WAVUVI : RUSHWA, WANASIASA CHANZO CHA UVUVI HARAMU ZIWA VICTORIA
Na Jovina Massano, Musoma
IMEELEZWA kuwa sababu ya kuendelea kuwepo uvuvi haramu maeneo ya uvuvi likiwemo Ziwa Victoria ni kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya Maafisa Uvuvi huku Serikali ikishindwa kukomesha hivyo kusababisha uzalishaji wa rasilimali ya mazao ya samaki kupungua.
Pia Wanasiasa wametajwa kuwa sehemu ya kuchangia vitendo vya uvuvi haramu kwakuwa wamekuwa wakiwatetea wavuvi haramu pindi wanapokamatwa.
Wanasiasa Kanda ya Ziwa wameombwa kutowatetea wavuvi haramu pindi wanapokamatwa ili kusaidia rasilimali ya mazao ya samaki kuendelea kuwepo.
Hayo yameelezwa katika kikao Cha wadau wa uvuvi na Serikali kilichofanyika hivi karibuni Februari 26/2023 katika ukumbi wa Musoma Club uliopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Kikao hicho kilihudhuliwa na wajumbe 66 kutoka wilaya za Rorya, Musoma vijijini, Musoma Mjini na kanda ya Ukerewe wakiwemo na wawakilishi kutoka Jeshi la Polisi mkoa wa Mara na mkoa wa Polisi Tarime Rorya.
Mjumbe kutoka Wilayani Rorya Joseph Onyesi jina maarufu Akudo, amesema kuwa kikao hicho ni cha wadau wa samaki na serikali kwa maana ya viongozi wa Mkoa na Wilaya na kwamba waliomba wawepo lakini hawakufika zaidi ya Jeshi la Polisi waliotuma wawakilishi.
Ameongeza kuwa walitamani kuwaona na viongozi wengine wakifika kuwasikiliza wananchama kwani lengo ni kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa.
" Ili rasilimali hizi zisiondoke ifanyike utaratibu wa kudhibiti nyavu haramu aina ya giza ambazo zinatumika kutegea samaki ni hatarishi kwa mazao ya samaki tunaomba hatua kali zichukuliwe ziwa lifungwe miezi sita, tunaomba Jeshi la wananchi wafanye doria ili kunusuru rasilimali hii wavuvi haramu tunawafahamu waondolewe"amesema Joseph.
Ameongeza kuwa wamekua wakiiomba Wizara husika ifike kupata taarifa na kudhibiti uvuvi haramu lakini hawaonekani.
"Wanakiona Chama cha Wavuvi ni wahuni wakati mfugaji akiingia mbugani tu anadhibitiwa kwa nini isiwe katika ziwa kama kweli serikali inahitaji kuendelea kukusanya mapato basi hatua zichukuliwe kwa haraka ili rasilimali hii isipotee.
Nae Abdalla Ulega amesema serikali inachangia uvuvi haramu
kwa kushindwa kudhibiti rushwa katika Ziwa Victoria ambayo imekithiri kwa baadhi ya maafisa uvuvi wanaokusanya mapato ya halmashauri na kushindwa kusimamia sheria zinavyoelekeza.
"Mimi naongelea ziwa lote Luhanga Mpina alipokuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi aliweza kudhibiti uvuvi haramu ukapungua, hivi sasa viongozi wanaongea kwa kuminyaminya maneno wanahofia kutopigiwa kura, hili jambo linaumiza sana ukiangalia nchi jirani ya Kenya samaki hawapatikani.
" Hata mkoa wa Simiyu mazao ya Samaki hayapo hivi sasa wamevamia kuja ukanda huu wa Ukerewe na Mara, siasa ndizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kwa kuwatetea wavuvi haramu pindi wanapokamatwa wasiwatetee tulinde rasilimali hii, amesema Abdalla.
Ameongeza kuwa chanzo kingine kinachochangia kukomaa kwa uvuvi haramu ni halmashauri kutofuata Sheria.
Akijibu hoja hizo Kaimu Mfawidhi Uvuvi Mkoa wa Mara, Ndosi Eliakunda amesema kuwa sheria imeelekeza kuwa mvuvi haramu anapokamatwa na kukiri kosa lake atatozwa faini na kurudishiwa vifaa vyake.
" Endapo mvuvi haramu akikamatwa na kukiri kosa lake atatozwa faini na kurudishiwa vifaa vyake akirudia zaidi ya mara tatu atafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria, amesema Ndosi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Matete Msimu Mgongo amesikitishwa kutokuwepo kwa viongozi wa chama na serikali kwa kuwa wao ndio wadau muhumu wenye majibu ya kero hizo na wasimamizi wa rasilimali.
"Sisi wavuvi tunakabiliwa na changamoto nyingi unyang'anyi wa samaki na mafuta ziwani,uvuvi haramu, uharibifu wa nyavu unaofanywa na Wavuvi wa dagaa,wizi wa nyavu na Mashine soko la samaki ambapo sasa kiwanda tulichokuwa tunapeleka samaki kimeanza kupunguza uzalishaji ukipeleka mzigo unalipwa kidogo kidogo hii inaumiza wavuvi", amesema Matete.
Mbali na malipo kuwa kidogo kidogo lakini pia kiwanda kimeanza kuondoa baadhi ya miundombinu ikiwemo chumba baridi kinachotumika kuhifadhia Samaki (cold room) na kupunguza wafanyakazi, hii yote ni kutokana na upungufu wa samaki ulipo uliosababishwa na uvuvi haramu ni vema sasa serikali ikachukua hatua za dharura kunusuru hali hii ameongezea Matete.
Hata hivyo Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi kutoka kitengo cha Ushirikishwaji jamii Isack Boniphace Katamiti ambae amemwakilisha Kamanda wa Jeshi la Polisi Mara Longnus Ntibashibamu, amewashauri wanachama hao kuhakikisha ratiba ya vikao vyao inakuwa siku ya kazi isiwe siku ya mapumziko.
Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi kutoka kitengo cha Ushirikishwaji jamii Isack Boniphace Katamiti
Amesema hiyo itasaidia viongozi kushiriki kikamilifu lakini pia amewaeleza kuwa kwakuwa wanautambua wajibu wao ni vema wakaunganisha nguvu ya pamoja ili kulinda rasilimali hiyo.
"Malalamiko yote yapo kwenye Wizara mtambuka kuna Uvuvi, TAMISEMI,Maliasili,Wizara ya Mambo ya ndani Kilimo,Mifugo na Mazingira katika vikao vyenu mhakikishe mnawaalika ili majibu yenu yapate majibu," amesema Isack.
Wanachama hao wameazimia kupeleka mwongozo wa kimaandishi ofisi ya Kamanda wa Polisi kwa kumtaarifu kuwa watakuwa na boti kwa ajili ya ulinzi katika maeneo yaliyo na uharibifu kwa wavuvi lakini pia wavuvi wa dagaa kupitia viongozi wao wakutane ili kushirikiana kukomesha uvuvi haramu.
Post a Comment