WASEMAVYO WENYEVITI WA VITONGOJI, WAJUMBE KUSIMAMISHWA MWENYEKITI WA KIJIJI
Na Dinna Maningo, Butiama
HIVI karibuni DIMA Online imekuwa ikiripoti habari mbalimbali katika Kijiji cha Magunga Kata ya Mirwa, wilaya ya Butiama mkoani Mara, zikihusu migogoro ya kiuongozi baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ya Kijiji pamoja na ujenzi wa miradi isiyoendana na fedha halisi.
Pia imeripoti habari kuhusu CCM ngazi ya Kata na Wilaya kumsimamisha uongozi Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga, Magige Mahera Msyomi na nafasi yake kukaimishwa mjumbe wa halmashauri ya Kijiji hicho.
Kubwa zaidi lililotikisa vichwa vya watu ni utaratibu unaotumika kuwasimamisha uongozi viongozi wa Kijiji akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji hicho na wajumbe wengine watatu Kama ilivyoripotiwa katika chombo hiki cha habari.
Wenyeviti wa Vitongoji, wajumbe wa halmashauri ya Kijiji wanashangazwa na utaratibu unaotumiwa na viongozi wa CCM kuwasimamisha uongozi viongozi wanaotokana na Chama hicho, wakiwa hawajakataliwa na wananchi kupitia mkutano mkuu wala kujadiliwa halmashauri ya kijiji na katika vikao vya chama hicho ngazi ya Tawi na Kata vikiwemo vikao vya Kamati ya maadili kuhusu tuhuma zilizotolewa na CCM.
Mbali na kuzungumza na viongozi wa CCM na Mwenyekiti wa Kijiji aliyesimamishwa uongozi, Mwandishi wa chombo hiki cha habari amezungumza na Wenyeviti wa Vitongoji na Wajumbe wa halmashauri ya Kijiji kuhusu yanayoendelea katika Kijiji hicho nao wana haya ya kusema.
Wenyeviti wa Vitongoji, wajumbe wafunguka
Ferista Washington Robert ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Magunga na mjumbe kamati ya ardhi halmshauri ya kijiji hicho ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa kamati ya ardhi 2014-2017, mjumbe wa Kamati ya ujenzi 2017-2019, anasema haoni makosa ya kusababisha Mwenyekiti Kusimamishwa uongozi.
"Mimi sioni makosa ya Mwenyekiti ingawa kila kazi kuna makosa madogomadogo lakini kosa kubwa la kumsimamisha silioni, angekuwa na makosa wajumbe wa halmashauri ya Kijiji tungekaa, tungemjadili alafu tungepeleka mkutano mkuu wa kijiji wakamkataa huko.
"Chama kilimsimamisha, wajumbe tuliitwa ofisi ya Chama Kata, Mwenyekiti wa Chama na Katibu wakasema kuna makosa Mwenyekiti wa Kijiji anaonekana anayo lakini hatukusomewa hayo makosa tuyajue wala kuyajadili.
"Binafsi sijaona changamoto zake, ni mzuri japo wakati mwingine ana kaubaguzi kwa baadhi ya wajumbe anapenda kubadilisha kila mara wajumbe kwenye kamati, anapenda kusikiliza watu wa nje, ila kiukweli wananchi wanampenda"anasema Ferista.
Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Magunga ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya ujenzi William Mriri Ghati aliyesimamishwa ujumbe na Chama bila kupewa barua anasema;
"Changamoto ni kusimamishwa mara kwa mara kwa viongozi, kuna wajumbe tulisimamishwa Februari, 02, 2020 na viongozi wa Kata,Mwenyekiti wa CCM na Katibu wakasema sisi tuna itikadi ya CHADEMA kisa tu tulikuwa tunapingana na matendo yao.
" Hadi leo hii hatujawahi jadiliwa kurudishwa au kuondolewa tupotupo tu Chama kipo kimya. Magunga kuna vita ya uchumi viongozi wa Chama hawataki Mwenyekiti anayesema ukweli, tulipogusia Machinjio ya Katibu wa CCM kuhusu mapato ya machinjio ikawa chuki.
'Mwenyekiti wa Kijiji alipogusia mapato mnara wa Vodacom uliowekwa tangu 2012 Mwenyekiti wa CCM akaleta shida, eneo kuliko na mnara lilikuwa eneo la mtu binafsi akamuuzia mtu mmoja waliokuja kuweka mnara yupo Arusha.
"Mnara unatoa huduma kwa jamii lakini Kijiji hakinufaiki chochote, ukienda kuzungumzia Mwenyekiti wa CCM anakuandama kana kwamba ana maslahi na huo mnara"anasema.
Akizungumzia ujenzi wa choo cha mnadani kilichogharimu zaidi ya Tsh. Milioni 12 lakini halijakamilika William anasema;
"Mwenyekiti wa Kijiji tangu ameingia madarakani amekuwa akijitahidi sana kufuatilia miradi ya maendeleo, hata hii choo alipojaribu kufuatilia matumizi ya fedha akajengewa chuki na wafujaji wa fedha.
"Wajumbe ilikuwa ni kuangalia tu wanavyojenga, ujenzi ulisimamiwa na Mtendaji wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi ni Chacha Wambura Kichune, Katibu Miliamu James, Fatuma Charles na Rahel Sosi Juma lakini tulikuwepo kama pambo sisi kazi ilikuwa ni kuangalia tu ujenzi unavyokwenda basi hakuna zaidi ya hapo " anasema.
Roza Robart Rubirya ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bwezindwi ambaye pia ni mtia saini wa Serikali ya Kijiji cha Magunga, anasema tamaa ya madaraka na kuvamia madaraka imekuwa shida kwenye Kijiji hicho.
"Viongozi wetu wa CCM Kata wamekuwa na tamaa ya madaraka wanatumia uzoefu wao walionao kwenye Chama kudhoofisha uongozi wa Serikali ya Kijiji kwasababu kila kitu wanataka Chama ndiyo kifanye Serikali ya Kijiji cha Magunga haina mamlaka.
" Mwandishi hiki kiwanja unachokiona vijana walikuwa wanakitumia kucheza mpira ni cha Serikali ya Kijiji lakini Chama kimekataa wakasema ni chao, vijana waliomba kujenga chumba kwa ajili ya kubadilisha nguo wanapotaka kucheza mpira lakini CCM imekataa inasema ni uwanja wao.
"Sisi tunaomba Serikali ije ituweke wazi kwamba huu uwanja ni wa Serikali au wa CCM? mkutano wa wananchi huitishwe wale wazee wa zamani waje tuwekwe wazi, maeneo ya Serikali yanachukuliwa kwamba ni ya CCM hata ofisi ya Kijiji wanasema ni eneo la Chama.
Anasema CCM Tawi haijawahi kumjadili Mwenyekiti wa kijiji na wajumbe watatu waliosimamishwa uongozi na Chama kwamba kinachofanyika ni maamuzi ya Viongozi wachache wa CCM ngazi ya Kata.
" Hatujawahi kukaa kikao chochote wala CCM Tawi kumjadili Mwenyekiti wa kijiji ila CCM Kata ndiyo ilituita kutupa maelekezo, sisi tunaitwa tu kupewa maelekezo na maagizo, tukaambiwa kwamba Mwenyekiti ana tuhuma wamezipeleka CCM wilayani lakini hatukutajiwa hizo tuhuma tulihoji ili tuelezwe lakini hawakusema".
"Wananchi hawajui kama kuna Mwenyekiti mwingine aliyeteuliwa na Chama kukaimu, nilishangaa siku moja Diwani anamtangaza Mwenyekiti aliyekaimishwa ofisi kwenye msiba kuwa ndiyo kaimu" anasema.
Akizungumzia kisima cha maji cha umma ambacho fedha zake zinakusanywa lakini zinaishia kwenye mifuko ya watu anasema.
" Hiki kisima lilikuwa cha HESAWA ni cha jamii kilikuwa kinasimamiwa na Serikali ya Kijiji, mradi wa maji ulipoingia kisima hiki kinasimamiwa na Kamati ya maji, Mwenyekiti wa Kamati ya Maji ameweka mkamwana wake anakusanya fedha pesa kila ndoo sh. 50 lakini pesa haziendi kwenye akaunti ya maji ya Kijiji pesa anachukua yeye anatumia kwa matumizi yake binafsi, tukifuatilia anasema mradi ni wa wilaya siyo wa Serikali ya Kijiji.
Alipohojiwa mkusanya fedha kwenye kisima hicho anasema" Maji ndoo moja ni sh. 50 kwa siku mauzo ni 6,000- 10,000, msimu wa mvua mauzo ni kidogo nakusanya nampa Mwenyekiti yeye ndiyo anajua anakopeleka"anasema.
Mwenyekiti huyo wa Kitongoji anasema Zahanati ipo kwenye kitongoji chake tangu ifunguliwe Novemba, 11,2022 na waganga kupelekwa lakini bado ujenzi haujakamilika japo baadhi ya vifaa vimo ndani ya Zahanati hiyo.
Zahanati hiyo ambayo imeelezwa kugharimu zaidi ya Milioni 70 katika ukamilishaji ambapo serikali ilitoa Milioni 50, fedha hazikutosha Serikali ya Kijiji ikaongeza Milioni 20 lakini bado haijakamilika.
DIMAOnline ilifika katika Zahanati hiyo na kukuta baadhi ya vyumba havina sakafu, baadhi ya madirisha yamewekwa vioo bila magrili, hakuna Sola,haijapakwa rangi na mahitaji mengine ya jengo.
Mwenyekiti Roza anaeleza utaratibu unaotumika kutoa fedha benk" Mimi ni mtia saini nipo na mwenzangu Miliam Magubo, tukienda Benk Muhasibu ni Mtendaji wa Kijiji Lucus Kagina yeye ndiye anatoa fedha sisi kazi yetu ni kusaini tu hatushiki fedha, kujua zimetumikaje sisi hatujui na nyaraka hubaki kwa Mtendaji.
"Kuna pesa tulienda na Mtendaji benk tukasaini Milioni 2 na laki nane tukasema lakini nane iende kwenye ujenzi wa Zahanati, Milioni mbili ilikuwa kwa ajili ya kununua Sola ya Zahanati, Mtendaji alichukua fedha lakini cha ajabu Sola haijawahi kununuliwa fedha hatujui Mtendaji alipeleka wapi.
"Baada ya Mwandishi wa habari kufika Kwenye zahanati, Mtendaji akakopa Sola ndogo mbili zimewekwa ambazo walisema ni laki tisa, sasa sijui italipwa kwa pesa ipi wakati Milioni mbili haijulikani ilipo na tulienda na Mtendaji akadroo fedha benk akaondoka nazo keshi, hajazisomea mapato na matumizi, ukiuliza inakuwa kosa unachukiwa" anasema Roza.
Mwenyekiti huyo wa Kitongoji anazidi kueleza " kwenye ujenzi kuna shida kidogo fundi anapoletwa kujenga wanasema tumekutafuta tupe ya maji sasa hii wakati mwingine unakuta miradi inakuwa chini ya kiwango inatolewa kwa kujuana na watu wanapata kitu kidogo inakuwa ngumu kuwasimamia maana huwezi msimamia vizuri mtu aliyekupa kitu kidogo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Rwamakore Warioba Msuri Warioba anasema kuwa Kijiji kina changamoto ya unyang'anyi wa madaraka unaofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM.
"Mwenyekiti wa Kijiji alitafuta vyanzo na ikabainika viongozi wanahusika, unapoonekana kusimamia vyanzo vya mapato viongozi wanakudhoofisha kuhakikisha unatoka madarakani.
"Wakiona kuna chanzo kinanufaisha Kijiji wanaingiza hila zao kile chanzo mtanyang'anywa ili mapato yaende wilayani yakienda kule wananchi hawanufaiki nayo hivyo ubunifu wa viongozi wa kijiji unapotea bure.
"Ila sisi viongozi hatutakata tamaa tunashirikiana na wananchi kufanya maendeleo japo tunapitia kipindi kigumu dhidi ya viongozi wa Chama"anasema.
Mjumbe wa halmashauri ya Kijiji cha Magunga Juma Wilson anasema yeye amesimamishwa ujumbe baada ya kukataa maelekezo ya Chama chake kushinikiza wamkatae Mwenyekiti wa Kijiji.
" Wajumbe tuliambiwa tuandike mahudhulio kuwa tukubali hatumtaki Mwenyekiti wa Kijiji mimi nikachaguliwa kama Katibu wa kuandika mahudhulio ya wajumbe, wajumbe walikataa maana hatukuambiwa sababu za kumkataa tukakataa ikawa kosa.
"Chama kinaingilia halmashauri na kuweka makundi lile kundi lililoletwa na Chama kwenye halmashauri ndilo linaleta shida dhidhi ya kundi ambalo halipo kwa Mwenyekiti wa CCM Kata na Wajumbe wake.
" Mwandishi kinachosumbua ni maslahi, pale mtu anapotokea kuhoji jambo wanasema wewe ni mpinzani wa CCM, hata yule Mwenyekiti wa CHADEMA aliyesimamishwa uongozi hao viongozi wa CCM ndiyo walitengeneza njama za kumuondoa, wajumbe wakienda kwenye kikao wanafukuzwa wakati hawajapewa barua ya kukusimamishwa uongozi".
" Mkuu wa wilaya alikuja wakati wa Kuhamasisha sensa hatujawahi kumuona tena akija kuongea na wananchi wala kuzungumzia swala la Mwenyekiti na wajumbe waliosimamishwa uongozi na Chama.
"Madaktari wawili waliletwa kwenye hii Zahanati na bajeti zikatolewa kwa ajili ya kufanya usafi zahanati ianze lakini hakuna huduma tangu waganga walipoletwa miezi 6 iliyopita na mganga mmoja kaondoka baada ya kuona hakuna kinachoendelea" anasema Juma.
Habari zilizoifikia DIMA Online zinaeleza kwamba baada ya Zahanati hiyo kuripotiwa kwenye chombo hiki cha habari huduma ya afya imeanza kutolewa.
Mazumbe Nyambika Sondobi aliyewahi kuwa mjumbe wa Serikali ya Kijiji hicho anasema" Mwenyekiti wa Kijiji amejitahidi kupigania maendeleo mfano ujenzi wa shule hatuna majengo yakutosha, aliingia akakuta mradi wa maji umestisha huduma lakini akasimamia ukaanza kutoa maji.
"Wabaya wakayumbisha uongozi wake migogoro ikaibuka Kamati ya maji aliyoiunda ikavunjwa kwa nguvu za wenye pesa wakaweka wajumbe wao hadi sasa zaidi ya miezi mitano hatuna maji wanasingizia mafuta ya dizeli yamepanda bei wakati kamati mpya iliyochaguliwa imeshindwa kusimamia mradi maji hayatoki na pesa hazijulikani zimefanya nini wakati wananchi walikuwa wanachota maji.
"Wenyeviti wakichaguliwa hawamalizi muda ni miaka miwili au mitatu anasimamishwa, hadi sasa huyu ni Mwenyekiti wa tatu kusimamishwa kwa awamu mfululizo sasa sijui nini tatizo.
"Mwandika, John,Julius Kawembe hawa walimaliza muda wao lakini Mzee Zabroni, Togoro na Magige wamesimamishwa hawakumaliza muda wao, " anasema.
Anaongeza " Kamati ya siasa haishirikishi wananchi kwenye uondoaji wa Wenyeviti wanaanzisha migogoro ambayo tunaisikia pembeni sisi wananchi hatuambiwi, wamemkaimisha Mjumbe kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji kwa kushirikiana na Diwani badala ya kukaimishwa Mwenyekiti wa Kitingoji.
"Diwani anaingilia mambo ya Kijiji amekuwa chanzo cha migogoro, kuna fedha ililetwa na Serikali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi, wananchi hatukuambiwa hizo fedha wala kujua matumizi yake" anasema.
" Uongozi wa Mwenyekiti tulikaa mkutano mara mbili migogoro ikaanza baina ya viongozi wa Chama na Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti aliyeondoka kwenye uongozi wake lilichimbwa shimo la choo, alipokuja huyu akaendeleza nae amekwamishwa na mwenye sheli ambaye ni afisa mifugo Kata.
"Kijiji kilimuuzia eneo lake, wakati anapata hilo eneo sisi tulipima na Serikali ya Kijiji akaweka sheli aliomba ukubwa wa eneo 16/8 ambalo halifiki kwenye choo, tulimpa kama mwekezaji wa ndani lakini kijiji hakinufaiki.
"Mnara wa Vodacom tangu umesimikwa hatujawahi kuona mapato yake Kwenye Kijiji wameshindwa hata kujenga madarasa shule iliyojirani na mnara, shule ya Sekondari maabara hakuna, tulichanga fedha zikaliwa na mtendaji aliyesimamishwa kazi kabla ya kuja Mtendaji tuliyenae sasa, naye kaendeleza yaleyale miradi inajengwa chini ya kiwango"anasema Mzumbe.
Jumanne Francis ni Barozi Kitongoji cha Rwamakore anasema " Tunasikitika tunapoletewa jina la mtu aliyeteuliwa na Viongozi fulani ambaye hajachaguliwa na wananchi, Wenyeviti wakichaguliwa hawamalizi muda wa miaka 5 tunajiuliza sana wanaondoshwa na Chama alafu kinamteua Kaimu Mwenyekiti.
" Kwanini wananchi hatushirikishwi kuwa kuna Mwenyekiti mwingine wakati Chama hicho ndio kilituletea Mwenyekiti waliyemsimamisha tukampigia Kura, kwanini kinapomsimamisha akiwashirikishi wapiga kura kuwaambia kuwa wamemsimamisha na hatujawahi kuletewa kumjadili.
" Hata mimi nimesimamishwa na CCM Tawi kwamba mimi nashirikiana na CHADEMA, sijawahi kupewa barua yoyote, wananchi wananitambua kama barozi wao lakini Chama hakinitambui na wananchi hawajanikataa" anasema Jumanne.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango Fatuma Charles alipoulizwa kuhusu miradi ya ujenzi akasema "Nipo shambani siwezi kuzungumza nitafute baadae".
Alipotafuta kwa siku mbili aliendelea kugoma kuzungumza akidai kwamba hawezi kuzungumza yupo shambani.
Adaka Paul Winyanya aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mirwa 2009-2014 anasema viongozi hao wa Chama wanachangia kuwepo upinzani ndani ya Chama.
"Hata Kijiji cha Mirwa kuna migogoro kati ya Chama na Serikali ya Kijiji na wanaosababisha migogoro ni viongozi wa Chama ndiyo chanzo cha migogoro.
"Hata wakati nagombea Katibu wangu wa tawi alininyima fomu, wananchi wakasema Chama siyo cha Katibu nenda upande wa pili nikaenda nikagombea nikashinda"anasema Adaka.
Adaka anakiomba Chama cha Mapinduzi kutotumia kigezo cha usimamizi wa Ilani kunyanyasa viongozi Serikali za Vijiji kwani wao wapo kusimamia utekelezaji wa Ilani na kutoa maelekezo pale mambo yanapokwenda tofauti na siyo kugeuka kuwa viongozi wa Serikali za Vijiji na kuingilia majukumu ya serikali.
"Wanamwandama Mwenyekiti wa Kijiji wanasahau wagombea walikuwa 11 wakapitishwa watatu wakapigiwa Kura za maoni Magige akawashinda, lakini mara wamfungie ofisi, tatizo halijulikani tunashindwa kuelewa hapa kwenye Chama kuna nini.
Anaongeza kwamba wakati wa uchaguzi baadhi ya viongozi wa CCM huwa na makundi na kutosimamia vyema mwenendo wa Kura za maoni na uchaguzi jambo linalosababisha baadhi ya wanachama kukimbilia upinzani kugombea nafasi za uongozi baada ya kutotendewa haki kwenye Chama cha CCM.
Mmiliki wa Sheli azungumza
Mmiliki wa Sheli ya mafuta ambaye pia ni Afisa Mifugo Kata ya Mirwa Washington Benasius, amesema yaliyosemwa na Mazumbe Nyambika kuhusu kuuziwa eneo na kijiji, vipimo vya ardhi ni uongo na kwamba amekuwa akichangia maendeleo katika Kijiji hicho.
"Taarifa zilizotolewa na Mazumbe dhidi yangu ni uongo na upotoshaji kwa jamii, sijauziwa eneo ila nilipewa na halmashauri ya Kijiji baada ya kuomba, kama niliuziwa alete mkataba maana amesema alihusika kwenye upimaji, hivyo vipimo alivyosema ni vyake mimi nilipewa eneo futi 60/50.
" Mimi namiliki eneo kihalali, malalamiko yalipelekwa hadi Wizara ya afya yakafika kwa aliyekuwa Rais Hayati Magufuli uchunguzi ukafanywa na ikaonekana ni mmliki halali, sheli haitolewi ushuru kwenye kijiji, tunachokifanya ni kutoa huduma kwa jamii kama kujenga mahusiano.
" Anasema Kijiji hakinufaiki na huwepo wa kituo cha mafuta (Sheli) nimeshawahi kupeleka mifuko sita ya saruji Kitongoji cha Kamimange ikapiga lipu darasa moja shule ya msingi Magunga chini ya Mwenyekiti wa Kitongoji Kichomi, nimetoa mipira miwili shule ya msingi Magunga.
" Mtendaji wa Kijiji ana taarifa yote ya vitu navyochangia kwenye kijiji, mfano ule ujenzi wa Zahanati nilichangia mchanga tripu saba, ujenzi wa tenki la maji shule ya msingi Magunga nilichangia mifuko ya saruji,nilitoa nondo wakati wakufunga lenta Zahanati, kuna barabara zilikuwa korofi nikapeleka greda barabara ikarekebishwa.
Anaongeza " Shule ya Msingi Kamimange nilipeleka mifuko mitano ya saruji,Soko la Magunga vibanda vilikuwa vya majamvi mimi ndiye nilihamasisha wakajenga vya bati na sasa wengine wana maduka, aliyehamasisha ujenzi wa choo sokoni ni mimi Washington likachimbwa shimo gari yangu ikasomba udongo na vibarua kwa gharama zangu.
"Daraja la Mirwa lilikatika mimi na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mirwa tukahamasishana wadau wakajitokeza wakachangia nikatoa gari tukasomba mawe kwa gharama zangu daraja likapitika, pia nina gari linasaidia kusafirisha mihili ya Marehemu bure kwa familia zisizo na uwezo na wagonjwa wasio na uwezo.
"Kuna kikao kimoja tuliwahi kukaa ikaibuliwa hoja ya eneo Hilo na mhitasari ulisomwa ikionesha sijauziwa eneo ila nilipewa na Kijiji, tulikaa mkutano wa hadhara eneo la kanisa la wasababo Mwenyekiti wa Kijiji Magige akaibua hoja ya sheli kutolipa ushuru, wananchi wakakataa kuwa siwezi kulipa ushuru mambo nayofanya ni mengi.
"Huyo Mazumbe ni mkulima lakini hajawahi kutoa hata debe moja la mahindi kupeleka shule watoto watengenezewe uji, lakini mtumishi wa Serikali anapoonekana kufanya biashara anachukuliwa kama ni mwizi wa fedha za Kijiji na kujengewa chuki, kwakuwa mimi ni afisa mifugo wanadhani biashara zangu zinatokana na makusanyo ya mifugo kupitia kazi yangu ya afisa Mifugo"anasema Washington.
Ameongeza kuwa amekuwa akijitahidi kuchangamana na jamii katika kusaidia huduma mbalimbali na kumiliki sheli na ni msimamizi mzuri wa makusanyo ya ushuru wa mifugo huku akijipongeza kwa uhamasishaji mzuri katika kuhaikisa bucha za nyama zinajengwa kwa ubora.
Kuhusu mnara uliopo jirani na shule ya msingi Kamimange kutochangia huduma kwa jamii, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Mirwa Moris Onyango Odhiambo amesema.
"Suala la mnara wa Vodacom hawajawahi kuomba kwa muhusika ili achangie huduma kwenye Kijiji, hakuna hata barua waliyowahi kukiandikia Chama wakiomba kupata huduma itokanayo na mnara uliopo kijijini" anasema Moris.
Endelea kufuatilia DIMA Online kufahamu nini wasemacho wananchi kusimamishwa uongozi Mwenyekiti wa Kijiji.
Post a Comment