HEADER AD

HEADER AD

ZAHANATI KUWAONDOLEA ADHA WANAKIJIJI KUFUATA HUDUMA KM 15


Na Annastazia Paul, Bariadi

WAKAZI wa Kijiji cha Chungu cha Bawawa kilichopo kata ya Nkololo wilayani Bariadi mkoani Simiyu wameeleeza kufurahishwa kwao na ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho ambayo wamesema itawapunguzia adha ya kwenda umbali mrefu takribani kilomita 15 kwa ajili ya kupata huduma za afya.

Wananchi wa kijiji hicho wamesema kwamba wagonjwa na akina mama wajawazito walikuwa wakiteseka kufuata mbali huduma ya afya na kwamba uwepo wa zahanati hiyo utakuwa ni mkombozi kwao.

Zacharia Susanya amesema "Kwa ujenzi wa zahanati hii tutapunguza shida na umbali wa kumsogeza mgonjwa katika huduma hasa akinamama wajawazito ambao mara nyingi ndio wanapata shida nyakati za usiku usafiri ni wa shida kufika eneo la huduma lakini jengo hili litakapoanza kutoa huduma mambo yatakuwa mazuri sana".

Mkazi wa Kijiji hicho Kasili Magagaa  ameiomba serikali kuleta wahudumu wa afya wa kutosha sambamba na dawa kwa ajili  ya wagonjwa watakaofika zahanati pindi itakapoanza kutoa huduma.

                   Zahanati ya Kijiji

 “Serikali ituletee watumishi wa kutosha kwenye zahanati yetu hii na dawa za kutosha ili huduma itolewe vizuri  na wananchi wanufaike na uwepo wa zahanati hii kijijini hapa.” Amesema Kasili.

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Balumbilwe Mashimba ameishukuru Serikali kwa kutoa Tsh. Milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ambayo kwa sasa inaelekea kukamilika.

            Zahanati ya Kijiji

“Sisi zahanati hii kwetu wana Chungu cha Bawawa ni mkombozi mkubwa sana kwasababu mama anaweza kujisikia akatembea tu kwa mguu kuja hapa kuliko ilivyokuwa hapo awali, kutoka Chungu cha Bawawa kwenda Nkololo ni kilomita 15 mama anayeumwa uchungu hawezi akafika kwa mguu mpaka usafiri.

"Hatuna barabara usafiri wenyewe mpaka utafute kwa shida, tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu kwa fedha alizotoa katika ujenzi wa zahanati hii, tunamuomba sasa aweze kutupatia wahudumu, tupate dawa za kutosha ili kusudi zahanati yetu iweze kufunguliwa mara moja na kuanza kutoa huduma.” Amesema Bulumbilwe Mashimba.

Diwani wa kata ya Nkololo Emmanual Nyawela ameeleza kufurahishwa kwake na ujenzi wa zahanati hiyo ambayo inatarajiwa kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange amesema kuwa madaktari na wauguzi wapo tayari kwa ajili ya kuhudumu katika zahanati hiyo mara tu itakapokamilika.

       Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange, (wa pili kulia).

“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu kwasababu tayari madaktari na manesi kwa ajili ya zahanati hii wamekwisha gawiwa kwa ajili ya kuja kuanza kutoa huduma katika zahanati hii itakapokamilika.” Amesema Kapange.

                                          

No comments