UBAGUZI MIRADI YA MAENDELEO UNAVYODIDIMIZA BAADHI YA VIJIJI
>>>Kijiji cha Mtana chajizolea Milioni 552
>>>Kembwi yaambulia Milioni 90, Bisarwi yajikongoja kwa Milioni 31
>>>Mwaka jana upande wa Afya Mtana ilipata fedha Tsh. Milioni 690
Na Dinna Maningo, Tarime
BAADHI ya Kata zimekuwa na ubaguzi na upendeleo katika fedha za utekelezaji wa miradi kwenye vijiji kwani vipo vijiji vimeonekana kutengewa fedha nyingi huku vijiji vingine vikiambulia fedha kidogo.
Halmashauri zikiwa ndio mama na mlezi wa Vijiji lakini zimeshindwa kusimamia vyema mgawanyo wa miradi kwenye vijiji ili kuwa na uwiano sana wa utekelezaji wa miradi ngazi za vijiji na mitaa.
Hali hiyo imesababisha vijiji vingine kubaki nyuma kimaendeleo huku baadhi ya vijiji vikiongoza kuwa na miradi mingi vikiwemo vile wanakotoka Madiwani.
KIJIJI cha Mtana anachotoka Diwani wa Kata ya Manga Steven Gibai kimeonekana kupata fedha nyingi za miradi ikilinganishwa na vijiji vingine vya Kata hiyo.
DIMA Online imebaini kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, imepeleka miradi katika Kata hiyo yenye vijiji vitatu ambavyo ni Mtana, Bisarwi na Kembwi huku kijiji cha Mtana kikizidi kujizolea miradi ya fedha nyingi.
Imebainika kuwa katika mwaka huo wa fedha, Kijiji cha Mtana kimepata miradi ya maendeleo itakayotekelezwa kwa fedha jumla Tsh. Milioni 552 kati ya fedha hizo Tsh. Milioni 17 zimepokelewa kukarabati vyumbe 4 vya madarasa.
Miradi hiyo ni ujenzi wa shule mpya ya Kata katika Kijiji cha Mtana kiasi cha Tsh Milioni 470 fedha bado hazijapokelewa chanzo cha fedha SEQUP, ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa shule ya msingi Abainano kiasi cha Tsh. Milioni 40, chanzo cha fedha EP4R fedha bado hazijapokelewa.
Ukarabati wa vyumba 4 vya madarasa shule ya msingi Abainano kiasi cha Tsh Milioni 17 kwa fedha za mapato ya ndani ambazo zimepokelewa na Tsh Milioni 25 za ununuzi vifaa tiba Zahanati ya Mtana fedha bado hazijapokelewa.
Kijiji cha Kembwi Tsh. Milioni 95 kati ya fedha hizo Tsh. Milioni 70 zimepokelewa ujenzi wa nyumba ya mganga na Kijiji cha Bisarwi Tsh.Milioni 31 ambazo zimepokelewa kwa ujenzi wa chumba 1 cha darasa na choo.
Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri hiyo ilipeleka miradi kwenye kata hiyo, Kijiji cha Mtana kimeonekana kuongoza kuwa na miradi iliyogharimu fedha nyingi ikilinganishwa na vijiji vingine.
Baadhi ya miradi iliyotekelezwa kwenye Kijiji cha Mtana kwa mwaka huo wa fedha, ni mradi wa ujenzi Kituo cha afya Mtana kilichojengwa kwa fedha kutoka Serikali kuu kiasi cha Tsh Milioni 500.
Ujenzi wa jengo la kufulia na njia za kupita wagonjwa Tsh Milioni 100 fedha kutoka Serikali kuu na Tsh Milioni 90 za ukamilishaji jengo la mama na mtoto na ujenzi wa njia za kupita wagonjwa ambazo ni fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo miradi hiyo mitatu imegharimu Tsh Milioni 690.
Kijiji cha Kembwi kimepata miradi yenye kiasi cha Tsh.Milioni 95, mradi wa ujenzi wa nyumba moja (2 in 1) ya mganga Zahanati ya Kijiji cha Kembwi kiasi cha Tsh Milioni 70 zimepokelewa, chanzo cha fedha CSR.
Kiasi cha Tsh.Milioni 25 za kuchimba kisima kirefu cha maji na kufunga pampu ya mkono katika Kijiji cha Kembwi ifikapo Juni, 2023, chanzo cha fedha Serikali kuu,fedha bado hazijapokelewa.
Kijiji cha Biswari nacho kimeambulia Tsh Milioni 31 kati ya fedha hizo ni Tsh. Milioni 20 ujenzi wa chumba kimoja cha darasa shule ya Sekondari Bukenye ifikapo mwezi Juni,2023, fedha zimepokelewa na chanzo cha fedha Serikali kuu.
Mradi mwingine ni kukamilisha ujenzi wa matundu 11 ya vyoo shule ya msingi Bisarwi ifikapo Juni, 2023 kiasi cha Tsh Milioni 11 unaojengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmshauri, fedha zimepokelewa.
Milioni 470 kujenga Sekondari Mtana ?
KATIKA kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara katika bajeti yake imepeleka mradi wa ujenzi wa shule mpya katika kijiji cha Mtana Kata ya Manga.
Mradi huo wa ujenzi utagharimu Tsh. Milioni 470 fedha kutoka SEQUP kwa ajili ya ujenzi wa shule ya kata katika kijiji hicho, fedha ambazo bado hazijapokelewa kutekeleza mradi.
Mradi huo umepelekwa kijiji cha Mtana licha ya kwamba kuna shule ya Sekondari Bukenye iliyopo Kijiji cha Bisarwi ambayo ilijengwa kama shule ya kata na inakabiliwa na changamoto nyingi.
Bukenye Sec ni shule changa iliyoanzishwa mwaka 2021, ina idadi ya wanafunzi wasiozidi 500. Shule hiyo ina kidato cha kwanza hadi cha tatu.
Wanafunzi 262 walichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule hiyo mwaka huu wa 2023, ina wanafunzi 139 wa kidato cha pili na wanafunzi 53 wa kidato cha tatu.
Shule ya Bukenye Sec inakabiliwa na changamoto nyingi kinyume na mwongozo wa mwaka 2020 uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wa uanzishaji shule na usajili wa shule za Serikali na binafsi kwa kutwa na Bweni .
Shule hiyo ina upungufu wa vyumba vya madasa, viti na meza, haina jengo la utawala, haina Maabara, Maktaba,chumba cha wasichana cha kujistili, nyumba za Walimu, Ofisi, umeme, maji, Bwalo na Jiko.
Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Tsh Milioni 20 zimepokelewa na kujengwa chumba kimoja cha darasa kwa fedha za Serikali kuu.
Januari, 3, 2023, DIMA Online iliripoti habari ya changamoto ya shule ya Bukenye Sec ambapo wananchi na viongozi walieleza sababu ya changamoto.
Post a Comment