HEADER AD

HEADER AD

CHADEMA : RC MARA ASIRUDIE TENA KUJA KUTISHA WANANCHI TARIME

Na Dinna Maningo, Tarime

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mara kimemuonya Mkuu wa mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee kufika Tarime na kuwatisha wananchi badala yake asikilize kero za wananchi na kuzitatua.

Wakizungumza kwenye mkutano wa Chama hicho uliofanyika Februari,17,2023 katika Kijiji cha Kegonga Kata ya Nyanungu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mara Lucus Ngoto amesema kuwa viongozi wa Serikali wasitishe wananchi bali watatue tatizo lililopo Kata ya Nyanungu.

Ngoto amesema Kata ya Nyanungu, Gorong'a na Kwihacha zina mgogoro wa mipaka kati ya wananchi na Hifadhi ya Serengeti ambao umesababisha baadhi ya wananchi kupotea, wengine kuuwawa kwa kupigwa risasi na kujeruhiwa na mifugo kukamatwa huku mingine ikiuwawa kwa risasi .

     Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA mkoa wa Mara, Lucus Ngoto Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Kegonga Kata ya Nyanungu

"Tumesikia wamekuja hapa viongozi wa Serikali wengine wanakuja kutisha wananchi, Serikali isije kutisha wananchi tunataka Serikali ije kutatua tatizo lililopo Nyanungu sio kutisha wananchi.

"Tumesikia juzi kati mkuu wa mkoa alikuja hapa anazungumza watu hawajibu, tunamtaka aje kutatua matatizo,Serikali ipo kwa ajili ya kutatua matatizo ya watu sio kwa ajili ya kutisha, vijana wamepotea hawajulikani walipo.

Ameongeza "Serikali haishtuki kwanini watu wamepotea watu wameenda wapi, jukumu la Serikali ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, kama kuna mgogoro Serikali njoo mkae na watu mtatue mgogoro uliopo watu waishi kwa amani,viongozi wasikilize vilio vya wananchi na wafanyie kazi."amesema Lucus.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya (CHADEMA) ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini 2015-2020, John Heche amemtaka mkuu huyo wa mkoa wa Mara asije Tarime kutisha watu na  kwamba hawatakubali hata mara moja kwakuwa wapo kwenye haki hawatashindwa.

    Mjumbe wa Kamati Kuu ya (CHADEMA) ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini 2015-2020, John Heche akizungumza na wananchi.

"Inakuwaje mtu anakuja kusema eti kule kwao ukimuuliza mtu mara tatu kanyamaza hapo amekubali? anawezaje kuja hapa kusema mambo ambayo ni ya kuzungumzia huko kwenye stendi, asije akarudia tena siku nyingine, asirudie tena.

"Mkuu wa mkoa anakuja hapa hasikilizi wananchi, hawa wananchi sio wajinga wana akili wanaweza kuchangia wazo, watu wanadharau watu wakijua hawajui chochote kila utakachowaambia watakubali, kama ana heshimu wananchi atawasikiliza mnasemaje nyie mliozaliwa hapa mpaka ni upi na nyie mnachangia mawazo.

"Kwamba sisi tunajua mpaka ni huu mnakubaliana mpaka usogezwe wapi, yeye anakuja kusema mpaka lazima uwekwe hapa! watu wanauwawa mkuu wa mkoa anakuja kutisha watu, huu mgogoro umewashinda viongozi wa mkoa wa Mara waje viongozi wa kitaifa wautatue "amesema John. 

Wananchi wamelalamika mkuu huyo wa mkoa kufika kijijini na kufanya mkutano lakini hakutona nafasi kwa wananchi kuuliza maswali na kueleza kero zao.

Nchangwa mganya mwanamke aliyezungumza kwa ujasili mkubwa amesema " Eti anakuja mtu akiwa kama Serikali anakataa eti maswali hayawezi kuulizwa, hivi ataongeaje hadi amalize aondoke bila kuulizwa maswali?.

         Nchangwa Mganya akieleza kero 

"Hivi mtu unaweza kwenda kwenye mji wa mtu uongee vizuri umalize uondoke hujaulizwa swali ulichokifuata au kusema jambo lililokuleta kuwa nitawasaidia hivi, watu wanakuja hapa wanatudanganya kuwa haya maneno yenu yatasikilizwa alafu tunashtukia wanakuja wanaburuza watu na kupelekwa hifadhini hatujui wapo hai au hawapo.

"Mpaka umesogezwa hadi kwenye makazi ya watu hadi kwa Mwita Oghagha, ukienda kuchota maji au kunywesha mifugo unakamatwa, hata mtoto akienda kujisaidia ni hivi akamatwe, mimi nimeozesha mabinti watano lakini sina ng'ombe hata mmoja wa kulimia wamekamatwa na kupelekwa hifadhini wengine kupigwa risasi nikilala sipati usingizi "amesema Nchagwa.

Ameongeza kuwa wamechoka na vitendo vya unyanyasaji na kwamba wanapata mateso kwakuwa hawana mtu wa kuwatetea na anaye jaribu kutetea Serikali huwakamata.

      Wananchi Kata ya Nyanungu wakisikiliza viongozi wa CHADEMA

         Viongozi wa CHADEMA

No comments