MWALIMU ALIYEMWADHIBU MWANAFUNZI ASIMAMISHWA KAZI
>>> Ni yule aliyeonekana kwenye Video Clip akimwadhibu mwanafunzi
>>>Mwanafunzi alionekana akichapwa viboko kwenye nyayo za miguu akiwa peku.
>>>Walimu waliokuwa wakicheka nao wasimamishwa kazi
Na Alodia Dominick, Kagera
MKUU wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila ametolea ufafanuzi juu ya video inayosambaa mitandaoni ikimwonesha Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kakanja wilaya ya Kyerwa mkoani humo Isaya Emmanuel akimwadhibu mwanafunzi kwa viboko kwenye nyayo za miguu akiwa peku.
Amesema tayari mwalimu huyo amechukuliwa hatua za kisheria kwa kushushwa cheo na kusimamishwa kazi na baada ya uchunguzi kukamilika atafikishwa mahakamani.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa ufafanuzi huo Januari 25,2023 wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya tukio hilo ambalo limetokea Januari 10,2023 siku moja baada ya muhula wa masomo kufunguliwa.
Rc Kagera
Chalamila amesema kuwa, richa ya kumchukulia hatua mwalimu mkuu huyo pia walimu wanne waliokuwa ofisini hapo wamechukuliwa hatua za kusimamishwa kazi kwa kutomshauri mwalimu mkuu juu ya adhabu aliyokuwa akitoa kwa wanafunzi wawili wa darasa la nne ambao ni Salmon Kakwezi miaka tisa na Anord Kweyamba miaka (10) ambao richa ya kumuomba msamaha lakini hakuweza kuwasamehe na walimu hao walikuwa wakicheka na kufurahi.
“Walimu ambao walikuwa pembeni wakicheka au kufurahia wakati mwalimu Emmanuel akichapa viboko walikuwa wanne ambao ni Godson Rwamwisho, Beatrice Osward, Jemsi Josia na Delifina Leonsi wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tukio lililofanyika kutokana na kutomshauri mwalimu huyo juu ya adhabu alizokuwa akitoa kwa wanafunzi hao” Amesema Chalamila.
Ameeleza sababu ya mwalimu huyo kuwapa adhabu wanafunzi hao ni kukataa kufanya zoezi/maswali waliyopewa wayafanyie nyumbani wakati wa likizo hivyo akawapa adhabu kwa kuwachapa viboko kwenye nyayo za miguu huku akiwa amewakanyanga miguu yao.
Mmoja wa wazazi Fulgence Kosmas amelaani kitendo cha mwalimu huyo cha kwachapa viboko wanafunzi katika nyayo za miguu yao na kusema kuwa huenda hiyo ikawa sababu ya baadhi ya wanafunzi kukataa kuendelea na masomo yao na hivyo kuwa watoro.
Emiliana Michael amesema utoaji huo wa adhabu kwa wanafunzi ni ukiukwaji wa haki za watoto hivyo mwalimu huyo anastahili apate adhabu nje ya adhabu alizopewa na wakuu wake wa kazi ili na walimu wengine wenye tabia ya kutoa adhabu zisizostakiwa kwa wanafunzi waache tabia hiyo.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema tayari wameshafuatilia na mwalimu huyo amesimamishwa kazi na kwamba uchunguzi unaendelea na hatua stahiki zimechukuliwa dhidi yake na kwa sasa hayupo kazini.
Post a Comment