HEADER AD

HEADER AD

BUKENYE SEC ILISAJILIWA BILA KUZINGATIA MWONGOZO


>>> Adhabu za kukiuka taratibu za usajili wa shule

>>> Kulipa faini, kufungiwa kusajili wanafunzi kwa muda na kufutiwa usajili wa shule.

>>> Adhabu hizo zinaweza kutolewa ama moja au zote kwa pamoja.


Na Dinna Maningo, Tarime 

UTOAJI wa Elimu Bora ni nguzo muhimu ya maendeleo katika nchi yoyote duniani na elimu bora husaidia kupata rasilimali watu wenye maarifa, stadi na mahiri katika nyanja mbalimbali na hivyo kuchangia maendeleo ya nchi.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imedhamiria kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa nchini inakidhi viwango vya ubora katika nyanja zote muhimu.

Baadhi ya viwango hivyo ni ubora wa mazingira wezeshi ya utoaji elimu yanayozingatia usalama, afya, ustawi wa wanafunzi sambamba na uwepo wa miundombinu bora na yenye utoshelevu na huduma muhimu za kijamii.

DIMA ONLINE imefika katika shule ya Sekondari Bukenye yenye usajili Na. 5605 iliyopo Kijiji cha Bisarwi kata ya Manga Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.

                   Shule ya Sekondari Bukenye

Ni shule ya kutwa ya Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ilianzishwa mwaka 2021, ilisajiliwa ikiwa na vyumba vya madarasa 5 na vyoo vya walimu na wanafunzi wa kike na kiume. Hadi sasa ina madarasa 8 yaliyokamika ikiwa na kidato cha kwanza hadi cha tatu.

Shule hiyo inakabiliwa na changamoto rukuki Madarasa ni pungufu, haina Ofisi ya walimu, Jengo la utawala, Maabara, Maktaba, baadhi ya madarasa hayana viti na meza.

Hakuna Bwalo, Mwalimu wa somo la Hisabati wa Serikali, nyumba za walimu, chumba cha wasichana cha kujistili, ina upungufu wa vitabu hakuna huduma ya maji na umeme, hakuna Bendera ya Taifa na kibao cha shule.

Mjumbe wa Bodi ya shule ya Sekondari Bukenye, Eliud Magesa anasema shule hiyo imepangiwa wanafunzi wa kidato cha kwanza 262 kwa mwaka 2023, Kidato cha pili wapo 139 na kidato cha tatu ni 53, ilisajiliwa ikiwa na madarasa 5 hadi sasa ina madarasa 8 yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi na Serikali.

 Mjumbe wa Bodi ya shule ya Bukenye

Mjumbe wa bodi anasema wananchi wameshindwa kuendeleza ujenzi kutokana na sababu za kisiasa hivyo kusababisha kuwepo mgomo katika kuchangia shughuli za maendeleo huku akiwasisitiza wenyeviti wa vijiji hivyo na uongozi wa kata na Serikali kwa ujumla kuhamasisha wananchi kujenga madarasa na nyumba za walimu.

Inaelezwa kuwa endapo wanafunzi hao wote wataripoti shule, wanafunzi 102 watakosa madarasa hivyo watalazimika kutumia madarasa manne badala ya sita kwa mujibu wa mwongozo wa elimu unaoelekeza shule za sekondari darasa moja litumiwe na wanafunzi 40.


Vyumba hivyo vinne vya madarasa ni darasa moja pekee ndilo lenye viti na meza hivyo kama wanafunzi wote wataripoti shule wanafunzi 40 ndio watapata viti na meza na 222 watakosa viti vya kukalia na meza.

Pia Darasa moja lenye viti na meza limejengwa kwa fedha za Serikali maarufu fedha za Samia, madarasa mawili yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi hayana madawati na viti pamoja na darasa moja lililojengwa kwa fedha za mapato ya ndani Tsh. Milioni 20 kutoka kwenye akaunti hiyo ya shule.

Mwenyekiti Kijiji cha Mtana katika Kata hiyo Marwa Sagaga anasema shule hiyo ina changamoto nyingi, awali wanakijiji walichanga fedha zikanunuliwa tripu sita za mchanga na mawe tripu 10 ili kujenga msingi wa madarasa mawili lakini siku chache baadae wananchi waligoma kuchangia ujenzi.

" Kuna fedha zilichangwa na wana Kijiji  laki saba, tutaanzia hizo ili tujenge nyumba ya mwalimu na tutahamasishana ili shule ikamilike ujenzi na nyumba za walimu" anasema Marwa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Kata ya Manga Masiaga Kasim anasema ametembelea shule hiyo nakubaini changamoto nyingi, ameiomba serikali kuingilia kati ili ujenzi wa shule ukamilike huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuwezesha fedha za ujenzi wa madarasa.
                  Mwenyekiti UVCCM Kata ya Manga

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Manga Samwel Mseti anasema katika utoaji wa elimu bora Ilani ya CCM inatakiwa kutekelezwa katika shule hiyo, ameahidi kusimamia kuhakikisha vijiji vyote vinashiriki katika ujenzi wa shule.

 Mwenyekiti wa CCM Kata ya Manga

Mwongozo 

Shule ya Sekondari Bukenye imesajiliwa ikiwa haijatimiza mahitaji ya miundombinu ya shule kama mwongozo wa uanzishaji na usajili wa shule unavyoelekeza.

Katika kutimiza azma ya utoaji wa elimu bora nchini, Wizara hiyo ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2020 ilitoa mwongozo wa uanzishaji na usajili wa shule za serikali na shule binafsi kwa kutwa na bweni ili kuhakikisha uwepo wa mfumo wa elimu wenye kuleta ufanisi na matokeo chanya.

Mwongozo wa uanzishaji na usajili wa shule unakusudia kuwaelekeza wadau wa elimu kuhusu masuala muhimu ya kuzingatia katika uanzishaji na usajili wa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.

Mwongozo huo umeandaliwa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo katika utoaji wa Elimu nchini. Walengwa wakubwa wa mwongozo huo ni wadau wote wa elimu wanaokusudia kuanzisha na kusajili shule.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina wajibu kisheria kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa ina ubora wa kutosha kuleta maendeleo ya haraka nchini.

Adhabu kwa kuvunja Sheria

Katika kuhakikisha elimu inayotolewa ina ubora , Serikali imeweka adhabu kwa kuvunja sheria, adhabu za kukiuka taratibu za usajili zimeainishwa katika Sheria ya Elimu ya mwaka 2002 Sura ya 353, sehemu ya 8 kifungu cha 60 (g) ikiwa ni pamoja na kulipa faini, kufungiwa kusajili wanafunzi kwa muda na kufutiwa usajili wa shule. Adhabu hizo zinaweza kutolewa ama moja au zote kwa pamoja.

Mwongozo unaelekeza kwamba mwombaji kama vile Halmashauri, Shirika, Taasisi, Jumuiya au mtu binafsi anayetaka kuanzisha shule anapaswa kuzingatia sheria ya Elimu Sura Na 353 na Sera ya elimu na mafunzo iliyopo na atawasilisha barua ya maombi kwa Kamishna wa Elimu.

Hatua za usajili wa shule

Mwongozo umetaja hatua tatu za kufuata ili kukamilishwa usajili wa shule, ambazo ni kuanzisha shule (kujenga au kutumia majengo yaliyopo), kuthibitisha kuwa mmiliki na meneja wa shule pamoja na kusajili shule.

Kibali cha kuanzisha shule

Mwongozo huo unamtaka mwombaji kuandika barua kuomba kibali kwa Kamishna wa Elimu na atatakiwa kuzingatia suala la elimu jumuishi ili kutoa fursa ya elimu kwa kila Mtanzania.

Miundombinu muhimu inayohitajika

Mwongozo huo wa uanzishaji na usajili wa shule unaelekeza kwamba ili shule ya kutwa isajiliwe inapaswa kuwa na miundombinu muhimu kwa kiwango cha chini kinachokubalika kwa ajili ya kuanzisha shule ya kutwa yenye mkondo mmoja.

Miundombinu hiyo inayohitajika katika shule ya Kutwa ya kidato cha kwanza hadi cha nne  (1-1V) ni vyumba vya madarasa 4,  Jengo la Utawala 1,Jiko 1, Ofisi 3, Maktaba 1, Bwalo 1, Maabara 3 kwa shule za sekondari,

Miundombinu mingine ni Vyoo vya Watumishi walimu na wasio walimu matundu 2, matundu 4 ya choo cha wasichana na matundu 4 ya choo cha wavulana, viwanja vya muchezo, huduma ya maji ya uhakika na chumba maalum 1 kwa ajili ya wasichana .


Imeelezwa kuwa pamoja na miundombinu iliyotajwa, uzio kuzunguka shule ni muhimu kwa ajili ya usalama wa wanafunzi na watumishi.

Pia kwa shule za Bweni mwombaji atatakiwa kuwa na miundombinu iliyotajwa kwa shule ya kutwa pamoja na mabweni, chumba cha matroni na patroni kulingana na jinsi, mabafu na vyoo vya bweni, sehemu ya kufulia na kuanikia nguo na mwanga wa uhakika.

Kibali cha kutoa huduma ya bweni kitatolewa kwa kulaza wanafunzi kuanzia darasa la tano na kuendelea.

Mwongozo huo umeelekeza ukubwa wa ardhi unaotakiwa ili kuanzisha shule, unatokana na mahitaji ya ngazi ya shule husika (Awali, Msingi, Sekondari na Chuo cha ualimu)

Hitaji la ukubwa wa eneo/ardhi kwa shule yenye mkono mmoja litanzingatia vipimo vya kiuhandisi vya majengo, viwanja vya muchezo na eneo la wazi. Kuongezeka kwa eneo/ardhi la shule kutategemea na ongezeko la mikondo.

Utaratibu wa kuwa mmiliki wa shule

Mwongozo unaeleza kuwa uthibitisho wa umiliki wa shule utatolewa kwa Shirika/ Jumuiya/Taasisi au mtu binafsi anayemiliki ardhi. Mmiliki wa shule ataomba uthibitisho wa yeye mwenyewe kuwa Meneja wa shule au kumwombea uthibitisho wa umeneja mtu mwingine.

Uthibitisho wa umiliki wa Shule

Mwongozo unaelekeza kwamba uthibitisho wa umiliki wa shule, mwombaji ataandika barua kwa Kamishna wa Elimu kupitia kwa Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule wa Halmashauri husika ambapo itaambatanishwa na barua iliyopitishwa na Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule wa Halmashauri.

Pia taarifa za ukaguzi wa shule kutoka kwa Mhandisu Ujenzi, Afisa afya na Mthibiti ubora. Kamishna wa Elimu atamthibitisha mmiliki kwa barua.

Mwongozo unaeleza udahili wa wanafunzi ufanyike mara baada ya mchakato wa usajili wa shule kukamilika.

Utaratibu wa kuthibitisha kuwa Meneja
Mwongozo unaelekeza kuwa mwombaji ataandika barua kwa Kamishna wa Elimu kupitia kwa Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule wa Halmashauri husika.

Imeelezwa kuwa barua ya maombi itaambatanishwa na nyaraka ambazo ni fomu iliyopitishwa na Mthibiti ubora, Cheti cha taaluma ya uongozi katika elimu kutoka chuo chochote kinachotambuliwa, na serikali, wasifu binafsi wa mhusika. Kamishna wa Elimu atamthibitisha Meneja kwa barua.

Kusajili Shule

Usajili wa shule ni hatua ya mwisho katika taratibu za usajili wa shule.Mwombaji aliyepewa barua na Kamishna wa Elimu kwa hatua ya kwanza na ya pili ndiye atakayewasilisha maombi ya usajili.

Mwongozo unaelekeza kwamba usajili utatolewa kwa mwombaji aliyekamilisha hatua ya kwanza na ya pili. Hata hivyo pamoja na kutimiza hatua ya kwanza na ya pili mwombaji atatakiwa kuwa na samani za kutosha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na ikama ya watumishi.

Utaratibu wa kuomba kusajili shule
Imeelezwa kuwa mwombaji ataandika barua kwa Kamishna wa Elimu kupitia kwa Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule wa Kanda husika.

Barua ya maombi itaambatanishwa na nyaraka zifuatazo;Fomu  namba US4(Kiambatanisho namba 5) iliyojazwa na kusainiwa na Mthibiti Mkuu Ubora wa Shule Kanda husika.

Mikataba ya ajira kwa watumishi wakiwemo walimu na wasio walimu izingatie uwiano wa kijinsia hasa kwa shule mchanganyiko na taarifa ya ukaguzi wa shule kutoka Kanda husika.

Kamishna wa Elimu atatoa barua yenye kuonesha namba ya usajili, aina ya shule, na idadi ya mikondo. Vilevile itaonesha kama shule ni ya kutwa/bweni ,mchanganyiko au ya jinsi moja.

Mwongozo unaelekeza kwamba ili mmiliki wa shule aweze kuongeza Mikondo atatakiwa kuandika barua kwa Kamishna wa Elimu kupitia kwa Mthibiti Mkuu wa Ubora wa shule Kanda na barua itaambatanishwa na taarifa ya ukaguzi kutoka kwa Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule Kanda.


Afisa Elimu afunguka

AFISA Elimu Halmashuri ya Wilaya ya Tarime, Vanance Babukege amesema wananchi wanatakiwa kushiriki katika maendeleo kwenye shule yao ukiwemo ujenzi wa madarasa, viti, meza na kwamba malumbano katika Kata hiyo yamesababisha shule kutokamilika.

"Nina miezi saba huu ni wa nane tangu nihamie Tarime, nilichokiona huku ni ubinafsi wanajenga shule nyingi  hawaziendelezi kitu ambacho ni shida, ukiwashauri fanya hivi wao wanafanya vile.

" Kila koo inataka iwe na shule yao, matokeo yake shule inakuwa na wanafunzi wachache wakati huo zikihitaji walimu, fedha za uhamisho ni changamoto na bado hawaendelezi ujenzi wa shule," anasema.

Afisa huyo wa Elimu anawahamasisha wananchi kuendelea kuchangia maendeleo ya shule na sio kujenga madarasa wakati shule inapoanzishwa tu hivyo ujenzi wa madarasa na vyumba za walimu unatakiwa kuwa endelevu kwakuwa Serikali imekuwa ikisaidia kukamilisha maboma na ujenzi wa madarasa unaokwenda sambamba na viti na meza.








No comments