ASILIMIA 86 WAPATA DOZI KAMILI YA CHANJO YA UVIKO-19
Na E. Kayombo, WAF – Dodoma.
WIZARA ya Afya kwa kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Afya wamefanikisha utoaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 na kufikia asilimia 86 ya Watanzania wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea kupata dozi kamili ya chanjo dhidi ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Januari, 19, 2023 alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Afya kwa kipindi cha Mwezi Julai hadi Desemba 2022 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Jijini Dodoma.
“Ndani ya miezi sita tumefanya vizuri kwenye utoaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19, tumeweza kufikia asilimia 86 ya Watanzania wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea kupata dozi kamili ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 ukilinganisha asilimia 24.7 hadi kufikia mwezi Juni, 2022” amesema Waziri Ummy.
Amesema kuwa hadi kufikia Desemba 31, 2022 jumla ya dozi 46,848,520 zilikuwa zimepokelewa ambapo dozi 41,581,670 zilikuwa zimesambazwa nchi nzima huku kiasi cha chanjo zilizosalia kwenye bohari ya kutunzia chanjo ni 5,266,850 ambazo zote ni aina ya J.J.
Amesema Wizara ya Afya hivi karibuni itazindua ‘Booster’ dozi ya UVIKO-19 ili wananchi waweze kuongeza kinga zaidi dhidi ya ugonjwa huo na kusema kuwa ni hiari kwa mtu yeyote kwenda kupata chanjo hiyo.
Kuhusu huduma za chanjo kwa Watoto, Waziri Ummy amesema huduma hizo ziliendelea kutolewa kwa Watoto wa chini ya umri wa mwaka mmoja kwa chanjo ya Penta3 ambayo hutumika kama kipimo kikuu ilifikia asilimia 107 ukilinganisha na mwaka 2021 iliyofikiwa kwa asilimia 96” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya Ummy MwalimuAmesema Wizara ya Afya imefanikisha vyema Kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio ya matone OPV3 katika raundi zote nne kwa asilimia 103 ukilinganisha na asilimia 79 mwaka 2021, sindano (IPV) kwa asilimia 107 ikilinganishwa na asilimia 95 kwa mwaka 2021, Surua rubella dozi ya kwanza asilimia 109 ikilinganishwa na asilimia 92 kwa mwaka 2021, Surua Rubella dozi ya pili asilimia 96 ilinganishwa na asilimia 76 kwa mwaka 2021.
“Kwenye utoaji wa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana dozi ya kwanza (HPV1) tulifanikisha utoaji wa chanjo hiyo kwa asilimia 83 ikilinganisha asilimia78 kwa mwaka 2021 na chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana dozi ya pili (HPV2) asilimia 62 ukilinganisha na asilimia 61 kwa mwaka 2021” amesema Waziri Ummy Mwalimu kwenye taarifa aliyowasilisha kwa Kamati.
Waziri Ummy amesema kuwa Wizara imeendelea kuboresha huduma za afya mipakani na kuhakikisha kuwa magonjwa ambukizi yaliyopo katika nchi jirani hayaingii nchini.
“Tumefanya kazi kubwa ya usimamizi wa masuala ya afya mipakani kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauingii nchini, na habari njema tumesikia hivi karibuni nchi ya Uganda imetangaza kumaliza mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kwa hiyo na sisi tunaamini tupo salama” amesema Waziri Ummy.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Stanslaus Nyongo (Mbunge) ameipongeza Wizara ya Afya pamoja na Taasisi zake kwa kuendelea kusimamia vyema Sera ya Afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za Afya.
Nyongo ameishauri Wizara ya Afya kushirikiana vyema na Ofisi ya Rais Tawala za Mikao na Serikali za Mitaa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuhakikisha kuna usimamizi imara katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Post a Comment