirikisho amesema mikutano ndio mawasiliano na ina faida kubwa kwa taifa na kwamba kuzuia mikutano ilikuwa ni uoga wa Chama Tawala kutokosolewa kwani mikutano inasaidia kujua kinachoendelea na kujua unasemwa vipi.

Ameongeza kuwa kipindi mikutano imezuiliwa ilileta athari kubwa kwakuwa watu hawakuweza kuwa na uhuru wa kuzungumzia mustakabali wa nchi yao kwani hata kama kulikuwa na jambo nyeti la kuzungumzwa watu waliogopa kusema.

"Zuio la mikutano lilididimiza Demokrasia, likadidimiza uhuru wa kujieleza, vyombo vya Habari vilikosa taarifa nyingi ambazo zingepatikana kupitia mikutano ya hadhara.

"Utulivu uliokuwepo siyo kwamba ni kwasababu ya kufunga mikutano ni kwasababu watu waliingiwa woga wakaogopa kuzungumza mioyo yao haikuwa huru na amani"amesema Mekausi.

Mkazi wa Mtaa wa Uwanja wa Ndege Myonge Paul, amesema mikutano ilipostishwa ilikuwa ni vigumu kufahamu Serikali ya CCM imewafanyia nini wananchi na hivyo kubaki kuwa siri kwenye ofisi za Serikali.

                    Myonge Paul

"Kustishwa kwa mikutano ilileta hasara kwasababu hata wanaccm hawakufanya mikutano ya hadhara ili kuwapa fursa kueleza wananchi yanayofanywa na serikali inayoongozwa na chama tawala kupitia viongozi wa chama.

"Pia jambo lilipofanyika ilikuwa ngumu kujua kama vile vitendo vya rushwa, ubadhilifu, ufujaji wa fedha za miradi, mambo mengine yalifanyika kwa usiri kimyakimya lakini ingekuwepo mikutano yangesemwa hadharani na wananchi wangeyafahamu.

Myonge amesema mikutano ya siasa ni sehemu ya mahubiri wananchi kuhubiriwa siasa, kutokuwepo mikutano ilitenganisha vyama vya siasa kuwa pamoja na wananchi kwakuwa mikutano inasaidia watu wakutane, waungane pamoja.

"Mikutano ya hadhara kila mtu anakuwa wazi anaeleza jambo lake wazi bila kufumbafumba na kuficha na watu wanamsikiliza hiyo ndiyo Demokrasia inayotakiwa kwenye nchi yetu.

"Mikutano ya siasa inasaidia watu kujifunza siasa kupitia mikutano ilimradi tu  izingatie taratibu na sheria vikiwemo vibali vya mikutano" amesema Mnyonge.

Yohana Wilson ameshukuru mikutano ya hadhara kuruhusiwa kwakuwa kila mtu atakuwa yupo tayari kusema la moyoni huku akimpongeza Rais Samia kwa kuendesha nchi vizuri.

               Yohana Wilson

"Mikutano ya hadhara ya kisiasa imerudi hakika mustakabali wa nchi yetu unaenda vizuri, sasa hivi mtu atakuwa tayari kusema la moyoni kwakuwa kuna uhuru kiasi fulani tofauti na huko nyuma wakati wa Serikali ya awamu ya tano.

"Angalau nchi imepambazuka na watu wameanza kujisikia wapo huru kwahiyo mtu akiwa na kero yake anaweza kueleza akasema hata lile linalomsumbua kutoka moyoni, watu waliogopa kusema hata kama anataka kuzungumzia cha kusaidia jamii.

Yohana ameongeza kusema" Watu waliogopa kusema wakihisi kupotezwa na wasiojulikana kwa sababu mengine yaliwahusu viongozi, na uongozi wa Serikali iliyopita haukuhitaji kukosolewa wala kusikiliza walio wengi wanasemaje.

Amesema Rais Samia amefanya maamuzi mema kwa kuilinda katiba na kwamba sasa wapo huru wana uhuru wa kuongea ilimradi sheria za nchi hazivunjwi.

                        Rais Samia

Nukuu ya Katiba

>>>Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 20-.(1) inasema Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.


No comments