HEADER AD

HEADER AD

CCM BUTIAMA ILIVYOMSIMAMISHA UONGOZI MWENYEKITI WA KIJIJI


Na Dinna Maningo, Butiama 

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Butiama, mkoa wa Mara kimesema kimemsimamisha uongozi Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga Kata ya Mirwa Magige Mahera Msyomi ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma saba zinazomkabili zilizowasilishwa na chama hicho ngazi ya Kata.

Novemba, 10,2022 Chama hicho kupitia Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Mkaruka Hamis Kura kilimwandikia barua ya kumsimamisha uongozi wa uenyekiti wa kijiji ambapo alieleza kuwa alipokea barua ya tuhuma kutoka halmashauri kuu ya Kata ya Mirwa wakimtuhumu kwa mambo yafuatayo;

       Katibu wa CCM Wilaya ya Butiama, Mkaruka Hamis Kura

Tuhuma hizo ni kutosoma mapato na matumizi ya Kijiji, kukwamisha ujenzi wa choo, kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari, kuchukua matofali 500 ya Chama na mawe ya umoja wa vijana Kata na kutumia kwa manufaa yake bila ridhaa yao.

Kuchukua fedha ya mwananchi ya maji Tsh.367,000 bila kutoa stakabadhi na kufanyia shughuli zake. Pia amefungwa kifungo cha nje kwa kesi ya jinai Na. 6/2020 ZANAKI na kukatalia kwenye eneo la Serikali (Daire) na kufanya makazi.

Katibu huyo wa CCM kupitia barua hiyo anaeleza "Kwa hoja hizo saba nakubaliana na uongozi wa Kata kwa kukusimamisha uongozi ili kupisha uchunguzi. Pia nakupa nafasi ya kujibu tuhuma zako kwa maandishi kwa mujibu wa kanuni na Maadili  Ibara ya 7 kifungu cha 4 (i), tuhuma hizo uzijibu ndani ya siku saba kuanzia siku utakapopata barua hii" barua imeeleza.

Barua aliyoisaini na kugonga mhuri na Nakala kwenda kwa Katibu wa CCM Kata - asimamie uongozi hadi uchunguzi utakapokamilika, Mkuu wa wilaya - Tuma vyombo vya ulinzi na usalama vimchunguze, Katibu wa CCM mkoa wa Mara na Katibu mkuu chama cha Mapinduzi Dodoma. Magige Mahera alithibitisha kupokea barua hiyo tarehe Novemba,10,2022.

Hata hivyo Magige Mahera alipinga tuhuma hizo kama ilivyoripotiwa na chombo hiki cha habari Machi, 23,2023 na Mwandishi wetu wa habari aliyekuwepo Kijiji cha Magunga kwa siku kadhaa akifuatilia changamoto mbalimbali na sakata la Mwenyekiti huyo kusikamishwa uongozi na Chama chake cha CCM.

       Mwenyekiti wa Kijiji Cha Magunga Magige Mahera aliyesimamisha uenyekiti na Chama cha Mapinduzi

Februari, 22, 2023, Ofisi ya CCM Wilaya kupitia Katibu wake Mkaruka alimwandikia barua ya wito wa kuhudhulia kikao cha Kamati ya maadili tarehe 28, 02,2023, ,saa 04:00 asubuhi ofisi ya chama hicho wilaya na kumtaka afike bila kukosa.

Barua iliyosainiwa na kugongwa mhuri na Katibu huyo na Nakala kwa Katibu CCM Kata ya Mirwa kwa Taarifa, Katibu CCM mkoa wa Mara kwa taarifa na Katibu mkuu chama hicho Dodoma.

Akizungumza na Mwandishi wa Habari wa DIMA Online 
Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Butiama amesema kuwa, licha ya kupewa siku saba kujibu tuhuma zinazomkabili hakuweza kuzijibu.

"Nilimwandikia barua mimi mwenyewe ajibu hizo tuhuma lakini hakujibu, alipewa nafasi kujitetea lakini hakujitokeza, bado kamati ya siasa haijakaa itakaa itatoa maamuzi kisha halmashauri kuu ya wilaya watamjadili na kuamua afutiwe dhamana au aendelee na uongozi, anasingizia kuwa alikuwa anauguza mama mkwe miezi miwili" anasema Mkaruka.

Mkaruka anasema licha ya kufika Kwenye kikao cha maadili alihojiwa akaambiwa ajibu tuhuma zinazomkabili lakini alikataa kujibu.

Kuhusu malalamiko ya wananchi ya Chama kumsimamisha uongozi akiwa hajakataliwa na wananchi kupitia mkutano mkuu wala kupewa taarifa ya sababu za Mwenyekiti wao kusimamishwa uongozi, Katibu huyo  anasema.

" Yule amedhaminiwa na Chama haitaji kupelekwa kwa wananchi, Chama kikipata malalamiko hata bila kupitia mkutano mkuu kinamjadili na kuchukua hatua, ana tuhuma saba ikiwemo ya kufungwa kifungo cha nje miezi sita" Anasema Mkaruka.

Kuhusu madai ya Mwenyekiti kusimamishwa uongozi bila kujadiliwa ngazi ya CCM Tawi amesema siyo lazima kujadiliwa kwenye Chama ngazi ya Tawi.

"Ukifanya kosa CCM haisubiri ujadiliwe na tawi, ngazi ya juu yako kama CCM Kata ikiona unatumia vibaya madaraka inakuchukulia hatua kwahiyo vikao ndiyo vitaamua aendelee au asiendelee.

Anaongeza kusema " Huyo mtu alishawahi kuua watu watatu, kamati ya maadili ilipendekeza afutiwe dhamana kwahiyo bado vikao vingine vitamjadili na kutoa maamuzi, tumechavishirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kama Polisi vimfanyie uchunguzi pamoja na TAKUKURU.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Butiama Christopher Marwa Siagi anasema kuwa Mwenyekiti huyo wa Kijiji alishaitwa na Chama kujibu tuhuma zinazomkabili lakini alikaidi hivyo chama kupitia vikao vyake vitafanya maamuzi.

        Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Butiama Christopher Marwa Siagi

Mwenyekiti wa Kijiji azidi kujitetea

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Magige Mahera anasema kwamba alikuwa anauguza mgonjwa nje ya Kijiji hicho hivyo asingeweza kumwacha peke yake.

"Nilikuwa nauguza mgonjwa aliyekuwa ananitegemea mimi ningewezaje kumwacha, pia nikaandikiwa barua ya kuitwa kwenye kikao cha maadili,nilienda ofisi ya Chama wilaya, nikawakuta watu watano akiwemo DC, Mwenyekiti na Katibu CCM Wilaya na Wajumbe wengine wawili.

"Wakaniambia ni kikao cha maadili natakiwa nijieleze tuhuma zangu, nikaambiwa mimi mlinisimamisha kupisha uchunguzi sasa leo mnaniambia nijieleze, mimi nilijua mmeniita kunipa matokeo ya uchunguzi" anasema Magige.

Anazidi kueleza" Nikawauliza kwamba nawezaje kujibu tuhuma wakati nilisimamishwa uongozi bila kuitwa kuelezwa tuhuma zinazonikabili wala kujadiliwa kwenye vikao vya Kamati ya maadili Tawi na Kata na halmashauri kuu CCM Tawi na kata?.

Anaongeza" Sijawahi kujadiliwa kwenye kikao chochote cha Halmashauri ya Kijiji kuhusu tuhuma hizo wala sijawahi kukataliwa na wananchi, yalikuwa maamuzi tu ya watu wachache Kati ya Mwenyekiti wa CCM na Katibu CCM Kata.

"Walifanya hivyo kwasababu tu ya mimi kufuatilia rasilimali za Kijiji yakiwemo mabati 180 yaliyokuwa yamechukuliwa na Mwenyekiti wa CCM Kata, kufuatilia mapato kwenye machinjio inayomilikiwa na Katibu wa CCM Kata na vyanzo vingine vya mapato.

"Chama Wilaya kikasikiliza upande mmoja kikatoa maamuzi na kunisimamisha uongozi kabla ya kunisikiliza na mimi au kuniita kwenye kamati ya maadili inijadili kwanza kisha nikionekana nina hatia ndiyo kinisimamishe uongozi kwa hatua zaidi.
 
"Mwenyekiti akaniambia wewe andika tu nikaandika maneno machache, niliwaambia kabla hamjafanya maamuzi mje kijijini  muongee na wananchi na wanachama wawaambie kama tuhuma hizo ni za kweli na sio kusikiliza upande mmoja" Anasema magige.

Kuhusu tuhuma za kuua watu watatu anasema" Sijawahi kuua mtu, wananchi wangu wananipenda hawajawahi kunikataa wala kulalamika, nimesimamishwa uongozi kwa uonevu kutokana na chuki tu za baadhi ya viongozi.

"Kama nishawahi kuua, vyombo vya ulinzi na usalama vipo vitachunguza, kama niliua itajulikana niliowaua na wapi na lini na mashauri yaliendeshwa Mahakama zipi pamoja na hukumu zilizotolewa.

"Kesi niliyohukumiwa ilikuwa ya kifungo cha nje miezi minne shauri la jinai Na. 06/2020 makosa mawili moja kufanya fujo na kutishia kuua kwa maneno, iliyotokana tu na hila za watu.

" Tuligombea uenyekiti kura za maoni tulikuwa watu 11 tukachujwa majina yakapita matatu kupigiwa kura nikashinda mimi, wananchi wakanichagua sasa unawezaje kushinda kura wakati ulishaua watu watatu?, kama niliua baada ya kuwa Mwenyekiti naamini vyombo vya Dola lazima vingenichukulia hatua na ningekataliwa na wananchi?" anasema Magige. 

"Ukisoma ile hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Zanaki kuna kipengele kinasema kwamba mshitakiwa huyu ni mkosaji wa mara ya kwanza, sasa wanavyosema nilishaua watu watatu waithibitishie Serikali na Chama maana wao ndiyo wanawajua kisha polisi wachunguze"anasema.

Machi, 9,2021 Magige Mahera aliandika barua kwenda ofisi ya Usalama wa Taifa mkoa wa Mara akilalamika usalama wa maisha yake kuwa hatarini baada ya kutoa kero za wananchi kwa mbunge wa jimbo hilo, Jumanne Sagini ambaye pia ni Naibu Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

      Mbunge wa jimbo la Butiama Jumanne Sagini ambaye pia ni Naibu Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mwenyekiti huyo aliomba msaada wa usalama wa maisha yake kwenye ofisi hiyo ya usalama wa Taifa kwa madai kuwa muda wowote anaweza kuuawa baada ya kutoa kero za wananchi.

Kwa mujibu wa barua hiyo Mwenyekiti huyo alidai kuwa Machi, 8,2021 alivuliwa uenyekiti wa Kijiji na viongozi wa CCM Kata ya Mirwa kwa kosa la kutoa kero za wananchi kwenye ziara ya Mbunge Machi, 02,2021, kwamba amefukua makabuli inatakiwa azikwe humohumo muda wowote.

Waliotajwa kwenye barua hiyo kumtishia maisha ni Mwenyekiti CCM Kata ya Mirwa Morice Onyango Odhiambo na Katibu wa CCM Kata hiyo Patrick Roche Pius akiomba uchunguzi ufanyike kuhusu kero zilizosomwa mbele ya mbunge na zilizosemwa na wananchi hadharani huku akiwa ameambatanisha na risala na vielelezo vingine.

      Mwenyekiti CCM Kata ya Mirwa Morice Onyango Odhiambo

Mwenyekiti wa Kijiji kupitia barua yake alieleza kuwa ameondolewa kwenye uenyekiti wa Serikali bila taratibu kufuatwa na kwamba aliondolewa pasipo wananchi kupitia mkutano mkuu na hawakuambiwa makosa yanayomkabili kiongozi wao yaliyosababishwa wamvue uongozi.

Nakala ya barua ilitumwa pia ofisi ya Waziri wa TAMISEMI- asaidiwe, Mkuu wa mkoa wa Mara- Kwa utatuzi, TAKUKURU- mkoa wa Mara- Uchunguzi na ofisi ya Upelelezi mkoa wa Mara-Kwa ufuatiliaji.

Barua kwenda ofisi ya Waziri Mkuu


Mwenyekiti huyo anasema kuwa wanaompiganisha ni viongozi wachache na sababu kubwa iliyochochea yeye kuendelea kuchukiwa ni baada ya kulalamika ofisi ya Waziri mkuu kutokana na malakamiko yake kutosikilizwa hivyo akajengewa chuki kuwa amekwenda kuwashtaki ofisi ya Waziri mkuu.

"Julai, 02,2022 niliandika barua ya malalamiko na kero za wananchi wanaoishi Kijiji cha Magunga kwenda ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, ikiomba Waziri wa Ardhi aingilie kati mgogoro wa Ardhi uliopo kati ya Kijiji cha Biatika na Magunga uliodumu kwa muda mrefu.

" Tulilalamika Mkuu wa wilaya Butiama amegawa eneo la ardhi ya Kijiji cha Magunga na kuwapa wananchi Kijiji cha Biatika bila kufuata ramani ya Vijiji ya mwaka 1974, yeye ameegemea upande mmoja kutoa maamuzi kwa kutumia ramani ya mwaka 1996.

Anaongeza "Novemba, 04, 2022 nilituma barua ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma ikihusu malalamiko na kero za wananchi Kijiji cha Magunga nikiomba msaada wa kisheria na usalama wa maisha yangu dhidhi ya Mkuu wa wilaya baada ya kupeleka malalamiko na kero za wananchi ambayo yana muda mrefu hayajatatuliwa".

Anasema kuwa tangu atume barua hiyo ofisi ya Waziri Mkuu amejengewa chuki na baadhi ya viongozi wa CCM na wa Serikali zilizopelekea Chama kumsimamisha tena uenyekiti kwa mara ya pili Novemba, 10,2023.

Mwenyekiti huyo anasema Machi, 8,2021 CCM Kata ilimsimamisha uongozi lakini Chama wilaya kwa wakati huo kilitengua maamuzi ya CCM Kata na kumrudisha madarakani kuendelea na uenyekiti wa Kijiji.

Viongozi waliotuhumiwa kumtishia maisha wamekana kauli hiyo wakisema ni uongo na yenye nia ya kuwachafua.

Hata hivyo anaushukuru uongozi wa mkoa wa Mara kwamba baadhi ya mambo inayafuatilia na kuyafanyia kazi.

              Katibu wa CCM Kata ya Mirwa Patrick Roche Pius


Msomaji, DIMA Online inazidi kukuhabarisha hatua kwa hatua na kwa kina kuhusu yaliyojiri Kijiji cha Magunga endelea kufuatilia habari zaidi.

No comments