HEADER AD

HEADER AD

WALIOCHANGAMANA NA WAGONJWA WA MARBURG WAWEKWA KARANTINI

Na Alodia Babara, Bukoba

WATU wapatao 193 miongoni mwao 89 wakiwa ni watumishi wa afya waliokuwa wamechangamana na watu waliobainika kuwa na ugonjwa wa Marburg wilaya ya Bukoba mkoani Kagera  wamewekwa karantini.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Bukoba Machi 23, mwaka huu Mganga mkuu wa serikali Dk Tumaini Nagu amesema kuwa, baada ya watu nane halmashauri ya Bukoba vijijini kuugua ugonjwa wa Marburg na watano kupoteza maisha kuanzia Machi 16, mwaka huu walianza kufuatilia wale wote waliochangamana nao na mpaka sasa watu 193 wamewekwa karantini.

“watu wapatao 193 ambao walichangamana na wagonjwa wa Marburg wamewekwa karantini na kati yao 89 ni watumishi wa afya na tangu tumeanza kuwafuatilia hakuna mwenye dalili ya ugonjwa huu” Amesema Dk Nagu

Amesema wagonjwa watatu wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea vizuri mmoja alikuwa na hali mbaya lakini  Machi 23,mwaka huu hali yake inaendelea kuimalika na serikali inagharamia chakula kwa watu waliowekwa karantini.

Ametaja mikakati ya serikali ya kupambana na ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kuendelea kuelimisha wananchi juu ya kupambana na ugonjwa huo kwa kunawa mikono na maji safi tiririka yenye sabuni.

Pia kutogusana mikono na kutoa taarifa kwa viongozi wao wanapobaini mtu mwenye dalili za kutapika au kutapika damu, kuharisha au kuharisha damu, kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili kuumwa kichwa na joto la mwili kupanda.

Aidha mkakati mwingine ni pamoja na kuweka vifaa vya kupima joto la mwili, vitakasa mikono na maji tiririka yenye sabuni maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vituo vya magari, maeneo ya soko kwenye viwanja vya ndege na bandarini.

Kwa upande wake  Askofu msaidizi wa jimbo katoliki la Bukoba Methodius Kilaini amesema kwa  wanahamasisha juu ya shida iliyopo ya ugonjwa wa Marburg na mambo yanayosemwa na wataalamu lakini kuwaambia waumini wao wasipaniki  na maelekezo yatakayokuwa yanatolewa na wataalamu wa afya nao kuyatoa kwa waumini wao.

No comments