RC KAGERA AWAHIMIZA WAKULIMA KUPANDA MITI YA MATUNDA
Na Alodia Dominick, Karagwe
MRADI wa uvunaji hewa ukaa kupitia upandaji miti unaogharimu zaidi ya Tsh.Milioni 700 umezinduliwa katika Kata ya Kamagambo wilayani Karagwe mkoani Kagera, zaidi ya wakulima milioni 1.5 wanatarajia kunufaika na mradi huo.
Mradi huo ambao unalenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi umezinduliwa Januari 13,2023 na Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mkurugenzi wa kampuni ya Karagwe Development and Relief Service (KADERES) Leonard Kachebonaho amesema mradi huo unatekelezwa na kampuni hiyo kwa ufadhili wa Banki ya Rabo ya nchini Uhoranzi .
Mkurugenzi wa kampuni ya Karagwe Development and Relief Service (KADERES) Leonard Kachebonaho aliyevaa suti ya Blue bahari akikabidhi mizinga ya nyuki kwa mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila ili naye aikabidhi kwa wafugaji nyuki.
Kachebonaho amesema mradi huo unalenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuzuia mmonyoko wa ardhi, kuongeza usalama wa chakula pamoja na utunzaji wa mazingira.
"Tulianza majaribio ya mradi huu na wakulima 2000 na mpaka sasa tayari wakulima 425 wameshanufaika, jumla Tsh. Milioni 703 zimepatikana na mgao wa fedha hizo kwa wakulima uko katika pesa tasilimu, mgao wa vifaa vya kuendeleza utunzaji wa mazingira na uvunaji hewa ukaa ikiwemo mizinga ya nyuki" Amesema Kachebonaho
Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila akihutubia katika hafla hiyo ya uzinduzi ametoa lai kwa wakulima kupanda miti mingi hasa ya matunda katika kipindi cha mradi huo.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila akikabidhi miche ya miti kwa wakulima wilayani Karagwe ambao watanufaika na mradi wa uvunaji hewa ukaa.
"Upandaji wa miti hii kusiwe kwa kuharibu kilimo cha kahawa kusiharibu ndizi kiwe kilimo mseto, pandeni miti ya matunda hapo mtakuwa mnavuna hewa ukaa mtapata fedha mtauza matunda kwahiyo msiishie kupanda miti ambayo baada ya hapo hamtapata ziada"Amesema Chalamila.
Mmoja wa wakulima ambaye ameanza kunufaika na mradi huo Theopil Kahatano amesema kuwa ameishaanza zoezi la upandaji miti na amepanda Miche ya miti ipatayo 100.
Mkuu wa mkoa Albert Chalamila anamkabidhi mche wa wilaya ya Karagwe mwalimu Juliet Binyura
Mradi wa uvunaji wa hewa ya Caboni kwa njia ya upandaji miti unalenga kusajili wakulima wapatao 1.5 milioni kwa kipindi chote cha mradi miaka 20.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila aliyevaa kanzu nyeupe akizindua mradi wa uvunaji hewa ukaa katika kata ya Kamagambo wilaya ya Karagwe lengo likiwa ni kupambana na tabianchi na wakulima milioni 1.5 wanatarajia kunufaika na mradi huo wa miaka 20.
Post a Comment