HEADER AD

HEADER AD

KAIRUKI: WANAFUNZI TOENI TAARIFA ZA UKATILI WA KIJINSIA SHULENI

Na Daniel Limbe, Kibaha

WANAFUNZI nchini wametakiwa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia wawapo shuleni ili hatua za kisheria zichukuliwe haraka badala ya kuficha na kuishi na msongo wa mawazo.

Kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza wimbi la ukatili huo shuleni na kwenye jamii wanazoishi watoto hao na kuwa na jamii yenye ustawi bora kwa maendeleo ya nchi.

Hayo yamesemwa Januari, 10, 2023 na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Angellah Kairuki, alipotembelea shule ya sekondari Sofu iliyopo Kibaha mkoani Pwani kisha kuzungumza na walimu na wanafunzi waliojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023.

     Waziri wa Tamisemi,Angellah Kairuki,akizungumza na wanafunzi wa kidato cha kwanza Sofu sekondari.

"Ninawasihi msome sana na ukiona kwa namna yoyote mtu anakushinikiza kuacha masomo, au unafanyiwa ukatili majumbani au kuna mwalimu hapa anakufanyia ukatili wa kimwili, kijinsia, kiakili, kisaikolijia au kingono toa taarifa kwa mkuu wa shule.

"Ikitokea ukaona hujapata msaada hapa shuleni ulizia taratibu zilipo ofisi za mkuu wa wilaya, ukiulizwa unamtaka wa nini waambie kuna mzazi wangu anataka kuongea naye, serikali yenu ipo imara na itaendelea kuwalinda ili msome hadi vyuo vikuu".

     Wanafunzi wakiwasikiliza viongozi

"Pia ninaamini walimu mtakuwa mmeshawapitisha kwenye elimu hiyo kabla ya kuanza masomo" amesema Kairuki.

Ameiasa jamii kujikita kwenye ujenzi wa shule za ghorofa badala ya ujenzi wa kutawanya majengo ambao umekuwa ukitumia eneo kubwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya diwani wa kata ya Sofu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Kibaha, Mussa Ndomba kumweleza waziri kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maeneo ya ujenzi wa shule.

Pia na huduma za afya, jambo ambalo serikali inapaswa kusaidia upatikanaji wa maeneo hayo kutoka kwa baadhi ya mashirika ikiwemo lile la elimu Kibaha.

           Watatu kulia ni Diwani wa Kata ya Sofu,Mussa Ndomba,akitoa maelezo kwa Waziri wa Tamisemi

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewataka wazazi kundelea kufuatilia maendeleo ya watoto wao majumbani ikiwa ni pamoja na kukagua madaftari ya wanafunzi hao badala ya kuwaachia kazi hiyo walimu.

     Wa tatu kulia ni Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, akiwaasa walimu,wazazi na wanafunzi.

"Niwatake wazazi kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao, wewe hata kama hujui kusoma unashindwaje kujua hii ni kosa na hii vema, alihoji Kunenge.

Ofisa Elimu Sekondari, Halmashauri ya mji Kibaha, Rosemary Msasi, mbali na kuipongeza serikali kwa jitihada kubwa za ujenzi wa miundo mbinu ya shule kwenye kata hiyo.

Amesema awali wanafunzi hao walikuwa wakitembea umbari mrefu kwenda sekondari ya Pangani, Picha ya ndege na nyumbu jambo lililokuwa likisababisha kuota vigimbi kwenye miguu yao.

                       



No comments