HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA JAMII

Na E. Kayombo WAF - Dar es Salaam

JUMLA ya Vituo vya Afya 685 hapa nchini vimekarabatiwa vingine kujengwa na vituo 421 vimeanza kutoa huduma ya upasuaji wa mtoto tumboni.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Januari 15,2023 wakati  akifungua mkutano wa Afya ya Mwanamke Barani Afrika uliofanyika Jiji la Dar es Salaam.

Ummy amesema Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwenye afya ya Mama na Mtoto kwa kuboresha ubora wa Huduma hiyo na kuzisogeza karibu na wananchi.

           Waziri Ummy Mwalimu

“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu itaendelea kutoa kipaumbele na kutenga rasilimali fedha kwa ajili ya kuboresha huduma bora za jamii ikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto ili kuifanya jamii iwe na maisha bora ikiwa ni pamoja na kuwaondolea usumbufu wanawake katika kupata huduma hizo” amesema Waziri Ummy.

Amesema Serikali imeimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya ya msingi pamoja na kuongeza idadi ya vituo vya afya ambapo huduma za afya zinapatikana karibu na wananchi.

Katika kuimarisha huduma hizo za msingi amesema hospitali za Wilaya 102 zimejengwa na kukarabatiwa ili kuimarisha mifumo ya rufaa za matibabu pamoja na kusogeza karibu na wananchi huduma za kibingwa. 


“Katika kuondoa unyanyasaji wa mtoto wa kike, mwaka 2021 Dkt. Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Tanzania aliruhusu watoto wa kike walioacha masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua” amesema Waziri Ummy.

Waziri huyo amesema suala la mimba za utoto bado ni changamoto kubwa hapa nchini hivyo amewakata wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutilia mkazo suala la elimu ya afya ya uzazi ili waweze kujitambua na kujikinga dhidi ya mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa.

Waziri Ummy amesema sekta ya Afya inakabiliwa na uhaba wa asilimia 50 ya watumishi wa kada za afya, amewaomba wadau wa maendeleo ya sekta hiyo kushirikiana na Serikali katika kuziba pengo la watumishi wanaohitajika ili kutoa huduma katika kulinda afya ya mama na mtoto.


“Tunawaomba sana wadau humu ndani mnapoandaa maandiko yenu kwenda kwa wafadhili muweke na kipengele cha kusaidia watumishi kada za afya wakiwemo watumishi wa afya ngazi ya jamii wote wana mchango mkubwa katika kuhakikisha wanalinda afya ya mama na mtoto” amefafanua Waziri Ummy.

“Tunaamini kabisa tukimwekea mwanamke mazingira rafiki zaidi kwa ajili ya afya yake ataweza kushiriki katika uzalishaji mali, malezi na matunzo ya watoto lakini pia ataweza kushiriki katika kuimarisha afya yake” amesema Waziri Ummy.

No comments