WANANCHI WAISHUKIA CCM BUTIAMA KUMSIMAMISHA UONGOZI MWENYEKITI WA KIJIJI
Na Dinna Maningo, Butiama
WANANCHI wa Kijiji cha Magunga Kata ya Mirwa wamesema kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mirwa na Wilaya ya Butiama mkoani Mara kumsimamisha uongozi Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Magige Mahela kumekwamisha shughuli za maendeleo kutokana na baadhi ya miradi ya ujenzi kusuasua.
DIMA Online ilikuwepo katika Kijiji hicho kwa siku kadhaa ikifuatilia kufahamu sababu ya kuwepo mgogoro baina ya viongozi wa Chama hicho hususani Mwenyekiti wa CCM Moris Onyango Odhiambo na Katibu Patrick Roche Pius Kata ya Mirwa na baadhi ya Viongozi wa Serikali ya Kijiji akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji na wajumbe wa halmashauri ya Kijiji wakituhumiwa kwa makosa saba likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka.
Wananchi wamezungumza na Mwandishi wa habari hii nakueleza changamoto za Kijiji ikiwa ni pamoja na kushangazwa Mwenyekiti wa Kijiji kusimamishwa uongozi bila wananchi kupewa taarifa wala kuelezwa tuhuma zake.
Steven Mazuzuru Kironga anasema tangu Mwenyekiti wa Kijiji asimamishwe uongozi Kijiji hakina maendeleo na kwamba amesimamishwa kwa fitina na watu wenye maslahi binafsi.
"Sasa hivi Kijiji hakina maendeleo tulimpata Mwenyekiti aliyenuia kutuletea maendeleo lakini baadhi ya watu wamepiga vita hadi ameshindwa kufanya kazi, mara wamfungie ofisi mara wamshitaki ni fitina tu ya watu wachache kwa maslahi yao binafsi" anasema Steven.
Phinias Charles anayefanya biashara eneo la mnadani anasema" Kila mwaka tunalipa leseni 30,000, ushuru wa usafi sh.1,000 usafi wenyewe wanafanya mara moja kwa wiki siku ya alhamis, siku zingine tunafanya usafi wenyewe kila mtu anajifanyia kwenye eneo lake" anasema Phinias.
Scola Chacha mama lishe katika mnada wa Kijiji hicho anasema kukosekana choo wateja wanaofika kupata huduma ya chakula wanapata tabu.
"Mwenyekiti alipoingia madarakani choo kikaanza kujengwa tangu walipomsimamisha ujenzi umekuwa wa kusuasua, choo ni shida mpaka ukatafute huko senta au kwenye miji ya watu au ukaombe mwaloni kwa wachimbaji wa Dhahabu.
" Kuna choo cha mtu binafsi chenyewe kinafunguliwa siku ya mnada jumamosi. alafu huwa tunatozwa ushuru sh.1,000 ya usafi wakati kila siku tunajifanyia wenyewe usafi kwenye maeneo yetu"anasema Scola.
Mama Lishe katika mnada wa Kijiji cha Magunga akisonga ugali
Sara Machera anaongeza " Wengi wanaenda kujisaidia kule mwaloni au ofisi ya mgodi, kuna choo cha Masanja cha mtu binafsi ambacho kilikuwa kinafunguliwa jumamosi kilishafungwa kilikuwa cha mtu binafsi. Tunalipishwa ushuru sh 500 au 1000, kodi ya pango la ardhi sh. 50,000 lakini choo hakuna" anasema.
Sara Machera anaongeza " Wengi wanaenda kujisaidia kule mwaloni au ofisi ya mgodi, kuna choo cha Masanja cha mtu binafsi ambacho kilikuwa kinafunguliwa jumamosi kilishafungwa kilikuwa cha mtu binafsi. Tunalipishwa ushuru sh 500 au 1000, kodi ya pango la ardhi sh. 50,000 lakini choo hakuna" anasema.
John Isack Mwita anasema Kijiji hakifaidiki na mapato kwani inapotokea kiongozi anakuwa mfatiliaji wa mapato anawekewa vikwazo.
"Anapotokea Mwenyekiti wa Kijiji mfuatiliaji wa mapato wanaibuka watu na kumkandamiza, msema kweli anakuwa hana nguvu ,mnada umeanza 2007 lakini choo hakuna kingekamilika ni maslahi ya Kijiji hatujui nini tatizo la kutokamilika.
"Mwenyekiti anapotokea kufanya maendeleo wanamkwamisha wanapachika wa kwao kukaimu wenyekiti wa Kijiji, serikali itusaidie maana kuna vyanzo vingi vya mapato lakini hata ukienda shuleni ni shida, madarasa yamezeeka, madawati hakuna watoto wanakaa chini, vyumba vya madarasa ni pungufu" anasema.
John Onaka Obare mkazi wa Kijiji hicho anasema Kijiji kinakabiliwa na utawala usio na mpaka kwa viongozi hususani Mwenyekiti, Katibu wa CCM Kata huku akisema kwamba Diwani wa Kata hiyo Willy Brown ameshindwa kushirikiana na wajumbe wake badala yake amekuwa mtu wa makundi.
" Diwani anatakiwa kushirikiana na wajumbe wake lakini nafasi hiyo ameigeuza na kuwa ndiyo Mwenyekiti wa Kijiji, kuna vikao vya Serikali ya Kijiji anatoa maamuzi yeye kama yeye na baadhi ya wajumbe ambao wapo upande wake na kutoa maamuzi" anasema.
Anaongeza" Tunapata changamoto pale Diwani anapomnadi Mwenyekiti asiye halali alafu wananchi wanamzomea hii inaleta shida sana viongozi wa CCM ngazi za juu walitizame hili kwa jicho la karibu juu ya viongozi wao wa ngazi za chini.
"Mpaka kuona choo kimesimama tatizo ni uongozi wa Chama, Mwenyekiti wa Kijiji ndiyo anaongoza Serikali lakini utakuta Mwenyekiti wa Chama ndiyo yupo saiti anasimamaia miradi ya Kijiji.
Ochieng' Alobart Nundu anasema maendeleo Kijiji cha Magunga yamekuwa hafifu kutokana na wananchi kuchonganishwa na viongozi wenye nguvu ya kifedha.
"Mwenyekiti tuliyemchagua alipoingia madarakani alikuta shimo lililokuwa limechimbwa takataka zimejaa la futi 60, likazibuliwa na ujenzi kuanza hadi hapo ulipofikia, tunasikia maneno kuwa kasimamishwa uenyekiti na hatujui makosa yake ni yapi.
"Watu wameendelea kutupa uchafu kwenye shimo la choo limeziba tena kwasababu Mwenyekiti na Katibu wa CCM Kata walisema shimo lifunikwe kwamba eneo ni la mmiliki wa sheli, tunaomba Waandishi wa Habari mje muishi Butiama muandike habari maendeleo yamekuwa hafifu kwa kuchonganishwa na viongozi wenye nguvu ya kiuchumi" anasema.
Daniel Omoro Ojwang'i fundi viatu anasema baadhi ya viongozi wanampiga vita Mwenyekiti wa Kijiji bila sababu za msingi kwasababu ya kufuatilia fedha za ujenzi wa miradi.
"Serikali yetu ilituletea fedha kukamilisha Zahanati tuliyoijenga kwa nguvu zetu lakini imeshindikana kuisha, wanampiga vita hata choo kimekuwa shida kuisha, wananchi bado wanampenda Mwenyekiti wa Kijiji.
"Chama kama kina mtuhumu Mwenyekiti kimlete mbele ya wananchi kitueleze makosa yake tuyajue tuyajadili na sio wao kumsimamisha bila ridhaa ya wananchi kisa tu wenye fedha zao hawamtaki kwasababu ya maslahi binafsi".
Dickson Julius Mafuru mkazi wa Kitongoji cha Rwamakore anasema wananchi wameshindwa kutambua Mwenyekiti ni nani na kwamba wao wanajua Mwenyekiti ni Magige aliyepigiwa Kura na wananchi.
"Eti Chama kinaleta mtu wao awe Mwenyekiti wa Kijiji yaani tangu Mwenyekiti wa Kijiji asimamishwe mwaka jana tunaona ni kama miaka miwili, hatujakaa mkutano, miradi yote imesimama, mapato yanakusanywa hatujui ni kiasi gani ,akijitokeza mtu kufuatilia anaundiwa mizengwe na kukataliwa.
" Chama kilituletea Mwenyekiti tukampigia kura sasa kilipomuondoa mbona hakijarudi kuwaeleza wananchi kwamba huyu Mwenyekiti tuliyewaletea mkampigia kura ana shida hii na hii ili tumjadili.
"Sisi wananchi hatujawahi kumkataa kimemsimanisha na kuleta mtu mwingine bila kutuambia tukienda ofisini tunahudumiwa na mtu ambaye hatujatambulishwa kwenye mkutano".anasema Dickson.
Daniel Chacha yeye anakitupia lawama Chama cha Mapinduzi kwa kutofuata taratibu za kumsimamisha uongozi Mwenyekiti wa Kijiji kwa kutoshirikisha wananchi ambao ndiyo wapiga kura na waamuzi wa mwisho.
"Chama kinachangia kurudisha nyuma maendeleo tangu kimsimamishe Mwenyekiti maendeleo yamesimama kwanini Chama kimtoe wakati wananchi hawajamkataa? CCM Kata inarudisha nyuma miradi kama Mwenyekiti ana makosa mbona hawajaja kutuambia.
"Wanasingizia kwamba wanasimamia Ilani tangu wamekuwa viongozi wa Chama kwa miaka kadhaa mbona kijiji hakiendelei zaidi tu yakuwa sehemu ya migogoro na kukwamisha jitihada za viongozi kwa sababu ya maslahi binafsi.
"Hao viongozi ni wabinafsi wanataka wajiendeleze maisha yao binafsi na sio kwa maslahi ya jamii, akipatikana Mwenyekiti mzuri mwenye nia ya maendeleo wanampinga na kumpiganisha kwa wajumbe wa Serikali ya Kijiji tangu wamemsimamisha hakuna maendeleo"anasema Daniel.
Viongozi wa CCM kuwa wajumbe wa Serikali
Silas Nashoni ni mkazi wa Kitongoji cha Bwezindwe anasema shida kubwa ni ung'ang'anizi wa madaraka kati ya CCM na Viongozi wa Serikali ya Kijiji kwamba asilimia kubwa ya viongozi wa CCM ni wajumbe wa Serikali ya Kijiji hali inayosababisha migongano ya kiuongozi.
"Mfano Katibu wa CCM Kata amekuwa mjumbe Serikali ya Kijiji wakati huohuo ni Katibu wa Chama ameondolewa mwaka jana wakati wa uchaguzi wa Chama akaambiwa achague moja ndiyo kubaki na nafasi ya ukatibu" anasema Silas.
Anaongeza "wanasema Wenyeviti hawasomi mapato na matumizi mbona hao wanaowaweka hatujaona wakisoma mapato na matumizi? wametanguliza tu maslahi yao.
"CCM ndiyo msimamizi wa Serikali na kuna viongozi wa Chama ni wajumbe halmashauri ya Kijiji, vikifanyika vikao vya chama kujadili viongozi wa serikali hao wajumbe wanasimamia upande gani wakati haohao ni viongozi wa Chama na haohao ni wajumbe halmashauri ya Kijiji.
"Nani atakosoa mwingine, na hawa ndiyo wanachukua maneno kwenye serikali kupeleka kwa hao viongozi wa Chama na kusababisha uchonganishi" anasema.
Viongozi hao wa CCM Kata ambao pia ni wajumbe Halmashauri ya Kijiji ni Grolia Nashoni ambaye ni Katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Matias Maleni mjumbe Halmashauri kuu ya CCM Tawi la Magunga, Fatma Charles, Raheli Sosi na Ferista Washton ambao ni wajumbe wa Halmashauri kuu ya Kata.
Mfanyabiashara katika soko lililopo senta ya Kijiji hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa Machinga Kata ya Mirwa Samson Orwa Atula anasema wafanyabiashara wanatoa ushuru kama pango la ardhi katika Serikali ya Kijiji hicho kila mwaka Tsh. 30,000 lakini soko halina choo.
"Watu wakitaka kujisaidia wanakwenda kuomba kwenye nyumba za watu, wengine wanaenda kuomba hotelini na kila jumamosi watu wanatozwa sh. 1000 ambayo ni siku ya mnada, tulipouliza ni pesa ya nini wakasema ni ya kutunisha mfuko wa halmashauri." anasema Samson.
Baadhi ya wananchi na wanachama cha CCM wamezungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao kwa kile walichoeleza kwamba watajengewa chuki na Viongozi.
"Diwani anasema kwamba alikuwa mjumbe ofisi ya Rais, Ila ajue kwamba yeye ni Diwani wa Kata anatakiwa apangilie kazi yake, yeye anaendeshwa na CCM, Mwenyekiti na Katibu wa CCM Kata wamemchagua mtu kukaimu uenyekiti alafu Diwani unaambiwa ukamtambulishe msibani unaenda.
" Diwani anapata wapi hayo mamlaka kwani yeye ndiyo anawajibika kumtangaza Mwenyekiti msibani! hawa viongozi wa CCM Kata na Diwani wamekuwa miungu watu, wana biashara zao wakibanwa kulipa kodi wanachukia watu,miradi ilianzishwa wanataka kila tenda wapewe wao ukibisha unasimamishwa uongozi" anasema mjumbe mmoja.
Anaongeza" Kibaya zaidi vikifanyika vikao vya Chama Serikali ya Kijiji kupitia Mtendaji wa Kijiji ambaye ni kitu kimoja na hao viongozi anawalipa posho vikao vya CCM, kuna siku tulikaa wajumbe tukasainishwa sh. 3,000 Diwani akasaini Laki moja na Mwenyekiti na Katibu wa Chama Kata, wao wakisani posho ni 100,000-150,000 fedha ambazo ni mapato ya serikali ya kijiji"anasema mjumbe mmoja Serikali ya Kijiji.
Mwananchi Mwingine anasema " Tunaiomba Serikali ichunguze uraia wa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mirwa ni Mkenya alihamia huku, yawezekana hajui taratibu za nchi katika kuongoza watu, ifuatilie na miradi yake kama analipa kodi inavyotakiwa yeye na Katibu wa CCM, haiwezekani akiwepo mtu kufuatilia vyanzo vya mapato wanawaundia njama za kuwaondoa madarakani ili tu asiwepo wa kuwafuatilia" anasema.
Mwanachama mwingine anasema" Katibu wa CCM Kata ya Mirwa alisababisha Kijiji kikawa na matawi mawili Katibu alipoangushwa kwenye uchaguzi akaenda kuanzisha tawi lingine la Kamimange ndani ya Kijiji lililovunjwa 2021 wakati wa uchaguzi huyu ni shida sana sema kwakuwa wana watu wao juu na fedha wanashinda chaguzi lakini hawapendeki" anasema.
" Hawa viongozi wanatumia Ilani vibaya wanakuwa na maslahi yao binafsi alafu wanasingizia kwamba wanasimamia Ilani, tangu wasimamie hilo Ilani mbona kila kukicha ni migogoro, siku Mwenyekiti na Katibu wakiacha uongozi Magunga itatulia Magunga inakuwa shida kwakuwa hao viongozi ni wakazi wa Magunga na Magunga ina vyanzo vya mapato".
Mjumbe mwingine anasema" Tatizo la Mwenyekiti wa Kijiji ana papara sana ahitaji ushauri, siasa haitaki uwe mwelevu sana inataka ukae katikati na ukubali kuelekezwa na kushauriana anajionesha yeye anajua sana.
"Mwenyekiti sio mwanasiasa alijaribu tu kugombea akashinda kwakuaminiwa na wananchi kutokana na uhanaharakati wake ni mwanaharakati sana, kinachomuuliza kingine ni kuwashitaki viongozi ngazi za juu sasa wanaona kama anawachongea na hivyo kumchukia" anasema.
Mwenyekiti mmoja wa Kitongoji anasema" Hivi vitu vinahitaji uzoefu kuna wajumbe wa Kamati ya maji waliochaguliwa kwa mpito waliokuwa wakisimamia mradi wa maji wakaondolewa sasa wameweka watu wengine hawajui chochote wanaambiwa wewe nenda kasimamie na wajumbe hao wakati wanawekwa, wajumbe wa zamani hawakushirikishwa hata wangekuwa washauri kwakuwa wana uzoefu wa kazi hiyo" anasema.
Anaongeza "eti vikao vikifanyika Mtendaji wa Kijiji Lucus Kagina anawaambia wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango waandae taarifa ya mapato na matumizi, kuna siku waliandaa taarifa ikakataliwa na wananchi mkutanoni" anasema.
Mwanachama Mwingine anasema " Tunawaomba viongozi wa Chama ngazi ya Mkoa na Taifa waingilie kati wanaoitesa Magunga ni Mwenyekiti wa CCM, Katibu na Diwani na kwakuwa wana fedha na vyeo wanalindwa na viongozi wa Chama na Serikali wilaya.
"Serikali iwe inatoa elimu kwa viongozi wa halmashauri ya Kijiji, watu walichaguliwa lakini hawajawahi kupata elimu ya matumizi bora ya fedha za Serikali, utawala bora, mtu anakuwa Mwenyekiti wa Kitongoji au mjumbe wa kamati lakini hajawahi kupata elimu juu ya nafasi yake aliyopewa kutumika.
Anaongeza "Rais Samia tunaomba tukwambie kwamba siyo kwamba watu hawaipendi CCM, wanaipenda sana tatizo ni viongozi waliopo hasa hawa wa Kata na viongozi wa wilaya.
"Hawa viongozi wakipewa taarifa hawafuatilii kwa kina wala kufika kijijini kuongea na wananchi na wanachama kujua uhalisia wa migogoro, wanahukumu watu bila kusikiliza mawazo ya watu wengine.
"Haiwezekani CCM wilaya iseme kwamba siyo lazima mtuhumiwa kujadiliwa kwenye vikao vya maadili vikiwemo vya Tawi na Kata, sasa matawi yaliwekwa kwa kazi gani na wajumbe wamewekwa kufanya nini?"anahoji.
Anaongeza "Kwa hali hii inaonesha viongozi wa CCM Wilaya wapo upande wa viongozi wa CCM Kata na sio kwa ajili ya Chama, wangekuwa wapo kwa ajili ya Chama ni lazima wangefika kijijini kusikiliza wananchi na wanachama badala ya kukaa ofisini na kuandika barua.
"Viongozi CCM ngazi ya za juu mjue kuwa sasa hivi hawa viongozi wanatutushia kwamba kwakuwa wao ndiyo viongozi wa Kata tukigombea ujumbe, uenyekiti wa Kijiji watakata majina.
"Kama hali ikiwa hivi CCM msijeshangaa kuona baadhi ya wanachama wanakimbilia upinzani, ni kutokana na hawa viongozi ambao wamekuwa wao ndiyo kila kitu wao ndiyo wanasikilizwa zaidi kisa wana pesa tusio na kitu tunaonekana mzigo" anasema.
Wananchi waniomba Serikali kutatua changamoto katika Kijiji hicho ikiwemo ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kama inaendana na fedha tolewa pamoja na changamoto ya uongozi katika Kijiji hicho.
Viongozi ngazi ya juu wanaombwa kuingilia kati maamuzi yaliyofanywa na viongozi wa CCM ngazi ya Kata na Wilaya wakisisitiza maoni ya wananchi na wanachama yasikiliwe zaidi na sio maoni ya viongozi wa chache jambo ambalo limechangia kuibuka kwa migogoro ndani ya Chama na Serikali ya Kijiji.
Diwani wa Kata ya Mirwa Willy Brown anasema " Kazi yangu ni kusimamia maendeleo ya Kata, suala la kumtangaza mjumbe kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji mimi nilifanya hivyo kwakuwa ndiyo mtu niliyepewa kufanya nae kazi.
"Mimi sibagui kufanya kazi na watu, hata nilipoletewa Polisi Kata nifanye nae kazi sikukataa kwahiyo huyo mjumbe kumtambulisha msibani sikufanya makosa.
Kauli ya viongozi wa Serikali
Mwandishi wa habari akawasiliana na Meneja Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Butiama, Mhandisi Dominic Mafuru kufahamu sababu ya mradi kutotoa maji ambapo amesema mradi huo ulisimama kutokana na gharama za uendeshaji baada ya kupanda gharama za mafuta ya dizeli.
Meneja Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Butiama, Mhandisi Dominic Mafuru
"Miradi yote ya maji kikiwemo hicho kisima fedha za makusanyo huwa zinaingia kwenye akaunti ya maji ya Kijiji, shida iliyopo ni gharama kubwa za uendeshaji ndiyo zimekwamisha mradi kutokana na kupanda gharama za mafuta ya Dizeli, ndoo moja ya maji ni sh. 50 na siyo wote wanachota.
"Kutokana na gharama kupanda fedha zikakosekana kuwezesha kuendesha mradi huo, ila tayari tumeshirikiana na TANESCO Transifoma imepelekea kwenye mradi ili utumie umeme badala ya mafuta ya Dizeli"amesema Mhandisi Dominic.
Machi, 13, 2023 Mwandishi wa Habari alitembelea mradi huo wa maji na kukuta ukiwa hautoi huduma ya maji, hata hivyo siku mbili baada ya Mwandishi wa Habari kufika Kwenye mradi huo mafundi wa TANESCO walifika na kuweka Transifoma. Huduma ya maji bado haijarejea.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama Patricia Kabaka alipoulizwa kuhusu Mwenyekiti wa Kijiji kusimamishwa uongozi amesema hana taarifa ya Mwenyekiti wa Kijiji kusimamishwa uenyekiti na Chama cha Mapinduzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama Patricia Kabaka
Alipoulizwa kuhusu miradi kujengwa chini ya kiwango isiyoendana na fedha tolewa amesema hawezi kuzungumza kupitia simu au ujumbe wa maneno. Na ilipopita siku moja baada ya kupigiwa simu alisema yupo safari na kuahidi atakaporudi atazungumza na Mwandishi huyo wa habari.
Baada ya Mkurugenzi huyo kudai kwamba yupo safari na kuahidi atakaporudi atazungumza nae, Mwandishi huyo wa DIMA Online alimtumia maswali kwa njia ya ujumbe (SMS) ili kuyajibu tangu Machi, 15,2023 lakini hakujibu chochote hadi habari hii inaripotiwa DIMA Online.
Mwandishi alichotaka kufahamu kwa Mkurugenzi Butiama
Mwandishi wa habari alitaka kufahamu baadhi ya mambo katika Kijiji cha Magunga Kata ya Mirwa kuhusu mapato ya Kijiji ambapo Mwenyekiti wa Kijiji aliyesimamishwa uongozi na CCM Magige Mahela alidai kuwa sababu ya kusimamishwa uenyekiti ni baada ya kufuatilia vyanzo vya mapato na ujenzi wa miradi inayojengwa kwa fedha za Serikali laki ujenzi hauendani na fedha halisi zilizotolewa.
Mwandishi wa habari hii alitaka kufahamu mapato ya ndani ya Kijiji hicho ikiwa ni pamoja na;
Madai ya kuwepo mnara wa Vodacom kutoingiza mapato kwenye Kijiji licha ya kuwekezwa kijijini, fedha kutoka mgodi wa Dhahabu uliopo kijijini zinazokusanywa na halmashauri lakini hazionekani kutekeleza miradi kijijini, Josho lililojengwa chini ya kiwango na mgodi, kutokamilika kwa choo cha sokoni na choo cha mnadani.
Miradi mingine ni ujenzi wa Zahanati kutumia zaidi ya Milioni 66 katika kupaua na ukamilishaji lakini bado haijakamilika, Fedha zilitolewa kwenye akaunti ya Kijiji kununua sola kwa ajili ya Zahanati lakini haijanunuliwa licha ya Mtendaji wa Kijiji na watia saini kwenda benk kudroo fedha hizo ambapo inadaiwa Mtendaji alichukua kuwa anaenda kununua sola lakini hakununua na badala Sola imenunuliwa kwa fedha za mkopo.
CCM kumkaimisha ukaimu unyekiti wa Kijiji Mjumbe kinyume cha taratibu za kiserikali, Makusanyo ya fedha za miradi ya Kijiji kama maegesho ya magari (beria), mnada,mgodi ,machinjio kutojulikana kama yapo eneo la serikali ya Kijiji au ya binafsi, kutokuwepo uwazi kwenye makusanyo.
Mgogoro wa ardhi wa mpaka baina ya Kijiji cha Magunga na Biatika, kutokamilika maabara shuleni licha ya fedha kuchangwa Milioni 10, shule ya msingi Magunga majengo kuwa katika hali mbaya , uhaba wa vyumba vya madarasa shule zilizopo kijijini licha yakwamba kuna mgodi kijijini unaochangia kodi halmashauri pamoja na mapato mengine katika Kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mwl. Moses Kaegele amesema Magige Mahela hajafutiwa dhamana ya uenyekiti ila amesimamishwa na Chama na kinaendelea na taratibu zao na kwamba wakikamilisha Serikali nayo itafanya taratibu zake.
Post a Comment