HEADER AD

HEADER AD

MAUAJI MGODI WA NORTH MARA PIGO KWA JAMII

Na Dinna Maningo, Tarime

HIVI karibuni Viongozi wa Serikali ya Vijiji 11 vinavyo pakana na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo katika Wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara nchini Tanzania, waliandika Taarifa ya kupinga wananchi kuuawa kwa kupigwa risasi.

Pia walipinga kuwapo vipigo na mateso vinavyosababishwa na askari wa Jeshi la Polisi wanaolinda mgodi huo. Taarifa iliyotumwa Mahakama kuu ya kisheria Ontario nchini Kanada.

Sababu ya viongozi kuandika taarifa hiyo, ni baada ya shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu nchini Uingereza la RAID, linalojihusiha na masuala ya haki za binadamu pamoja na kuibua vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu, kuripoti habari mbalimbali mtandaoni.

RAID imechapisha habari zikielezea ukiukwaji wa haki za Binadamu vikiwemo vipigo, mauwaji na mateso vinavyofanywa na Polisi wanaolinda Mgodi wa North Mara.

Watanzania 21 wanadaiwa kufungua kesi ya kisheria katika Mahakama Kuu ya Sheria ya Ontario dhidi ya kampuni kubwa ya madini ya Barrick Gold, yenye makao yake makuu nchini Kanada kwa ukiukwaji wa haki za Binadamu unaofanywa na mgodi wa dhahabu wa  North Mara uliopo nchini Tanzania. 


Watanzania hao wamefungua kesi wakiulalamikia mgodi wa North Mara kwa vitendo vya mauaji ya kikatili, Vipigo, mauaji ya kupigwa kwa risasi na mateso wanayodai kufanywa na Polisi waliokuwa wakilinda mgodi huo.

Taarifa ya Viongozi hao imeambatana na majina, saini na mihuri ya Wenyeviti wa Vijiji 7 Kati ya 11, ambao ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja, Bunini J. Bunini, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamwaga, Chacha Michael Babere.

Wengine ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyagoto, Mwita .M. Kirindo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakunguru, Chacha Makuri, Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru John M.Otunga, Mniko Magabe Kijiji Cha Kerende na Stephano Ng'weina wa Kijiji cha Msege.

Wenyeviti wa Serikali za Vijiji ambao majina yao na saini hayakuonekana kwenye taarifa hiyo ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mjini Kati Paul Isack Bageni,  Daud Itembe Kijiji cha Matongo, Mgaya Ryoba Kisire Kijiji cha Nyabichune na  Nyamaganya Marwa wa Kijiji cha Komarera.

Wenyeviti hao wanatokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) Chama tawala kilichopo madarakani pamoja na Watendaji wa Serikali za Vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wapatao 11 na Watendaji wa Kata wanne kati ya Kata tano zinazopakana na mgodi.

Kata hizo ni Kemambo,Nyamwaga, Nyarokoba na Kibasuka, isipokuwa Mtendaji Kata ya Matongo katika fomu halikuonekana jina lake na saini.

Viongozi wa Vijiji wameeleza kusikitishwa na uchapishaji wa habari mbalimbali unaoendelea kupitia mtandao wa RAID na kueleza kuwa ripoti hizo ni za uongo na za kudhalilisha.


"Kama wawakilishi wa jumuiya ya wenyeji kutoka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi, tumefanya kazi na mgodi ili kuhakikisha uzingatiaji thabiti wa masuala ya haki za kibinadamu na heshima na jumuiya ya watu wa eneo hili.

 "Ripoti zao zinasema wamefanya misheni mbili za utafiti katika vijiji vyetu mnamo Mei 2022 kuhusu masuala ya mashambulizi toka kwa vyombo vya usalama na kusababisha mauaji. 

"Wamesema walipokea ripoti za kuaminika za wakazi wa eneo hilo kwamba kuna watu waliouawa na kushambuliwa na operesheni za vyombo vya usalama kati ya Februari na Julai 2022" Taarifa imeeleza. 

Taarifa hiyo inaongeza "Wamezidi kudai kwamba watu wawili waliuawa na angalau wengine kumi kujeruhiwa vibaya baada ya vipigo, kupigwa risasi na kuteswa.

"Maafisa wa Polisi wanaolinda mgodi mara kwa mara huingia kwenye jamii na kurusha risasi za moto na mabomu ya machozi ovyo, kuvunja mali bila kibali, kuwakamata na kuwapiga wakazi kiholela na kusababisha uharibifu wa mali.

"Tunaweza kusema kwa majigambo kwamba, mgodi wa North Mara unazingatia na kudumisha kwa dhati kanuni za haki za binadamu na utu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa serikali za mitaa zinashiriki katika usalama na ulinzi wa shughuli na mali za mgodi" Imeelezwa kwenye Taarifa.

Viongozi hao wa vijiji wamesema kwamba vyombo vya Habari, Asasi za Kiraia (NGOs) vinavyofanya kazi ndani ya nchi ya Tanzania na serikali ya Tanzania havijaripoti wakati wowote, wala kugusia masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu, yakiwemo mauaji kufanywa na askari Polisi wanaolinda mgodi wa North Mara dhidi ya wananchi wanaoishi kandokando ya mgodi huo wakati wowote.

Waliouawa Mgodi wa North Mara

DIMA Online imefanya uchunguzi kwa baadhi ya Vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara kupitia vyanzo mbalimbali vya habari na kubaini baadhi ya wananchi waliouawa kwa kupigwa risasi, waliojeruhiwa kwa risasi, vipigo vilivyo tendwa na askari Polisi wanaolinda mgodi wa North Mara.

Baadhi yao ni Wilfred Itama Machera mkazi wa Kijiji cha Nyabichune aliyezaliwa Machi,22, 2002 na kuuawa kwa kupigwa risasi Machi, 13, 2022, Isaack Maswi mkazi wa Kijiji cha Komarera aliuawa kwa kupigwa risasi Machi, 2022.

Emmanuel Daniel Nyakina mkazi wa Kitongoji cha Masinki Kijiji cha Nyabichune alizaliwa Julai, 01,2002 aliuawa kwa kupigwa risasi Julai, 14, 2022, Bahati Kirindo Matiko aliyezaliwa 2001, mkazi wa Kitongoji cha Masinki aliyeuawa kwa kupigwa risasi Desemba, 01,2022 na Samwel Matiko Irondo aliyezaliwa Agasti, 09, 1997, mkazi wa Kitongoji cha Masinki aliuawa kwa kupigwa risasi Julai, 14, 2021 eneo la Teringi.


Wengine ni  Mhere Ikaya Mgaya mkazi wa Kitongoji cha Kemachale alizaliwa Agasti, 15,1993, alifariki Februari, 26, 2022 alifariki baada ya kudondokewa na jiwe wakati akikimbizwa na Polisi Mgodini.

Mwita Joel Ghati mkazi wa Kitongoji cha Masinki alizaliwa Mei, 19, 1999 alifariki Desemba, 30, 2020 kwa kupigwa risasi, Juma Kuro Mkazi wa Kitongoji cha Kwimange alizaliwa Juni, 20, 1997, alifariki kwa kupigwa risasi Julai, 03, 2019.

Wengine ni Cosmas Luben Kirindo mkazi wa Kitongoji cha Masinki aliyezaliwa Julai, 01,2002, aliyefariki Desemba, 03, 2019 baada ya kutumbukia Kwenye rambo la maji wakati akifukuzwa na Polisi.

Matiko Mwita Gaigiri mkazi wa Kitongoji cha Kwimange aliyezaliwa Mei,29,2000 na kufariki kwa kupigwa risasi Machi, 15, 2021, Magige Gesabo mkazi wa Kitongoji cha Nyamanche Kijiji cha Nyakunguru aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka 2011.
 
Makuri Mahili aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka  2017, Mwita Chenche alipigwa risasi ,Keng'anya Marwa maarufu Madini aliyevunjika mguu baada ya kuangukiwa na jiwe akiwa anafukuzwa na askari Polisi waliokuwa wanalinda mgodi mwaka 2016.

Pia Nyangi Chacha aliyepooza sehemu ya mwili baada ya kuteleza wakati akikimbizwa na askari waliokuwa wanalinda mgodi maarufu Mobile mwaka 2018 ambao ni wakazi wa Kijiji cha Komarera.

Wengine ni Mhono Marwa Gibare mkazi wa Kitongoji cha Kegonga 'B' alizaliwa Juni,18,1984 alifariki Mei, 23,2009, Jack Black mkazi wa Kijiji cha Murito alizaliwa Machi, 26, 1991 na kufariki Septemba, 19, 2018.

Mahara Mwita aliyezaliwa 1996 aliuawa mwaka 2015 kwa kupigwa risasi na Polisi kisha mwili wake kutupwa kwenye shimo lililokuwa na maji. Alitambuliwa siku ya tatu baada ya mwili wake kuelea juu ya maji na kuopolewa.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Tarime Rorya Lazaro Mambosasa alifika na kushuhudia tukio hilo.

Msonzo  Christopher mkazi wa Kijiji cha Kewanja aliuawa kwa kupigwa risasi na Polisi kisha kuvamia mazishi yake na kuwapiga mabomu waombolezaji wakitaka familia pekee izike ili kupunguza msongamano kwakuwa familia ya marehemu walikuwa wanaishi jirani na mgodi mita 200.

Paul Sarya, Mwita Werema wakazi wa Kijiji cha Nyangoto waliuawa kwa kupigwa risasi, Matiko Mwita Gairigi mkazi wa Kitongoji cha Kwimange alizaliwa Mei, 05,2000 alifariki kwa kupigwa risasi Machi, 15, 2021.

Matiko Mwita Ketomwe alijeruhiwa kwa kupigwa bomu mkononi mwaka 2021 na hivyo kukatwa mkono, Chacha Marwa Mirumbe alijeruhiwa kwa kupigwa risasi mwaka 2022 ambao ni wakazi wa Kitongoji cha Kegonga 'A' na Kegonga "B' Kijiji cha Matongo.

Wengine Waliojeruhiwa ni, Nyaseba Matiko Irondo, Nyaheri Marwa Nyakorenga, Ezron Mwita Taban, Kemori Mwise Gasaya, Mwita Matoka Mniko, Baraka Nyamhanga Mahita alijeruhiwa kwa kupigwa risasi jichoni na kupata ulemavu wa jicho. Marwa Mwita Nyantento, Marwa Juma, Marwa Mwita Nyamhanga na Kisiri Isack Bageni wakazi wa Kijiji cha Mjini Kati.

Mwaka 2014  Polisi wakiwa wanafukuza watu walioingia mgodini, waliwafukuzwa kwa mabomu hadi shule ya msingi Nyabigena na kusababisha baadhi ya wanafunzi kupata majeraha baada ya kuanguka na wengine kung'oka meno wakati wakiwakimbia Polisi.

Habari zilivyo ripotiwa

DIMA Online imepitia baadhi ya Habari zilizo ripotiwa katika vyombo vya Habari vya nchini Tanzania na vyombo vya habari vya nje ya nchi hiyo zikielezea ukiukwaji wa haki za binadamu yakiwemo mauaji, migogoro ya fidia kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Baadhi ya viongozi wa Serikali ya Tanzania, Vyama vya kisiasa na Asasi za kiraia walifika katika vijiji vinavyozunguka mgodi kuzungumza na wananchi juu ya malalamiko ya mauaji, mateso, vipigo na fidia.

Miezi sita iliyopita baadhi ya vyombo vya habari viliripoti habari kuhusu wananchi kuuawa kwa kupigwa risasi yaliyotekelezwa na askari Polisi wanaolinda mgodi wa North Mara.

Aprili, 2022 Mwanamke mmoja mbele ya Waziri wa Madini Doto Biteko aliyefika Nyamongo baada ya kupasuka bomba la maji la mgodi, alimweleza kuhusu wananchi kupigwa risasi na Polisi wanaolinda mgodi licha ya sheria za Tanzania kutaka mtu anayekosea kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo na sio kujichukulia sheria mkononi.

Mwanamke huyo alilaumu kuwa Serikali inachangia kuwepo mauaji kwakuwa haiwachukulii hatua askari wanaovunja sheria lakini pia akasema Serikali iliahidi kujenga chuo cha Veta ili vijana wajifunze ufundi.

Alisema lengo la chuo kujengwa ni kuwaepusha kwenda kuokota mawe yenye Dhahabu katika mgodi huo unaosababisha wapigwe risasi na Polisi na wengine kujeruhiwa, lakini chuo hakijajengwa.

Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, John Heche Januari, 2023 alisikika akilalamika kupitia vyombo vya habari juu ya vipigo vilivyotendwa na Polisi kwa wananchi wa Kijiji cha Komarera na kubomoa nyumba zao wakiwa hawajalipwa fidia ambao walifanyiwa uthamini na mgodi.

                 John Heche

Machi, 7,2017 chombo cha habari cha Kimataifa kiliripoti makala ya utafiti iliyoangazia athari za vipigo,mauaji kwa watu wanaoishi karibu na mgodi wa North Mara. Mwaka 2022 ziliripotiwa habari za wananchi kubomolewa nyumba zao katika Kijiji cha Komarera kata ya Nyamwaga bila kulipwa fidia.

Novemba, 2013 ilichapishwa habari ya aliyekuwa Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye kwa sasa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alifika eneo la Nyamongo kusikiliza kero za wananchi.

             Nape Nnauye akizungumza na Wananchi Nyamongo mwaka 2013

Wananchi walimweleza kero zikiwamo za unyanyasaji wa Polisi, ukiukwaji wa mikataba baina ya wawekezaji na vijiji, utaratibu ulivyo mbovu wa kuhamisha na kuwalipa fidia wakazi wanaoishi kando kando ya mgodi, na utiririshaji wa maji yanye kemikali kutoka mgodini kwenda mto Mara.

Katika mkutano huo aliyekuwa Mkurugenzi wa kushughulikia malalamiko dhidi ya Jeshi la Polisi , Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji, Agustine .D. Shio aliahidi kushughulikia kero kuhakikisha haki inapatikana.

Julai, 2014 gazeti moja lilichapisha habari yenye kichwa cha habari kisemacho Waziri Chikawe, IGP Mangu na changamoto za usalama Tarime.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mathias Chikawe akiwa ameongozana IGP Ernest Mangu na Waziri kivuli wa Mambo ya Ndani, Vicent Nyerere aliyekuwa Mbunge wa Musoma mjini kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na viongozi  wengine walifika Tarime.

      
     Viongozi wakiwa Nyamongo mwaka 2014

Viongozi waliongozana na baadhi ya viongozi wa Serikali mkoa wa Mara na Tarime akiwemo aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Tarime John Henjewele na aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya Lazaro Mambosasa.

Viongozi hao walifika Nyamongo kujua sababu za kutokuwapo kwa usalama katika eneo la Nyamongo na wakazungumza na aliyekuwa Kaimu Meneja wa mgodi wa Afrika Barrick Gold Mine (ABG) ambaye alikuwa pia Meneja machimbo Jimmy Ijumba.

Ni baada ya kuwapo malalamiko ya wananchi wanaopakana na mgodi kuwalalamikia askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakilinda mgodi kwa kuwanyanyasa, kuwapiga, kuwajeruhi kwa risasi na wengine kuuawa.


Novemba, 11, 2014 chombo kimoja cha habari likiripoti habari ya Baraza la Wanawake kupitia Chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilichopo nchini humo, lilimtaka mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuchukua hatua za haraka za kudhibiti mauaji ya kikatili na kinyama yanayoendelea katika eneo la mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Septemba, 2012, Vyombo vya Habari vilichapisha mauaji ya watu wawili waliouawa kwa kupigwa risasi na Polisi kwa tuhuma za uvamizi wa mgodi. 

Septemba, 2012, zilichapishwa Habari za watu sita kujeruhiwa kwa kupigwa na mabomu ya machozi wakiwa majumbani kwao jirani na mgodi huo uliokuwa unamilikiwa na Kampuni ya ABG.

Mei, 2011 Vyombo vya habari nchini humo vilishapisha na kuripoti mauaji  ya watu watano na wengine kadhaa kujeruhiwa, waliopigwa risasi na Polisi waliokuwa wanalindana mgodi huo uliokuwa ukimilikiwa na Kampuni ya Afrika Barrick Gold (ABG) waliodaiwa kuvamia mgodi na kisha maiti zikiwa ndani ya majeneza kutelekezwa barabarani.

            Wananchi wakishuhudia moja ya jeneza likiwa na maiti lililotelekezwa barabarani mwaka 2011

Mei, 2011, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Nyambari Nyangwine (CCM) msafara wake ulipondwa mawe na wananchi wakidai ameshindwa kutoa kauli juu ya unyanyasaji wa Polisi na mauaji ya watu watano katika mgodi huo.

Hali hiyo ililazimu Serikali ya nchi hiyo kuunda timu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  na Jeshi la Polisi kufuatilia mauaji ya watu watano ambapo aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki alisema Serikali imechukua jukumu hilo kwasababu waliokufa katika tukio hilo ni Watanzania.

Juni, 2011, Habari zilichapishwa na kuripotiwa kwenye vyombo vya habari juu ya wabunge wa CHADEMA walioleza kumshtaki Spika wa Bunge Anne Makinda katika Kamati ya Kanuni za Huduma za Bunge, wakimtuhumu kumkingia kifua aliyekuwa Waziri mkuu, Mizengo Pinda asiwajibishwe na Bunge.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Spika Makinda kuzuia kujibiwa kwa swali la aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) Tundu Lisu kuhusu sababu za Serikali kutowafikisha mahakamani askari Polisi waliohusika katika mauaji ya watu 72 yaliyofanyika mwaka 2008-2011 katika mgodi huo.

                     Tundu Lisu

Juni, 2011, chombo kimoja cha habari kiliripoti habari yenye kichwa cha habari kisemacho ' Toronto wakumbuka waliouawa North Mara 'ambapo watu 70 walikusanyika nje ya chuo kikuu cha Toronto, Munk shool of Global Affairs kwa ajili ya kumbukumbu ya mauaji ya Raia saba yaliyotokea 2011 katika mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliokuwa unamilikiwa na Barrick.

Juni, 2011 ilichapishwa habari katika chombo kimoja cha habari iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho 'Uko wapi uhuru wa habari Tanzania ? wakati huo Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ikiongozwa na Dkt. Emmanuel John Nchimbi.

Habari iliyokuwa ikizungumzia namna Waandishi wa Habari walivyokamatwa wakiwa wanafuatilia sakata la Polisi kudaiwa kutorosha miili ya marehemu alfajiri saa 11 ikiwa kwenye majeneza, 

Miili hiyo ilikuwa imehifadhiwa katika hospitali ya Wilaya Tarime, ambao waliuawa kwa kupigwa risasi na Polisi katika mgodi huo.

 Juni, 2011 ilichapishwa Habari kuhusu Polisi Nyamongo kudaiwa kukamata ovyo wananchi bila makosa na kuwabambikiza kesi ya uvamizi wa kutumia silaha hali iliyowafanya wananchi kuyakimbia makazi yao.

Machi,25, 2011 ilichapishwa habari ikieleza sababu za wananchi Nyamongo kuvamia mgodi zikiwamo sababu za ukosefu wa ajira, ukosefu ardhi ya kilimo na ufugaji baada ya mgodi kuchukua maeneo kwa shughuli za mgodi.


Pia mgodi kuwa karibu na makazi ya watu hivyo wananchi kushawishika kwenda kuokota mawe ya dhahabu, mgodi kuchukua mashimo ya watu binafsi ya uchimbaji wa dhahabu.

Mashimo ambayo yaliyotumiwa na wananchi kuchimba Dhahabu, hivyo kukosa mahali pa kupata kipato na kulazimika kuingia mgodini kutafuta mawe yenye Dhahabu ili wakauze wapate fedha za kujikimu .

Septemba, 2012, Mtafiti kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Shirika lisilo la kiserikali lililopo nchini Tanzania, Onesmo Ole Ngurumwa kupitia vyombo vya Habari alisema zaidi ya watu 30 walijeruhiwa na askari wa Jeshi la Polisi katika mgodi wa ABG kwa kipindi cha kuanzia 2009-2012 mauaji yanayoendelea kila mara.

Vilio vya fidia

Mgodi wa North Mara umekuwa ukitoa matangazo kwa wananchi ya kuwataka kustisha shughuli za kimaendeleo kwa ajili ya kufanyiwa uthamini lakini hukaa miaka kadhaa bila kufanya tathmini na wafanyapo tathmini huchelewa kulipa fidia hali inayosababisha wananchi kuyaendeleza maeneo yao.

Mei, 20, 2020, Serikali kupitia vyombo mbalimbali ilitangaza kuwa wakazi 1,639 wa Vijiji vya Matongo na Nyabichune wamelipwa fidia jumla ya Tsh.Bilioni 33 baada ya kusubiri kwa miaka 10.

Mei, 02, 2021, ilichapishwa Habari yenye kichwa cha habari kisemacho ' Wananchi walalamika kwa Waitara walivyosotea fidia zao mgodi wa North Mara'. 

Wananchi wa Kijiji cha Nyakunguru walilalamika mbele ya mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara kuchelewa kulipwa fidia za mali zao kwa miaka minane baada ya kufanyiwa tathmini ili kupisha shughuli za mgodi.

                           Mwita Waitara

Februari, 2016, ilichapishwa habari ambayo wananchi walimweleza kero aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospiter Muhongo. Wananchi wanaoishi jirani na mgodi uliokuwa unamilikiwa na Kampuni ya ACACIA.

Wananchi wakilalamika kutolipwa fidia na hivyo kuathiliwa na mabomu ya machozi yanayopigwa na Polisi wanaolinda mgodi, maji ya sumu kutoka mgodini yaliyoathiri afya za watu na mifugo, watu waliofanyiwa uthamini kuchelewa kulipwa fidia pamoja na malipo kidogo ya fidia.

         Prof. Sospiter Muhongo akizungumza wa wananchi Kijiji cha Matongo mwaka 2016

Juni, 2016, zilichapishwa habari juu ya wakazi 1,500 wanaoishi jirani na mgodi huo uliokuwa ukimilikiwa na Kampuni ya ACACIA waliandamana hadi mgodini kudai fidia, ambapo Polisi waliwatawanya kwa kuwapiga mabomu ya machozi, kumwagiwa maji ya kuwasha na vipigo.


Ni baada ya wananchi kusimamisha shughuli za mgodi huo kwa zaidi ya saa tatu kwa lengo la kushinikiza mgodi kuwalipa fidia nyumba zao na mali zingine zilizofanyiwa uthamini tangu 2012.

Juni, 19,2017 Chombo cha habari cha Kimataifa kiliripoti habari ya idadi kubwa ya wananchi kukusanyika katika mgodi wa North Mara kwa siku mbili mfululizo kushinikiza walipwe fidia kutokana na kile walichodai kufanyiwa madhira.

Kumekuwepo malalamiko kwa miaka kadhaa tangu wawekezaji kuwekeza mgodi wa North Mara kwamba mgodi unapofanya uthamini hukataa kuhesabu baadhi ya mali.

Mgodi hudai kuwa wananchi wamejenga nyumba au kuotesha mimea na mazao baada ya kutolewa matangazo ya zuio maarufu ' Tegesha' na hivyo kutolipa fidia na wengine kulipwa fidia kidogo.

Novemba, 6, 2022 Kupitia Tovuti ya Serikali ya Wizara ya Madini Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa aliagiza wanaodai fidia mgodi wa North Mara kuwasilisha vielelezo ofisi ya madini alipokuwa ziara Tarime.

Mgodi huo umekuwa ukilalamikiwa kuwa unapofanya uthamini huchelewa kwa miaka kadhaa kulipa wananchi fidia licha ya kuwastisha kuendeleza maeneo yao.

Pia malalamiko ya ulipaji wa malipo usio sawa ambapo viwango vya malipo havizingatii mwongozo wa uthamini na ulipaji fidia, huku wenye ardhi ndogo wakilipwa fedha nyingi isiyoendana na uhalisia, waliostahili kulipwa kwa haki wakipunjwa.

Baadhi ya wananchi wanaolalamikia mapungo ya malipo hushindwa kufungua kesi kwakuwa hukosa ushahidi wa mali kwakuwa baada ya malipo mgodi ubomoa nyumba na mali zingine kuondolewa kwenye ardhi, huku kukiwa na usiri wa mgodi kutowaonesha wananchi gharama wanazopaswa kulipa kabla ya kuwekewa fedha benki. 

Wananchi usainishwa fomu ya malipo pasipo kujua kiwango wanacholipwa na mali zao kama zinaendana na zilizo kwenye nakala wakati wa ufanyaji tathmnini. 

Hali hiyo upelekea baadhi ya wananchi kugomea malipo huku wengine wasioweza kufungua kesi wakilazimika kuchukua fedha licha ya kulalamikia viwango vya malipo.

Pia kumekuwepo na janjajanja nyingi wakati wa ufanyaji tathmini unaofanywa na maafisa wa mgodi kwa kushirikiana na Serikali na malipo ya fidia jambo ambalo baadae husababisha kuwepo na majina hewa au ardhi hewa zinazoainishwa kwa ajili ya malipo.

Baadhi ya maeneo kikiwemo Kijiji cha Kewanja, mgodi ulitoa matangazo ya kuchukua eneo na kufanya tathmini na kuahidi  kulipa fidia lakini baada ya miaka kadhaa Mgodi ulipunguza eneo ililotaka ekali 378 hadi 57 zilizokusudiwa na haukulipa wananchi fidia ya usumbufu.

Sababu za kupunguzwa ilielezwa kuwa ni fidia kufika Tsh. Bilioni 21ambapo mgodi ulitoa mfano shamba lenye pungufu ekali moja limeoteshwa miti 3,421 wakati kitaalam eka moja huoteshwa miti isiyozidi 640.  kuendeleza maeneo 

Tovuti ya Serikali ya mkoa wa Mara iliripoti kuwepo kwa ufisadi ulipaji wa fidia Nyamongo habari iliyochapishwa Juni, 15, 2020, taarifa ambayo ilitolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Taasisi hiyo ilibaini kuwepo kwa ufisadi wa Tsh. Bilioni 3.2 katika malipo ya fidia mgodi wa Barrick North Mara na kuwepo upendeleo katika ulipaji pamoja na majina hewa.

Septemba, 12, 2015 zilichapishwa habari kuhusu Kampeni za mgombea urais, Hayati John Pombe Magufuli ambaye alishinda na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwa Nyamongo wananchi walilalamika Serikali kushindwa kutatua kero zao zikiwemo za ukosefu wa haki katika malipo na uonevu.

Awali machimbo ya dhahabu yalimilikiwa na wananchi ambapo Serikali iliyakabidhi kwa wawekezaji na Kampuni za uchimbaji wa dhahabu kuwekeza, uwekezaji ulioanza mwaka 2002.

Kampuni zilizowahi kuwekeza mgodi wa North Mara ni Kampuni ya East African Gold Mine (EMGM), Kampuni ya Africa Mashariki Gold Mine (AMGM), PRASADOM, Barrick North Mara, ACACIA na sasa Barrick North Mara

Mwongozo wa Uthamini wa Fidia

Kwa mujibu wa mwongozo wa Serikali wa uthamini wa fidia wa march, 2016 uliotayarishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi unasema fidia ni malipo yanayotolewa kwa mtu au taasisi kama mbadala wa mali yake kutokana na kuondolewa kwenye eneo lake lililotwaliwa kwa manufaa ya umma na kupangiwa matumizi mengine tofauti na yale yaliyopo sasa.

Pia Kifungu cha 13(2) cha kanuni za sheria ya Ardhi Na.4 za mwaka 2001 na Kifungu cha 19(1)–(3) cha kanuni za Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na.5 za mwaka 2001 na kifungu Na.3(1) (g) cha Sheria ya Ardhi Na.4 ya 1999 na Kanuni zake pamoja na vifungu Na.(7-11) vya kanuni za Sheria ya Ardhi, 2001 vimeelekeza namna ya ulipaji wa fidia ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa wakati ndani ya miezi sita.







No comments