MBUNGE MATHAYO : FEDHA MFUKO WA JIMBO ZITAFUNGUA BARABARA KM.32
Na Jovina Massano, Musoma.
MBUNGE wa Jimbo la Musoma mjini Mkoani Mara Vedastus Mathayo amesema fedha za mfuko wa jimbo zaidi ya Tsh Milioni 59 zinatarajia kufungua barabara zipatazo 211 kwenye Kata 10 zenye urefu wa kilometa 32 kulingana na tathimini ya ufunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amewaeleza kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Manispaa ya Musoma imepokea kiasi cha Tsh. 59,981,000 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
" Fedha za mfuko wa Jimbo ni fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuchochea maendeleo, kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi kwa wananchi tumeona ni vema zifunguliwe ili TARURA waweze kuziendeleza na ziweze kupitika
" Awamu hii mimi pamoja na wajumbe wangu wa kamati tumekubaliana kwamba kwa kuwa wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) haijihusishi na ufunguaji wa barabara mpya tumeona tuzifungue kwa fedha za mfuko wa Jimbo " amesema Vedastus.
Amefafanua kuwa katika mradi huo hautaenda sambamba na mitaro kwa kuwa barabara ndio zinafunguliwa kitakachofanyika ni kuondoa mawe, kukata miti na vizuizi vyote vinavyozuia barabara.
"Baada ya hapo Greda zitapita zimetambulika zote zitakuwa na majina baada ya kufunguliwa zitaendelezwa na TARURA kwa kuwekewa mitaro hata lami kwa kuzingatia utaratibu wao kulingana na bajeti.
"Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuongeza kiasi cha fedha kwani awamu zilizopita Jimbo lilikuwa likipokea kiasi cha Tsh. 36,600,000 hivi sasa imeongezeka hadi kufikia Tsh.59,981,000.
Amesema Kata zinazotarajiwa kunufaika ni Bweri Km 3, Rwamlimi Km 4, Mshikamano Km 3,Kwangwa km 3,Buhare Km 3, Mwisenge Km3,Kigera Km3,Makoko Km3, Nyakato Km 4, na Nyamatare Km 3.
Mjumbe wa Mfuko huo Haji Mtete ambae pia ni Diwani wa Kata ya Nyasho amesema ufunguzi wa Barabara mpya utashirikisha viongozi wa Kata husika kwa kushirikiana na wajumbe wa kamati.
"Kama tulivyokubaliana na Mwenyekiti wetu kuwashirikisha viongozi wa Kata husika kwa maana ya Diwani na watendaji wa Kata na mitaa akiwemo na Mhandisi wa Halmashauri lakini pia tutakuwa na mita ili kupata urefu halisi wa barabara ili kuepusha udanganyifu", amesema Haji.
Ameongeza kuwa usimamizi ukiwa mzuri fedha inaweza ikabaki na kusaidia kufungua barabara nyingine hasa kwenye Kata zenye uhitaji na za pembezoni na kwamba kabla ya mradi kuanza Viongozi na Madiwani watajulishwa kufika katika barabara hizo ili waweze kujua namna zoezi hilo litakavyofanyika katika maeneo yao.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mwisenge Mbogo Mnyugu amewaomba wajumbe hao kuwashirikisha Viongozi wa Chama wa Kata husika ili waone utekelezaji wa Ilani unavyofanyika na kuweza kutoa ushauri pia kwa kamati hiyo.
Post a Comment