HEADER AD

HEADER AD

MBUNGE WAITARA, DIWANI GIBAI WATUMIA WDC KUMJADILI MWENYEKITI CCM



>>>Wamuhoji kwanini alizungumza  kwenye Vyombo vya Habari

>>>Kwamba yalipaswa kuzungumzwa kwenye vikao vya ndani tu.

MBUNGE wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara na Diwani wa Kata ya Manga Steven Gibai wanadaiwa kutumia kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata(WDC) kumjadili na kumgombeza Mwenyekiti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Manga Samwel Mseti kisa Kuongea na Waandishi wa Habari kuelezea changamoto za shule na Zahanati.

Viongozi hao wanadaiwa kutumia kikao  cha WDC cha Januari, 10, 2023 katika ofisi ya Kata ya Manga ambapo walimtaka Mwenyekiti huyo kuwaeleza kwanini alienda katika shule ya Sekondari Bukenye na Zahanati ya Biswari akiwa na Waandishi wa Habari na habari hizo kurushwa kwenye vyombo vya Habari zilizohusu changamoto ya shule na Zahanati.

Kwamba kitendo hicho ni kuichafua Serikali ya CCM na nikuwapa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupata hoja za kusemea, licha ya kwamba Kata hiyo ina wakazi ambao ni wanachama wa CHADEMA ambao nao wanazifahamu changamoto za Shule na Zahanati.

Habari zinasema Mwenyekiti wa CCM Kata alikuwa na kikao chake cha Kamati ya Siasa katika ofisi ya Kata cha makabidhiano ya uongozi.Wakiwa wanasubiri wajumbe wengine ili wafike waanze kikao ghafla mida ya saa sita mchana Mbunge akiwa ameongozana na Katibu wake, Diwani, Wajumbe wa WDC ,wakiwemo Wenyeviti wa vijiji, Watendaji wa Vijiji,Wataalam ngazi ya Kata na baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya shule waliingia ndani ya ofisi wakitokea Bukenye Sec.

               Ofisi ya Kata ya Manga

Habari zinasema kwamba walipofika waliwaomba viongozi hao wa Chama kuwaacha waendelee na kikao cha WDC cha kujadili maendeleo wakati huo  wakisubiri wajumbe wao.

Imeelezwa kuwa Mtendaji wa Kata ya Manga Olita Masatu alisimama na kusema kikao ni cha WDC cha kujadili maendeleo.Wakati viongozi hao wa Chama cha CCM wanataka kuondoka ili kupisha kikao cha WDC, viongozi hao waliwaomba wabaki wasikilize kwakuwa Serikali ni ya CCM si vibaya wakisikiliza.

Hata hivyo inaelezwa kuwa hakuna hoja zilizozungumzwa zaidi ya kumshambulia Mwenyekiti wa CCM wakimlaumu kuongea kero za shule na Zahanati kwenye Vyombo vya Habari.

Mbunge, Diwani wahoji nani aliyeruhusu watu kufika shuleni

Habari zinasema kwamba Diwani wa Kata ya Manga-Tarime, Steven Gibai  alisimama kufungua kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ambapo alisema kwamba kuna mambo yapo mitandaoni ya kumshtumu yeye Diwani kuwa amegomesha maendeleo ya Manga na kwamba wale watu waliokuwa kwenye taasisi yao ni wapuuzi na wajinga.

          Diwani Kata ya Manga Steven Gibai

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Diwani huyo alimtaka mkuu wa shule hiyo Rejina Everest kumweleza ni nani aliyeruhusu watu kufika shuleni, mkuu huyo alisema kwamba yeye aliambiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya shule kuwa kuna wageni wanakuja ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Kata anafuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM na kujua changamoto za shule ili zifanyiwe kazi.

Hata hivyo inaelezwa kuwa Diwani Gibai aliendelea kumuhoji mkuu wa shule kuwa nani aliyetoa kibali cha wao kuja shuleni akimaanisha Waandishi wa Habari, mkuu huyo alisema ni Mwenyekiti wa CCM kama alivyoambiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya shule.

Imeelezwa kuwa baadhi ya wajumbe wa kikao hicho walimgombeza Mwenyekiti  kwa kuwatuhumu kupitia Vyombo vya Habari kuwa Vijiji vyao vimegoma kufanya maendeleo ya ujenzi wa shule.

Habari zinasema kuwa Mbunge Waitara aliposimama kuzungumza hakuzungumzia maendeleo bali aliomba Kanuni na Katiba ya Chama cha CCM na kuisoma kisha akasema kiongozi yeyote atakayetumia vibaya madaraka yake atakosa sifa na kufukuzwa nafasi aliyonayo na kwamba viongozi wasiovumilia wanadhani ni kiongozi wa chama kumbe ni wa upinzani huyo anakosa sifa na kuondolewa madarakani.

          Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara.

Inadaiwa kuwa Mbunge huyo alimtupia lawama Mwenyekiti huyo kwa kitendo cha kuongea kupitia mitandao katika Vyombo vya Habari huku akisisitiza kuwa yalikuwa yakujadiliwa katika vikao vya ndani.

Wajumbe wengine walisema hakupaswa kuzungumza kwenye Vyombo vya Habari ilipaswa kuitana kwenye vikao na alifanya ziara bila kuongozana na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Kata. 

Mwenyekiti CCM asema yeye ni Kiongozi na alichokisema ni ukweli.

Imeelezwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Kata ya Manga Wilaya  ya Tarime Samweli Mseti alijitetea katika kikao hicho na kusema kuwa yeye ndiye aliyewaita Waandishi wa Habari kama Mwenyekiti wa Chama aliyeaminiwa na kuchaguliwa na wanachama hivyo aliamua kutembeleza Shule na Zahanati kujua changamoto zake.

     Mwenyekiti wa CCM Kata ya Manga Samwel Mseti

Habari zinasema Kiongozi huyo alisema changamoto alizozizungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu shule ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa, shule kutokuwa na Bendera ya Taifa na kibao cha shule;

Ukosefu wa jengo la utawala, Maabara, Dawa kusota kwenye Zahanati bila Zahanati kutoa huduma si za uongo ni za kweli na kwamba tayari zimeanza kushughulikiwa.

Imeelezwa kuwa kikao hicho kilichodumu kwa masaa matatu hakikuzungumzia hoja yoyote ya maendeleo isipokuwa kumjadili na kumshambulia kwa maneno yenye mlengo wa kuudhoofisha uongozi wa Mwenyekiti huku wengine wakidai ni chuki za uchaguzi kwakuwa Mwenyekiti huyo hakuwa chaguo la Diwani.

Je Sheria inasemaje kuhusu Wajumbe halali wa Kamati ya Maendeleo ya Kata WDC ?.

Je Mbunge ni Mjumbe wa WDC ?

Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), baadhi ya Walimu wa shule ya Sekondari Bukenye, baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya shule na Watendaji wa Vijiji,  imedaiwa kuwa baadhi yao walioshiriki kikao hicho hawakuwa wajumbe halali wa kikao.

Kwa mujibu wa wa kifungu cha 30 (2)cha Sheria namba 7 ya Mwaka 1982 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 6 ya mwaka 1999, uanzishwaji wa Kata huanza kwa Halmashauri kutuma maombi kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa ambaye ndiye mwenye madaraka ya kuanzisha Kata.




Kifungu cha 31 cha sheria namba 7 ya Mwaka 1982 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 6 ya mwaka 1999 ilianzishwa Kamati ya Maendeleo ya Kata kwa kila Kata yenye wajumbe ambao ni;

Diwani wa Kata ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata, Wenyeviti wa Vijiji vyote katika kata hiyo, Diwani wa viti maalumu mkazi wa kata husika, Watu walioteuliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata kutoka Mashirika yasiyo ya serikali (NgOs) au vikundi vya kiraia kama vile Wanawake, Vijana, Walemavu, n.k lakini hawatakuwa wapiga kura na Afisa Mtendaji wa Kata kama Katibu.

Sheria: Majukumu ya Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC)

Jukumu kubwa la Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ni kusimamia na kuratibu shughuli zote za maendeleo ya Vijiji au Mitaa na kuhakikisha kwamba Serikali za vijiji katika Kata husika zinatekelezwa ipasavyo.

Kifungu cha 32 (1) cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Namba 7 ya mwaka 1982 kama ilivyorekebishwa na Sheria namba 6 ya mwaka 1999 na kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Na.8 ya Mwaka 1982 kama ilivyorekebishwa na sheria Na. 6 ya Mwaka 1999, imetaja majukumu ya Kamati za Maendeleo za Kata (WDC) ambayo ni;

Kukuza uanzishaji na uendelezaji wa biashara na shughuli za ushirika katika Kata, uanzishaji wa kazi au shughuli yenye lengo la kuleta ustawi wa jamii wa kazi katika Kata, kusimamia na kuratibu utekelezaji wa miradi na programu za Halmashauri katika kata.

Kupanga na kuratibu shughuli na kutoa msaada na ushauri kwa wakazi walio katika Kata ambao wanajihusisha na shughuli yoyote au biashara (Hali ya aina yoyote), Kupendekeza kwa utungaji wa Sheria ndogo, kufuatilia ukusanyaji wa mapato ya Halmshauri.

 Kuanzisha na kuendeleza ushirikishwaji wa wananchi katika maendeleo ya Kata, kusimamia mifuko yote ya fedha iliyoanzishwa na kukabidhiwa kwa kata na kusimamia maafa na shughuli zinazohusu mazingira na kuendeleza masuala ya kijinsia.

Ilani ya Uchaguzi ya CCM

Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025  Ibara ya 10 inasema CCM itahakikisha Serikali zake zinatekeleza mambo yote yaliyoahidiwa katika Ilani hiyo kwa manufaa na ustawi wa Taifa.

        Ilani ya Uchaguzi ya CCM

Utekelezaji wa Ilani hiyo utaongozwa na kauli mbiu isemayo " Tumetekeleza kwa kishindo; Tunasonga mbele pamoja.

Ibara ya 11 inasema Ilani hiyo ni tamko na ahadi maalum ya nia inayodhihirisha uwezo wa CCM kuendelea kuongoza nchi, kuleta ustawi wa Watanzania wote na kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi,hususani wanawake,vijana, watoto,wazee,pamoja na watu wenye ulemavu.Katika miaka 5 ya CCM itahakikisha matarajio ya wananchi katika nyanja zote yanafikiwa.

 Ibara ya 83 inasema lengo la Chama ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya njema ili kuwezesha kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Taifa na kuboresha maisha yao.

Ilani inaeleza kwamba Chama kitaisimamia Serikali katika kutekeleza ikiwa ni pamoja na (a) kuimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto na kuzitoa bila malipo ili kupunguza vifo vya akinamama, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka 5.

(b) Kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma ya afya ili viweze kutoa huduma Bora zaidi kwa wananchi.

Katika kuhakikisha vituo vya kutolea huduma ya afya Ilani hiyo Ibara ya 81 imeeleza; (a) kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa sekta ya afya kwa kuhakikisha kuwa kila kituo cha afya au Zahanati inayojengwa inakuwa na nyumba za watumishi.

Katiba : Haki ya uhuru wa Mawazo

DIMA ONLINE ilipowasiliana na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara kumlalamikia Mwenyekiti wa CCM Kata ya Manga Samwel Mseti kutoa ushirikiano wa kihabari kwa waandishi wa habari wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa Zahanati ya Bisarwi na shule ya Sekondari Bukenye alisema yeye hakuzungumzia yaliyoandikwa huku akimtaka Mwandishi wa DIMA Online kutoingilia vikao vyake wala vya chama.

Diwani Gibai yeye akisema kuwa ameamua kukaa kimya kumwacha Mwandishi aendelee kuandika habari hadi atakapochoka.

Katiba

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Ibara ya 18 inasema kila mtu (a) anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake.

        Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania


(b) Anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; 

(c) Anao Uhuru wa kufanya Mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika Mawasiliano yake.

(d) Anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.

Vyombo vya Habari kupitia Waandishi wa Habari vina haki ya kutoa taarifa kwa wakati kuhusu matukio mbalimbali kwa maisha na shughuli za wananchi pia kuhusu masuala muhimu.

Kuripotiwa kwa changamoto za shule ya Sekondari Bukenye na Zahanati katika Kata ya Manga na maeneo mengine ni haki ya msingi kwa mijibu wa Katiba ya Nchi.

Hata hivyo Vyombo mbalimbali vya Habari kupitia Waandishi wa Habari vimekuwa vikiripoti habari mbalimbali za ziara ya Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara kama ilivyo kwa wabunge wengine.

Baadhi ya habari zinazoripotiwa  wakati wa ziara ya mbunge ni pamoja na habari za kutembelea miradi, changamoto za wananchi, ukosoaji wa baadhi ya viongozi ikiwemo habari iliyotikisa Bunge ya wananchi wanaopakana na hifadhi ya Taifa Serengiti kuuwawa hifadhini na zinginezo.

Pia Diwani wa Kata ya Manga Steven Gibai katika uongozi wake wa udiwani kwa miaka 12 kupitia vikao vya Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Tarime amekuwa akiwasilisha hoja mbalimbali zikiwemo na changamoto kama vile miradi kujengwa chini ya viwango.


No comments