RHOBI SAMWEL AWANYOOSHEA KIDOLE VIONGOZI, WANASIASA KUHUSU UKEKETAJI
Na Jovina Massano, Serengeti.
VIONGOZI na Wanasiasa mkoani Mara wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto haswa katika suala la ukeketaji ambalo bado linaendelea.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Shirika la Matumaini kwa Wasichana na Wanawake Tanzania Rhobi Samweli alipokuwa akiwasilisha taarifa kwa Mkuu wa mkoa huo Meja Jenerali Suleiman Mzee hivi karibuni Januari, 10,2023 wakati wa ziara yake ya kutembelea mashirika yanayohudumia wahanga wa ukatili.
Amesema sababu zinazosababisha hali ya ukeketaji kutopungua licha ya elimu kutolewa na hamasa za kuokoa watoto kuja kwenye nyumba salama ni wanasiasa kuendelea kuhamasisha vitendo vya ukeketaji kwa madai ya kuwa wananchi ni wapiga kura wao hivyo hawataki kuwakasirisa
Aliyesimama ni Mkurugenzi wa Shirika la Matumaini kwa Wasichana na Wanawake Tanzania Rhobi Samwel aliyeketi ni Mkuu wa mkoa wa Mara, Suleiman Mzee
"Nina mfano mzuri tu mwezi August msimu wa sensa kupitia klabu za kupinga ukatili tulipokea taarifa kutoka kwa watoto16 kuwa walikuwa wanaandaliwa kwenda kufanyiwa ukeketaji, ila kupitia Dawati la jinsia na Ustawi wa jamii walikwenda kuokoa watoto hao,matokeo yake wazazi kwa kushirikiana na Diwani wa Kata walihamasishana na kudai kuwa watoto wao wametekwa.
"Walikwenda ofisi ya mkuu wa wilaya ya Serengeti kulalamika mkuu huyo alifuatilia ndipo akabaini kuwa watoto wamehifadhiwa nyumba salama kwa kujiridhisha alifika nyumbani hapo akaongea na watoto hao nao walieleza hali halisi namna wazazi wao walivyokuwa wamejipanga kutekeleza adhma ya kuwakeketa ndipo mkuu aliwaeleza wazazi wa watoto hao hawatawachukua mpaka msimu wa ukeketaji utakapokwisha". amesema Rhobi.
Ameongeza kuwa watoto waliokimbia ukeketaji katika msimu wa ukeketaji na kupokelewa katika nyumba salama ya Mugumu-Serengeti August-Desemba ni 105 lakini mwezi September shule zilipofunguliwa walezi wa nyumba salama walijenga mahusiano na wazazi hivyo watoto 33 walipokelewa na familia zao na 72 wamebaki.
Meja Jenerali Suleiman Mzee amesema kuwa hajaona wala kusikia viongozi wa mkoa huo wakipinga suala la ukeketaji hivyo haoni haja ya kuendelea kutoa elimu kwa kuwa imeshatolewa sana lakini hakuna mabadiliko kilichopo ni ubabaishaji tu wa kusema elimu Iendelee kutolewa.
Amesema hivi sasa ni sheria kuchukua mkondo wake kwa kuwapa adhabu ya ukatili kama ilivyo, amevitaka vyombo vya usalama vifanye kazi yake kuhakikisha vinawakamata wote wanaohusika.
"Nilitoa maagizo ya kupinga suala la ukeketaji mwezi Decemba wakati wa kutoa zawadi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu kwa ajili ya sherehe za Christmas na Mwaka mpya katika nyumba salama ya Masanga wilayani Tarime.
"Inasikitisha kuona maagizo yanavyotolewa na viongozi wa Serikali hayapewi umuhimu wala uzito kwa kuwa wamekaidi nguvu yangu nitaielekeza kwenye kuchukua hatua kwa wazazi na viongozi wa maeneo yao"amesema Suleiman.
Ameongeza kusema wapo viongozi na wanasiasa ambao hawaungi mkono jitihada za serikali za kupinga ukatili huo na hakuna walio gerezani kwa kosa la ukeketaji.
Amesisitiza kuachana na suala la utolewaji wa elimu na kusema kuwa ni ubabaishaji tu wa kutumia fedha vibaya na kwamba hatua za kukomesha ukatili huo usiendelee ni kuwaweka jela ndio itakuwa njia sahihi ya kuelewa elimu ya ukeketaji.
Shirika lina nyumba salama 2 wilayani Serengeti na wilayani Butiama ambazo zinatumika kuhifadhi wahanga wa ukatili na linafanya kazi kwa kushirikiana na Dawati la jinsia na Ustawi wa jamii.
Shirika linawawezesha wahanga kwa kuwapa elimu na kuwaendeleza ambapo wahanga 11 wapo shule za bweni na vyuo vikuu.
Post a Comment