BARAZA LA MADIWANI LAWAFUKUZA KAZI WATUMISHI WAWILI WA AFYA
Na Abdala Amir, Igunga
KATIKA kukabiliana na tatizo la utoro kazini, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora limewafukuza kazi watumishi wawili wa idara ya Afya kwa kosa la utoro.
Uamuzi huo ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Baraza la madiwani kuafikiana kwa kauli moja watumishi hao waondolewe kazini.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Lucas Bugota alitaja majina ya watumishi hao kuwa Erica Benjamini Jacob (31) aliyekuwa anafanya kazi Hospitali ya Wilaya ya Igunga.
Amesema mtumishi huyo hajaonekana kituo chake cha kazi tangu Oktoba 15 mwaka 2022 na hakuna taarifa yoyote ya yeye kutokuwa kazini.
Mtumishi mwingine alimtaja kuwa ni Andrew Blez Mlabu (27) aliyekuwa akifanya kazi Zahanati ya Kijiji cha Iborogelo katika Halmashauri ya Igunga ambapo hakuonekana kazini tangu tarehe 4 Julai, 2022 huku kukiwa hakuna taarifa zozote kwa mwajiri wake kuhusu kutokwenda kwake kazini.
Katika hatua Nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo aliwataka madiwani hao kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato ya halmashauri hiyo na kuacha kutegemea mapato kutoka kwenye mazao pekee kwani kwa sasa mwenendo wa hali ya hewa imebadilika huvyo si chanzo tena cha uhakika cha mapato.
"Nimatumaini yangu sasa mtakwenda kujielekeza kutafuta vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitawafikisha katika malengo yenu ya makisio ya bajeti au kuvuka kabisa kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato.
"Ndugu zangu wilaya yetu imebarikiwa kuwa na madini, hivyo tukakusanye sasa mapato kutoka vyanzo hivi vya madini na tusiruhusu mianya ya utoroshwaji wa madini katika maeneo yetu," alisema mkuu huyo wa wilaya.
Aidha Mtondoo aliwataka kukusanya mapato katika mazao machache yaliyoanza kuvunwa ikiwemo choroko, vitunguu na kusema kuwa utakapofika msimu wa uvunaji wa pamba pia wakusanye mapato hayo kwa wingi huku akitoa wito kwa viongozi wote wakiwamo madiwani kufata sheria na kanuni za nchi kwenye maeneo yao.
Post a Comment