BILIONI 38 KUONDOA ADHA YA MAJI CHATO MJI
Na Daniel Limbe, Chato
ZAIDI ya Bilioni 37.9 zinatarajiwa kuondoa adha ya maji kwa wakazi wa kata ya Chato, Bwina na Muungano wilayani Chato mkoani Geita na kwamba itasaidia kulinda afya za wananchi.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Chato, ambapo utajengwa kwa kipindi cha miezi 32 hadi kukamilika kwake.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji mjini Chato, Mali Misango, wakati akitoa ufafanuzi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo,ambapo amesema usanifu unaendelea ili kuhakikisha mradi huo unaanza mapema mwaka huu.
"Mradi huu utajengwa kwenye kijiji cha Buzirayombo na mkandarasi anayefahamika kama Afcon Infrastructure Ltd na Vijeta Projects and Infrastuctures Ltd kutoka jijini Dar es Salaam" amesema Misango.
Kadhalika mradi huo utajumuisha shughuli za ujenzi wa chujio (Treatiment Plant),matanki matatu yenye ujazo wa lita 2,000,000 litakalojengwa Ilyamchele,Lita 500,000 kijiji cha Buzirayombo na lile la lita 200,000 kwenye kijiji cha Katende.
"Ujenzi huo utachukua eneo lenye ukubwa wa ekari 70 ambapo wataalamu wa idara ya ardhi wanatarajia kuanza kufanya uthamini wa ardhi itakayoguswa na mradi huo kwa lengo la kulipa fidia"amesema.
Kukamilika kwa mradi huo utasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa maji pamoja na kero ya wananchi kutumia maji machafu, kutokana na mradi uliopo sasa kutokuwa na chujio.
Mbali na kupongeza hatua hiyo, baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo wakaomba mtandao wa maji uongezwe ili kusaidia wananchi wengi kunufaika na mradi huo mkubwa unaotekelezwa katika programu ya miji 28 nchini.
Post a Comment