HEADER AD

HEADER AD

DIWANI ADAIWA KUKWAMISHA UJENZI BUKENYE SEC.


>>>Wananchi wagoma kujenga shule
>>>Wasema Diwani alisema wasichange michango
>>> Wamuhitaji Dc waseme kero zao

Na Dinna Maningo, Tarime

IMEELEZWA kuwa sababu ya shule ya Sekondari Bukenye Kata ya Manga, Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara, kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, Ofisi ya walimu ni kuwepo mgomo wa wananchi kutochangia maendeleo ya shule.

Baadhi ya Wananchi na Viongozi wa Serikali za Vijiji na wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Manga, wamesema kwamba kipindi cha kampeni uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Diwani wa Kata ya Manga Steven Gibai aliwaambia endapo wakimchagua na akashinda udiwani hawatachangia maendeleo na shule itajengwa kwa fedha za Serikali.

Kauli ya Diwani wakati wa kampeni imeelezwa kuleta athari jambo ambalo litasababisha wanafunzi 262 waliochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo kuchangia vyumba vinne vya madarasa kutokana na upungufu wa madarasa.

                         Madarasa

Endapo wanafunzi hao wote wataripoti shule, wanafunzi 102 watakosa madarasa hivyo watalazimika kutumia madarasa manne badala ya sita kwa mujibu wa mwongozo wa elimu unaoelekeza shule za sekondari darasa moja litumiwe na wanafunzi 40.

Vyumba hivyo vinne vya madarasa ni darasa moja pekee ndilo lenye viti na meza hivyo kama wanafunzi wote wataripoti shule wanafunzi 40 ndio watapata viti na meza na 222 watakosa viti vya kukalia na meza.

Pia Darasa moja lenye viti na meza limejengwa kwa fedha za Serikali maarufu fedha za Samia, madarasa mawili yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi hayana madawati na viti pamoja na darasa moja lililojengwa kwa fedha za mapato ya ndani Tsh. Milioni 20 kutoka kwenye akaunti hiyo ya shule.

DIMA ONLINE imefika katika Shule ya Sekondari Bukenye iliyopo Kijjiji cha Bisarwi Kata ya Manga, pia imefanikiwa kuzungumza na baadhi ya wananchi, viongozi wa serikali za vijiji na viongozi wa CCM ambao wameeleza sababu ya shule hiyo kuwa na changamoto lukuki.

                        Madarasa

John Mwita mkazi wa Kijiji cha Bisarwi amesema" Tatizo la wananchi kutochangia maendeleo ni kwasababu wakati kata ya Komaswa haijaanzishwa tukiwa kata moja ya Manga tulijenga Sekondari ya Manga, baadae vijiji vitatu vikaundwa na kuwa Kata ya Komaswa tukabaki vijiji vitatu, wale wa Komaswa hawakuwahi kuchangia ujenzi shule ya Bukenye.

" Kitendo hicho kiliwakatisha tamaa wananchi wa vijiji vingine wanaona hata hii shule wakitoa nguvu kazi siku zijazo wataiacha na kujenga yao, wanaona ni kama wanajisumbua ndio maana hawataki kuchangia maendeleo" amesema John.

Mkazi wa Kijiji cha Kembwi Marwa Chacha amesema" Wakati wa kampeni Diwani alijinadi kwenye mikutano yake kwamba tukimpa kura akashinda hatutasumbuka kufanya maendeleo na shule itajengwa" amesema.

                         Darasa

Ghati Chacha mkazi wa Kijiji cha Mtana amesema," Tuliambiwa tukimchagua Diwani hatutachangishwa michango kujenga shule, akatuambia Serikali itajenga madarasa yote, sasa leo anawezaje kuwahamasisha wananchi kuchangia maendeleo wakati aliwahakikishia kuwa akishinda hawatasumbuka na michango ya ujenzi wa shule" amesema.

Viongozi Serikali ya Kijiji wazungumza

Viongozi wa Kijiji hicho wamesema Kata hiyo ina vijiji vitatu, Kembwi, Bisarwi na Mtana, shule ya Bukenye ilianzishwa kama shule ya Kata lakini ujenzi ulipoanza Kijiji cha Mtana anakotoka Diwani pamoja na Kijiji cha Kembwi waligomea ujenzi.

Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Bisarwi Nyakimori Machango amesema wananchi wa Kijiji hicho wana nia njema ya kuchagia mendeleo lakini wamekata tamaa baada ya kuona watoto wa vijiji jirani ambao wazazi wao wamegoma kuchangia ujenzi wakisoma katika shule hiyo bila kuchagia chochote.

             Mjumbe Serikali ya Kijiji, Nyakimori

" Diwani ndiye msimamizi wa maendeleo ameshindwa kusimamia maendeleo amekibagua Kijiji, baada ya kuona haungwi mkono na Kijiji kutokana na mapungufu haya ya shule ametutenga na anatarajia kuanzisha shule kwenye Kijiji chake na Mtedaji wa kata nae ameungana na Diwani ameshidwa kusimamia shule.

"Shule karibu ifunguliwe madarasa ni machache hakuna madawati, cha ajabu Diwani anasema ameshaomba fedha Halmashauri kujenga shule mpya ya Sekondari Kijiji cha Mtana , kiongozi anatakiwa kuwakusanya watu wake kuwaweka pamoja alafu yeye ndiye anatugawa" amesema Nyakimori.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makoro Juma Matinde amesema" Rais Samia anajitahidi sana kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira mazuri lakini baadhi ya viongozi  wanakwamisha maendeleo, viongozi wanaotenga wananchi hao sio viongozi, tunamuomba Mkuu wa Wilaya aje atembelee hii shule aone changamoto" amesema Juma.

        Mwenyekiti wa Kitongoji, Juma Matinde

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bisarwi Robert Mosonja amesema " Hii shule ina changamoto nyingi wanafunzi 262 wamepangwa kusoma kwenye hii shule lakini madarasa yaliyopo ni matatu, shule ilianzishwa kwa mpango wa shule ya Kata lakini vijiji viwili Mtana na Kembwi hawajawahi kushiriki kwenye ujenzi wa shule, kijiji cha Bisarwi ndicho kimejenga lakini watoto wao wanasoma kwenye hii shule huu ni uonevu.

"Kuna Madarasa matatu yamejengwa hayajakamilika ila yameezekwa bati, wakati wanataka kusajili hii shule Diwani alituambia ili ipate usajili mpaka iwe na madarasa matano, akaenda kuongea na mtu mmoja bila kushirikisha viijiji akamwambia atumie fedha zake ajenge madarasa mawili kwa Milioni 40 alafu Halmashuri ikiingiza fedha kwenye akaunti watamlipa.

Ameongeza kusema "Yule mtu akajenga madarasa mawili yakaezekwa kwa bati ila bado hayajakamilika hayana, lipu, madirisha, milango na sakafu na ukamilishaji mwingine.

" Alipoenda kuomba malipo ya awali ili akamilishe ujenzi imeshindikana kumlipa kwamba taratibu za zabuni na fedha hazikufuatwa wakasema yalikuwa makubaliano ya Diwani na huyo aliyechukua kazi kujenga hayo madarasa matatu ambayo hayajakamilika.

              Mwenyekiti Kijiji cha Bisarwi

"Wakaguzi wakaja na TAKUKURU jengo likasimamishwa wakasema hawezi kulipwa hivyo madarasa mawili yapo na moja lililojengwa kwa fedha za mapato ya ndani yameshindwa kukamilishwa ili kusaidia kupunguza changamoto ya vyumba vya madarasa kwakuwa taratibu za ujenzi na fedha hazikufuatwa , huyo mtu amepanga kufungua kesi Mahakamani akidai malipo yake.

             Ujenzi uliosimama

Mwenyekiti huyo amesema fedha Milioni 70 ziliwekwa kwenye akaunti ya shule kama malipo lakini imeshindikana kulipwa kwa madai ya taratibu za ujenzi kutofuata ikiwemo kutotangazwa zabuni na kwamba kati ya fedha hizo Milioni 20 zilitolewa zikajenga darasa ambalo litatumiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza.

"Mbunge Waitara aliwahi kuja hapa japo safari hii amepita kwenye vijiji vingine hiki cha Bisarwi hajapita tena, alisema shule nyingine isijengwe hadi hii ikamilike.

"Tunashangaa Diwani tukiwa kwenye vikao akatuambia tayari ameshaomba fedha Milioni 450 kujenga shule nyingine ya Sekondari katika Kijiji chake cha Mtana  wakati hii shule ambayo ndio ya kata haijamalizima ujenzi amekuwa mbaguzi na mkwamishaji wa maendeleo ya hii shule " amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kembwi Mwita Yacobo amesema shule hiyo ilianzishwa kama shule ya Kata lakini wananchi wamegoma kujenga wakidai watajenga kwenye Kijiji chao.

             Shule ya Sekondari Bukenye

"Wananchi wanakataa wanasema wakijenga shule ya Bukenye ambayo ipo Kijiji cha Bisarwi kwa baadae watalazimika kujenga yao, nilishawashawishi lakini wananchi hawataki.

"Viongozi wa juu waje maana sisi wadogo tunapuuzwa, wanasema walijenga shule ya Sekondari Manga lakini walivyogawa kata Komaswa haikushiriki huu ujenzi ndio sababu wamesusia.

" Wanasema wakijenga na hii badae wakigawa Kata wataiacha, hii imekuwa changamoto sana, tulijenga Manga tukiwa vijiji sita baadae vijiji vya Surubu, Nyamirambalo na Komaswa vikatengwa na kuwa Kata ya Komaswa.

 Shule ya Manga ikahesabiwa Komaswa tangu hapo Komaswa hawakutusaidia ujenzi wakati Manga tuliijenga vijiji vyote, awali tulipanga mchango sh.33,000 kwa kila kaya ili kujenga nyumba ya mwalimu lakini hakuna waliochangia" amesema Mwita.

Mwenyekiti Kijiji cha Mtana Marwa Sagaga amesema shule hiyo ina changamoto nyingi, awali wanakijiji walichanga fedha zikanunuliwa tripu sita za mchanga na mawe tripu 10 ili kujenga msingi wa madarasa mawili lakini siku chache baadae wananchi waligoma kuchangia ujenzi.

                        Darasa

"Tulifanya mkutano ili tuchange fedha za kujenga nyumba ya mwalimu lakini wakakataa kuwa walishajenga Sekondari ya Manga lakini wao hawajawahi kusaidia ujenzi wa shule ya Bukenye.

"Kitu kingine kinachosumbua ni siasa mtu anaahidi kuwa mkinichagua hamtachangia ujenzi kuwa Serikali itajenga madarasa, wananchi wamegoma wameiachia Serikali ijenge, mtatulaumu Wenyeviti, Kijiji tuna  fedha zilichangwa laki saba tutaanzia hizo kujenga msingi wa nyumba ya mwalimu, serikali ya wilaya ije itusaidie kutatua hili jambo" amesema Marwa.

Mjumbe wa Bodi ya shule  Eliud Magesa amesema Wenyeviti wa vijiji vilivyokacha maendeleo wameshaitwa mara nne kwenye vikao vya bodi ya shule lakini hawakutii wito.

                   Mjumbe wa Bodi ya shule

"Tatizo kubwa ni upungufu wa shughuli za maendeleo hasa ya shule, mimi natoka Kijiji cha Kembwi lakini viongozi wangu wa kijiji na wananchi walishagoma kushiriki maendeleo, tulishawaita kwenye vikao vya bodi mara nne wenyeviti wa vijiji Mtana na Kembwi, Diwani na Mtendaji wa Kata lakini hawakufika.

"Wenyeviti ni wahamasishaji wa maendeleo, Mtendaji ni mtekelezaji ,wakati wa ujenzi wa shule mwaka 2018 tulipendekeza kijiji cha Kembwi na Mtana wenyewe wajenge nyumba za walimu lakini hadi sasa hakuna nyumba ya mwalimu hata moja wanaishi kwenye nyumba za kupanga, wanatembea umbali mrefu kuja kufundisha.

Mjumbe huyo amesema Diwani amekuwa ni tatizo " Anataka shule nyingine ijengwe kwenye kijiji chake, wakati wataalam toka Wizarani walikuja kupima eneo la kujenga shule, Diwani aliwataka wakapime eneo la Nyabiga anakoishi yeye wale wataalam wakakataa wakasema eneo waliloambiwa wapime ni hapa palipojengwa shule .

"Tangu siku hiyo Diwani akakichukia Kijiji cha Bisarwi, akajitenga na maendeleo ya Kijiji , Kijiji changu niliwaomba wachangie maendeleo mimi nipo tayari kuleta fundi kwa gharama zangu lakini hakuna waliojitokeza kuchangia maendeleo ya shule" amesema Eliud.

Mjumbe huyo wa Bodi amesema Shule ya Bukenye ina wanafunzi 262 wanaotarajiwa kuanza masomo mwezi huu, kidato cha pili wapo 139 na kidato cha tatu wanafunzi 53, walimu wapo watano.

 " Ina vyumba vya madarasa 8 ,vyoo matundi sita na choo cha walimu matundu mawili,  kwa kidato cha kwanza kuna madarasa manne, yanahitajika madarasa sita na hivyo kuwepo na upungufu wa madarasa mawili huku madarasa matatu yakiwa hayana viti na meza.

Viongozi CCM wasema Ilani itekelezwe

Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 Ibara ya 77 inasema Sera ya msingi ya CCM kuhusu huduma za kijamii ni kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na fursa ya kupata huduma za kijamii bora na za kutosha bila kikwazo.

Ibara ya 78 inatambua rasilimali watu ikiwa ni pamoja na elimu kutolewa bila malipo, kuimalisha mazingira ya kujifunza na kufundisha na kuajili walimu katika ngazi zote za elimu.

Mwenyekiti wa Tawi la Bisarwi Chama cha Mapinduzi amesema" Mimi nina miezi minne tangu nichaguliwe wananchi huwa wananihoji hii ni shule ya Kata au ya Kijiji? kama ni ya Kata kwanini vijiji vingine havishiriki ujenzi wakasema kama ni hivyo jina libadilishwe shule iitwe Bisarwi Sec. jina la kijiji," amesema.
                  Mwenyekiti Tawi la Bisarwi

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Kata ya Manga Masiaga Kasim amesema ametembelea shule hiyo nakubaini changamoto nyingi, ameiomba serikali kuingilia kati ili ujenzi wa shule ukamilike huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuwezesha fedha za ujenzi wa madarasa nchi nzima.

"Shule ina upungufu wa madarasa,viti na meza, hakuna maji,Umeme, nyumba za walimu, maabara, darasa lililokuwa linatumika kama ofisi ya walimu litatumiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza.

           Mwenyekiti UVCCM Kaya ya Manga

" Hawa ni vijana wenzangu wanatakiwa kusoma kwenye mazingira rafiki wapate elimu bora, hizi changamoto hushusha viwango vya taaluma," amesema Masiaga. 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Manga Samwel Itinde amesema katika utoaji wa elimu bora Ilani ya CCM inatakiwa kutekelezwa katika shule hiyo, ameahidi kusimamia kuhakikisha vijiji vyote vinashiriki katika ujenzi wa shule.

             Mwenyekiti CCM Kata ya Manga

"Tumechaguliwa hivi karibuni na bahati nzuri nimefanya ziara ya kushtukiza hapa shuleni nikakuta ina changamoto nyingi haina kibao cha shule, hakuna bendera ya Taifa, madarasa ni pungufu na hakuna viti na meza kwa baadhi ya madarasa, lazima Ilani itekelezwe na lazima tumuunge rais kwa vitendo" amesema Samwel.

Diwani wa Kata hiyo alipotafutwa kwa njia ya simu ili kujibu malalamiko yanayoelekezwa kwake kwamba yeye ndio mkwamishaji wa maendeleo ya shule, simu yake haikupokelewa na alipotumiwa ujumbe wa maneno alisema yupo kikaoni.

Diwani Kata ya Manga, Steven Gibai

DIMA Online ilimtafuta kwa mara nyingine lakini kila alipopigiwa simu alipokea na kukata simu, jitihada zilifanyika za kumtumia ujumbe wa maneno kumsihi apokee simu, naye alituma ujumbe akiuliza maswali yanahusu nini?

Mwandishi alimtumia maswali kwa ujumbe wa maneno kuhusu madai ya kukwamisha maendeleo ikiwemo kauli iliyotolewa kwenye kampeni zake yakwamba endapo wakimchangua hawatachanga michango, Diwani hakuweza kujibu chochote licha ya kutaka kufahamu maswali.

Afisa Elimu afunguka

AFISA Elimu Halmashuri ya Wilaya ya Tarime, Vanance Babukege amesema wananchi wanatakiwa kushiriki katika maendeleo kwenye shule yao ukiwemo ujenzi wa madarasa, viti, meza na kwamba malumbano katika Kata hiyo yamesababisha shule kutokamilika.

"Nina miezi saba huu ni wa nane tangu nihamie Tarime, nilichokiona huku ni ubinafsi wanajenga shule ovyoovyo hawaziendelezi kitu ambacho ni shida, ukiwashauri fanya hivi wao wanafanya vile.

"Kila koo inataka iwe na shule yao, matokeo yake shule inakuwa na wanafunzi wachache wakati huo zikihitaji walimu, fedha za uhamisho ji changamoto," amesema.

Akizungumzia kutokuwepo bendera shuleni amesema suala la bendera na kibao cha shule vinatakiwa kuwekwa na mkuu wa shule na kwamba bendera ipo isipokuwa hakuna mlingoto. Pia shule hiyo ina miezi miwili toka ianze kupokea fedha za uendeshaji wa ofisi tangu ianzishwe  mwaka 2021.

Kuhusu upungufu wa madarasa amesema wanafunzi hawatakaa chini, shule zitakapofunguliwa kama madawati na viti vitakuwa hakuna utabaki mkondo mmoja wanafunzi wengine (Kidato cha kwanza) wataenda kusoma Manga Sekondari. Ni takribani km.5-6 kutoka vijiji vya Kembwi, Bisarwi na Mtana katika Kata ya Manga kwenda shule ya Manga Sec iliyopo Kata ya Komaswa.

>>> Diwani ni mwakilishi wa wananchi katika Halmashauri, nikiungo na kitovu cha mawasiliano kati ya wananchi  na Halmashauri

Miongoni mwa majukumu na kazi ya Diwani ni pamoja na ;

>>>Kudumisha na kuendeleza udumishaji  wa amani, usalama na utawala Bora.

>>>Kusukuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo la mamlaka yake na Taifa kwa ujumla kwa kuzingatia Sera za Taifa.

>>>Kutekeleza upelekaji wa madaraka ya kisiasa, kiuchumi, kifedha na utawala kwenye ngazi zote za Halmashauri na hasa ngazi za chini za vijiji, vitongoji na mitaa.

>>>Kutafuta na kudumisha vyanzo vya mapato vya kutosha ili kuwezesha kutekeleza majukumu na kazi  zake.

>>>Kuendeleza na kuhimiza afya bora, elimu na burudani na kukuza maisha ya watu ya kijamii na kitamaduni.

>>>Kuwa karibu sana na wapiga kura na kupata ushauri wa wananchi katika mambo yanayotarajiwa kujadiliwa kwenye Halmashauri.

>>>Diwani atateuwa angalau siku moja kila mwezi kukutana na wananchi katika eneo lake la uwakilishi ili kupata maoni yao na kuwajulisha maamuzi ya jumla ya Halmashauri na hatua zilizochukuliwa na Halmashauri kuondoa matatizo yaliyowahi kuelezwa na wananchi wa eneo lake la uchaguzi.

>>>Diwani ana wajibu wa kufuatilia utekelezaji wa miradi na hutoaji wa huduma katika eneo analoliwakilisha, kukosoa hatua za utekelezaji au hutoaji wa huduma za kupendekeza.





No comments