SERIKALI YATOA BILIONI 2.2 KUBORESHA MAKUMBUSHO ILI KUVUTIA WATALII
Na Mwandishi Wetu, Arusha
SERIKALI kupitia Mpango wa Fedha za Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 imetoa jumla ya shilingi Bilioni 2.2 kwa ajili ya kuboresha na kukarabati maeneo mbalimbali ya kihistoria ikiwamo Makumbusho ya Taifa na malikale kwa lengo la kuendelea kuvutia watalii wanaokuja nchini.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo March, 16,2013 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipokagua marekebisho na ukarabati wa Makumbusho ya Azimio la Arusha na Makumbusho ya Elimu ya Viumbe jijini Arusha.
"Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha hizo kwa sababu Makumbusho za Taifa zilikuwa zinaendeshwa kwa kusuasua kutokana na changamoto ya ufinyu wa bajeti.
" lakini kwa kipindi hiki bajeti imeanza kuongezeka na moja ya maeneo ambayo Wizara ya Maliasili na Utalii imeipa kipaumbele ni Makumbusho za Taifa na Malikale”Masanja amesema.
Amefafanua kuwa Serikali imeamua kuboresha maeneo ya kihistoria na malikale ili kuwafanya watalii wanapokuja kwa mara ya kwanza nchini, waweze kurudi tena kwa mara nyingine ili kutembelea maeneo ya kihistoria na malikale kujifunza na kupata ladha tofauti ya vivutio vingine vilivyoko nchini Tanzania.
Aidha, amesema kuwa kuboreshwa kwa maeneo ya kihistoria na malikale kutasaidia kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya utalii na kuchangia katika pato la Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Innocent Bilakwate (Mb) amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu na kutoa fedha za kuboresha maeneo ya kihistoria na malikale nchini.
“Makumbusho haya yamekuwa ni ya miaka mingi yakiwa na hali mbaya lakini Mheshimiwa Rais tunamshukuru kwa kuliona hili na kuamua kuwekeza fedha nyingi ambazo kwa kweli tumeona matunda yake na tunaamini kwa jinsi mlivyoboresha tunaenda kupata watalii wengi ambao watakuja kujifunza lakini pia hata vijana wetu ambao wanahitaji kujua mambo ya kale watajifunza vitu vingi” Bilakwate amesisitiza.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii inaendeleza na ziara ya kukagua miradi mbalimbali iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake na Machi 17,2023 itatembelea Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) kilichopo Mkoani Kilimanjaro.
Post a Comment