MADEREVA WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI ILI KUEPUKA AJALI ZA BARABARANI
Na Catherine Sungura, Tabora
WANANCHI pamoja na madereva wanaoendesha vyombo vya moto nchini wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari wanapokua wanatumia barabara kwa kufuata sheria za barabarani.
Kwa kufanya hivyo wataepusha ajali kwa wao wenyewe au watumiaji wa barabara ili kupunguza ajali na kuepushia Serikali kutumia gharama kubwa za kuwahudumia wagonjwa wanaotokana na ajali.
Rai hiyo imetolewa March, 17, 2023 na Dakatari Bingwa wa Mifupa na Majeruhi kutoka hospitali ya Rufaa ya Kanda- Kamanga ya jijini Mwanza Dk. Fikiri Martin wakati wa kambi ya utoaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mkoa wa Tabora inayofanyika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete.
Dakatari Bingwa wa Mifupa na Majeruhi kutoka hospitali ya Rufaa ya Kanda- Kamanga ya jijini Mwanza Dk. Fikiri Martin“Niwahimize wananchi wachukue tahadhari wanapotumia barabara kwa kufuata alama, sheria za barabarani na kwa wale wanaotumia vyombo vya moto kuwa na leseni na kuzihuisha leseni zao pia kuendesha vyombo hivyo wakiwa wanajihami ili kuepusha ajali kwa wao wenyewe au kwa watumiaji wengine wa barabara”.
Ameongeza kuwa ni vyema kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto kujenga mazoea ya kufunga mikanda na kwa madereva kuendesha magari kwa mwendo unaoendana na hali ya barabara.
Kwa upande wa madereva wa bodaboda Dk. Martin amesema ni vyema waendelee kuvaa kofia ngumu na kuzingatia suala zima la mwendo pamoja na kuwajali abiria wao na wanaowapita barabarani.
“Boda boda ni ajira kubwa na tutaendelea kuwatumia hivyo ni vyema wakawa makini, wakaweka kipaumbele cha afya zao mbele kwani endapo atapata ajali na kuumia mguu au vinginevyo unakua na asilimia hamsini ukapona kabisa au ukatibiwa na kubaki na madhara maisha yako yote, kimsingi ni kuendesha kwa kufuata sheria za barabarani na kuweka maisha yako salama.
Kuhusu kambi hiyo ya utoaji wa huduma za kibingwa Dk. Martin amewashukuru wananchi ambao wamejitokeza kupata huduma za kibingwa kwani zaidi ya wagonjwa wa mifupa mia mbili na hamsini wameonwa katika idara hiyo.
Baadhi ya wagonjwa waliopata ajali hivi karibuni wamefanyiwa upasuaji wa kuwekewa vyuma kwa ajili ya kuunga mifupa ipate muelekeo wake wa zamani.
Naye, mmoja wa wazazi waliopatiwa huduma za kibingwa idara ya mifupa katika kambi hiyo Helena Salumu anayeishi kata ya Kiloleni ameishukuru Serikali kwa kuwafikishia huduma hizo katika hospitali ya Kitete na kutoa ushauri kwa wazazi wengine kutokukata tamaa.
Ameongeza kuwa huduma zipo hivyo wawapeleke watoto wao kwenye vituo vya kutolea huduma pale wanapoona matatizo na kuongeza kuwa mwanaye huyo mwenye umri wa miaka minne aliyapata matege hayo akiwa ameanza kutembelea.
Post a Comment