HEADER AD

HEADER AD

TAKRIBANI WATANZANIA 620,000 WANA ULEMAVU WA KUTOONA

Na WAF – Dodoma

INAKADILIWA kuwa Watanzania takribani 620,000 wana ulemavu wa macho nchini ikiwa ni sawa na asilimia moja ya watu kwenye nchi zinazoendelea na za uchumi wa kati kwa mujibu wa makadirio na takwimu za Shirika la A fya Duniani (WHO).

Hayo yamesemwa leo na Ziada Sellah kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe katika uzinduzi wa  miradi ya afya ya macho yenye jumla ya thamani ya Tsh. Bilioni 1.47 iliyofadhiliwa na shirika la Christoffel Blinden Mission (CBM) iliyofanyika katika Ofisi za WIzara ya Afya jijini Dodoma.

Ziada amesema fedha hizo zitaelekezwa katika maeneo tofauti ambapo Tsh. Milioni 646.85 ni kwa ajili ya Mfumo wa huduma za macho na shilingi Milioni 819.23 ni kwa ajili ya Huduma jumuishi za macho katika mkoa wa Lindi.

“Ni Dhahiri kuwa pamoja na kuwa na fedha hizi zimelenga maeneo yaliyotajwa lakini jamii ya watu kutoka mikoa ya Jirani na Taifa kwa ujumla watanufaika na msaada huu”. Amesema Ziada.

Aidha, Ziada ameongeza kuwa watu wenye matatizo ya kuona kwa kiwango cha kati na cha juu hapa nchini wanakadiriwa kuwa ni mara tatu ya watu wasioona ambao ni takriban watu milioni 1.86, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni mtoto wa jicho, upeo mdogo wa macho unaorekebishika kwa miwani, shinikizo la macho na madhara ya ugonjwa wa kisukari huku akisema asilimia 90 ya matatizo haya yanatibika.

Takwimu za hapa nchini zinaonesha kuwa watu milioni 1.37 kwa mwaka 2022 ndio walifikiwa na huduma za macho katika vituo vya kutolea huduma za afya ikilinganishwa na uhitaji wa takriban watu milioni 12.4 na kati yao asilimia 33.5 wanakua tayari wana upungufu wa kuona hivyo msaada wa Shirika la CBM utasaidia kufikisha huduma za macho kwa watu wengi zaidi.

Naye Meneja Mpango wa Huduma za macho nchini Dkt. Bernadetha Shilio amesema Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa inatekeleza mikakati iliyo ndani mpango wa utekelezaji wa afya ya macho kwa wote 2022-2030 ambao una lengo la kutokomeza upungufu wa kuona unaoepukika ifikapo mwaka 2023.

Akiongelea msaada huo Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CMB nchini Nesia Mahenge amesema shirika hilo linatambua umuhimu wa afya ya macho hivyo limewekeza katika kuisaidia Serikali katika kutatua changamoto ya uoni hafifu na kutoona kabisa ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma za macho katika vituo vya afya nchini.

No comments